Na Kija Elias,JamhuriMedia,Same
Wanafunzi wa shule ya Sekondari Makokane iliyopo Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro, wameshindwa kwenda shule kutokana na makundi ya tembo kuingia katika kijiji hicho yakitafuta maji.
Kufuatia hali hiyo Wananchi wa kijiji hicho, wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia kuawa na tembo ambao wamekuwa wakitoka hifadhi ya Taiafa Mkomazi na kuingia katika makazi hao.
Diwani wa Kata ya Kalemawe Athuman Mbwero aliyasema hayo mwishoni mwa wiki kwenye kikao cha robo ya nne ya Baraza la Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Amesema kijiji cha Makokane wazazi wamekataa watoto wao wasiende shuleni kutoka na tembo kuonekana kwenye makazi yao na kuharibu mimea huku wengine wakiweka kambi barabarani.
“Kwenye kijiji changu cha Makokane wazazi wamekataa kuwapeleka watoto wao shule kutokana na kuhofia kuawa na tembo, hata sasa hivi nikiwa kwenye kikao hiki, nimepigiwa simu na Mwenyekiti wa kijiji changu kuwa bado watoto wako majumbani wazazi wamegoma kuwapeleka shule,”amesema.
Mbwero amesema “Tangu Serikali ilipotangaza kufunguliwa kwa shule nchini Septemba 5 mwaka huu, wanafunzi wa Kata ya Makokane wameshindwa kuhudhuria masomo yao kutokana na makundi makubwa ya tembo kutoka Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kuweka kambi katika kijiji cha Kalemawe na hivyo kuzuia wanafunzi kupita,”.
Hata hivyo Diwani huyo ameiomba Serikali kuweka kituo ambacho kitakuwa na askari wa wanyamapori watakaokuwa wakiwafukuza wanyama hao waharibifu pindi wanapowaona wanakuja hali ambayo itakuwa usalama wa wananchi hawa.
Naye Diwani wa Kata ya Ndugu Abedi Salehe Ally-amesema suala la tembo limekuwa ni changamoto kubwa kwenye kata ya hiyo, kutokana na wanyama hao kutoka mbuga ya Mkomazi na kuja kwenye Skimu ya Umwagiliaji Ndungu kutafuta maji.
“Tembo wamekula mazoa yote ambayo wananchi walikuwa wamelima jambo ambalo limesababisha wakulima kukata tamaa na suala zima la uzalishaji,”amesema Diwani Ally.
Akizungumza kwenye kikao hicho cha braza la Madiwani Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Anastazia Tutuba na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Yusto Mapande wamesema tembo wamekuwa ni changamoto kwenye halmashauri ya wilaya Same, licha ya juhudi mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na wadau wa wanyapori kuwarejesha tembo hao walikotoka lakini bado wamekuwa wakirudi.
“Tumekuwa tukifanya jitihada mbalimbali kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuhakikisha kwamba wanawatafuta wadau wa wanyamapori ili waweze kuja na kutoa elimu kwa wananchi,”amesema Tutuba.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Same Edward Mpogoro alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo ya wanafunzi kushindwa kwenda shule kutokana na kuhofia kuawa na tembo.
“Serikali tumeomba fedha kwa ajili ya kujenga mabweni kwenye kata zenye changamoto ya tembo, wakati tunasubiria fedha hizo za kujenga mabweni hayo, wanafunzi ambao wanatoka kwenye vijiji vya Makokane, Karamba waweze kilituma kama bweni,”amesema DC Mpogoro.
Aidha amesema kwa kipindi cha miaka miwili tembo wameongezeka kwa wingi baada ya Serikali kuwadhibiti majangili, jambo ambalo limewezesha tembo kuzaliana kwa wingi.