*Tume ya TEHAMA yafikiria Tuzo kwa wanahabari

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

WASHINDI wa kwanza wa Tuzo za TEHAMA 2025, wanatarajiwa kutangazwa rasmi leo katika hafla ya Tuzo hizo zinazotarajiwa kufanyika katika Hoteli ya Nyota Tano ya Gran Melia, jijini Arusha.

Katika Tuzo hizo zilizoandaliwa na Tume ya TEHAMA (ICTC) kwa kushirikiana na kampuni ya SoftVentures, Chama cha Watoa Huduma za Intaneti Tanzania (TISPA), Kampuni ya Ukaguzi ya Deloitte, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Jerry William Silaa(Mb).
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Moses Mwasaga, amethibitisha kukamilika kwa maandalizi ya tuzo hizo ambazo zinafanyika kwa mara ya kwanza nchini ikiwa sehemu ya kutambua mchango mkubwa wa uwekezaji,uundaji mifumo,utoaji huduma na ubunifu unaofanyika katika sekta ya TEHAMA.

“Tunalenga kutambua na kuchochea kasi ya ubunifu nchini ili kuhakikisha vijana na Watanzania kwa ujumla wanaonekana kitaifa na kimataifa. Tunataka Tanzania iwe shindani kwenye soko la kikanda na kimataifa ambako faida ni nyingi mno kuelekea katika uchumi wa kidigitali,” alisema Dkt. Mwasaga.

Katika tuzo hizo, zaidi ya washiriki 380 waliwasilisha kazi zao zilizochujwa kitaalamu na kuthibitishwa na Kampuni ya Deloitte ambayo imekuwa na jukumu la kutoa ushauri na usimamizi katika mchakato wa tathmini ya tuzo, kusaidia katika usimamizi wa utawala bora, kuchangia maarifa ya sekta ili kuendeleza mabadiliko ya kidijitali Tanzania, vyote vikilenga kukuza uvumbuzi, utawala bora na ukuaji endelevu wa kidijitali.


Washiriki hao walichuana katika vipengele 10, huku ushiriki mkubwa ukiwa katika vipengele vidogo 21 kati ya 22.

Maeneo makuu yaliyoshindaniwa ni Matumizi ya TEHAMA katika Elimu, Fedha, na Afya, Uvumbuzi wa Usalama wa Mtandao, Mbinu Bora za Ulinzi wa Taarifa, Teknolojia Zinazochipukia, Miradi ya TEHAMA katika Sekta ya Umma na Binafsi, Tuzo za Muunganisho wa Mtandao (Mtoa Huduma Bora wa Mawasiliano, ISP, na MNO), Utofauti katika Teknolojia (Mvumbuzi Mwanamke, Kiongozi wa Teknolojia Mwanamke, Ubora wa Wanafunzi).

Wakati hao wakichuana katika tuzo za mwaka huu, Dkt. Mwasaga amewashukuru waandishi wa habari kwa ushiriki wao katika kuuhabarisha umma juu ya habari za sekta ya TEHAMA.

Aidha, kwa kutambua mchango wao, amesema Tume ya TEHAMA inafikiria kuanzisha Tuzo Maalumu kwa Wanahabari wanaoandika, kuihabarisha na kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa sekta ya TEHAMA ambayo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasssan imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha Tanzania inajikita vyema katika kuujenga uchumi wa kidigitali ili iweze kuendana na kasi ya nchi nyingine duniani.