Leo nimeona nijiegemeze katika tasnia ya maigizo ya hapa Tanzania. Tangu kuwasili kwa utandawazi katika upwa wa Afrika Mashariki mwanzoni mwa miaka ya 1990s, kufunguliwa kwa milango ya soko huria, tasnia ya maigizo nayo haikuwa nyuma.
Mabadiliko makubwa tukaanza kuyashuhudia ikiwemo kujitokeza kwa sura mpya katika kazi hiyo, wengi wao wakiwa vijana ambao walikosa ajira na kuamua kujitumbukiza katika shughuli hizo.
Hivi sasa hapa nchini kuna utitiri wa vikundi vya maigizo ambavyo vimekuwa vikifanyakazi katika hali ambayo baadhi ya watu wameanza kulalamika kwamba vinakwenda kinyume na maadili ya Watanzania.
Lakini kabla ya kuingia kwa undani katika mzizi wa hoja yenyewe, ni vema nikaeleza tunapozungumzia maigizo ni nini hasa?
Kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili sanifu, imetafsiri maigizo kuwa ni sanaa katika fasihi simulizi ambayo watendaji huwa ndio wahusika.
Inaelezwa kwamba katika maigizo hayasimuliwi kama mbinu nyingine za fasihi. Bali wahusika ndio huzungumza katika sehemu zao mbalimbali kulingana na hadhira ambapo pia shughuli yenyewe ya maigizo inahusisha masuala ya mila,silka a utamaduni wa nchi.
Pia katika kundi hili, kuna vichekesho ambavyo navyo ni aina ya sanaa ya fasihi simulizi ambayo watu hutoa vihadithi vifupi au sentensi zenye uwezo wa kuifanya hadhira kupata burudani.
ya kuona kwa ufupi nini maigizo, sasa tuendelee katika mzizi wenyewe ambao ni kushamiri kwa hulka za “kihuni”, uvunjaji wa makusudi wa mila,desturi na utamaduni wetu kunakofanywa na hao wanaoitwa “ wachekeshaji” ambao sasa wameanza kuchukua mkondo mpya wa kuiga mambo ambayo hayakuwepo awali.
Katika baadhi ya maigizo, si ajabu tena leo kuwaona wahusika wanaume wakiwa wamevaa hereni, wamesuka nywele na wengine hata kutumia madawa ya kujibadili nyuso zao ili waonekane waupe ilhali wao ni Weusi kama chungu.
Afadhali ingeishia hapo, lakini matamshi watamkayo katika maigizo yao, yanakarahisha, yanatia kichefuchefu, yanayoweza kumtapisha msikilizaji,mtazamaji ambayo hayastahiki kutamkwa hadharani.
Watamkaji matamshi yao, hayana staha, hawatazami wanazungumza na nani na wapi. Inasikitisha na kukatisha tamaa kwamba sasa sanaa ya maigizo imevamiwa na imeshageuka kuwa “chaka la watoro”.
Kuna tofauti kubwa baina ya waigizaji wa kale na hawa wa kizazi kipya ambao sio wote,lakini wengi wao wanafanya vitendo vya utovu wa adabu hadharani kuanzia wao wenyewe na hata maigizo yao.
Sikutapata kusikia matamshi yenye kukarahisha enzi za akina Mzee Khamis Tajiri jina la usanii akiitwa Janja, Meneja Mikupuo, Fundi Said maarufu mzee Kipara, Ibrahim Raha,akijulikana kama Mzee Jongo.
Wengine ni Rajab Kitwana Hatia, jina la usanii Pwagu, Bi. Tunu Mrisho(Mama Hambiliki), Salum Tambalizeni na wengi ambao wametoa mchango katika kukuza tasnia hiyo hapa nchini.Sikuwahi kuwasikia watu wakilalamika kwamba kuna ukiukwaji wa maadili umefanywa siku hizo.
Leo huwezi kutazama igizo mbele ya watu unaowaheshimu, huwezi kutazama igizo mbele ya watoto wako, huwezi kutazama hata ukiwa peke yako maana utajikera na kuwakera wengine.
Vituko, visa na mikasa inayoambatana na ukosefu wa ubunifu, ujuzi ndio utakavyoshuhudia katika maigizo mengi yanayofanywa na hao waigizaji wanaojiita wa kizazi kipya.
Hivi karibuni, nilimsikia, Mzee Amri Athumani maarufu kama King Majuto akilalamikia mwenendo wa baadhi ya wasanii wa maigizo kuwa wanapotea katika kazi hiyo.
King Majuto, naye anajisikia kichefuchefu pale anapowaona wachekeshaji wanavyofanya mambo ambayo hayajapata kufanywa huko nyuma na ambao amewaita “wavamizi” wa tasnia ya maigizo.
Anaziona kazi zao kuwa zinakiuka maadili ya Kitanzania na kwamba vichekesho hivyo si tena vinaburudisha na kuelimisha, bali vinatia kinyaa kuviangalia!
Amesema kwamba baadhi wa wachekeshaji wanamchukiza kwa kufanya mambo ya aibu na kujidhalilisha wenyewe.
“Wapo vijana wanafanya kitu ukiangalia unafurahi na kwa sisi wachekeshaji wa siku nyingi unajifunza kitu, lakini hawa wavamizi ukiangalia unaweza kutapika. Sipendi na wananiudhi. Kama vipi wajipange upya,” amesema King Majuto.
Nimekuwa nikijiuliza hivi Baraza la sanaa Tanzania liko wapi, limekwenda likizo au halina meno? Nitakuwa mtu wa mwisho kuamini kama BASATA halina meno kwani tumeona katika baadhi ya mambo ukionesha nguvu zake,lakini katika hili la kudhibiti, kusimamia maigizo limewashinda kiasi cha wananchi kuanza kupiga kelele.
Basata limeanzishwa kwa mujibu wa Sheria Na. 23 ya Mwaka 1984 zinatoa uwazo wa kuzuia kazi yeyote ambayo inakwenda kinyume na maadili ya jamii. Kwanini basi mnashindwa kuvichukulia hatua vikundi ambavyo vinafanya vitendo ambavyo jamii haikubali?
Haiwezekani kila mwenye igizo lake akalisambaza mitaani na jamii kuanza kutazama ilhali maudhui yake yanapotosha umma, yanavuruga mila, utamaduni na pengine hata kuchochea vitendo visivyofaa.
Jamii nayo lazima ibadilike, ikatae kupokea kila kitu, umefika wakati kupembua, ipi ni igizo lenye kufaa kutazamwa na lipi halifai maana ni sisi wazazi ndio tunaowajibu wa kuhakikisha tunalinda maadili yetu.
Wazazi na walezi wasikubali kuona vijana wao wakitazama maigizo ambayo hayana maadili na wao kukaa kimya, wakemee kwa nguvu zote. Hatuwezi kuvumilia mwenendo huu ambao sio mwema.
Ziko nchi nyingi leo zinajuta baada ya kupuuzia mambo kama haya ambayo yanaonekana yanataka kuota meno ya juu. Wahenga wanatwambia, mchezea zuri baya umfika. Jamani tusichezee utamaduni wetu mzuri katika bahari yenye papa wakali, tunaumia sote.
Tanzania sio nchi ya ulimwengu wa bata, ikawa mama kufuata watoto ambao hawajui waendako. Tanzania ina heshima na sifa zake ambazo zinafanya sehemu muhimu ya utamaduni wetu.
Utamaduni ni moja ya nyenzo muhimu katika nchi yeyote ile. Tuna kila sababu ya kuhifadhi, kulinda na kuendeleza utamaduni wetu ambao umekuwa ni kilelezo cha umoja na mshikamano wetu. Wanayofanya hawa wasanii wasio na staha, tuyakatae.