Na Magrethy Katengu, Jamhuri Media, Dar es Salaam
WASANII wa Tasnia ya Filamu Tanzania (BONGO MOVIE) wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kauli yake ya kuanza kuwajumuisha Wasanii mbalimbali kwenye ziara zake rasmi nje ya mipaka ya Tanzania kwa lengo la kujifunza zaidi juu ya tasnia yao .
Rais Samia alitoa kauli yake ya kuanza kuwajumuisha Wasanii mbalimbali kwenye ziara zake rasmi nje ya mipaka ya Tanzania kwa lengo la kujifunza zaidi juu ya tasnia hiyo hivi karibuni alipohudhuria hafla ya uzinduzi wa Albamu ya Staa wa Muziki wa Bongo Fleva Harmonize aliyoiita “Muziki wa Samia”.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 29, 2024 jijini Dar es Salaam Muigizaji na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao Steve Nyerere amesema kuwa jambo hilo ni kubwa na wanazo sababu za kumshukuru Rais Samia.
Amesema kuwa wao kama wasanii watahakikisha wanaitumia fursa hiyo katika kujifunza, kulinda maadili na kuitangaza Tanzania vizuri kiutamaduni na kiutalii jambo ambalo litaivuta Dunia kuifahamu vyema Tanzania.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Waigizaji Tanzania Chiki Mchoma amesea kuwa kitendo hicho cha Rais Samia kinakwenda kuimarisha Tasnia ya Filamu Tanzania.
Aidha wasanii hao wametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya kwa Tasnia nzima ya Sanaa, Utamaduni na Michezo.