Kuna wakati nilikuwa najaribu kuangalia stahili ya maisha ya baadhi ya wasanii wa muziki kutoka katika nchi nyingine. Lengo langu lilikuwa ni kuangalia na kutafuta chanzo cha wasanii wetu kufanya mambo ambayo ni kinyume na maisha ya kibongo.

Maisha yako katika nyanja nyingi, katika hili nilikuwa nikiangalia ni jinsi gani wasanii wa Kitanzania wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kwa ile stahili ya ‘ndivyo sivyo’. Yaani kwa tafsiri ya haraka ni kwamba wanatumia mitandao hiyo vibaya.

 

Kama ilivyokuwa nchi nyingine, Wasanii wa Tanzania wanapenda kuishi maisha ya kifahari, hata kama uwezo wake ni mdogo. Kuna wasanii ambao wanapenda kuishi maisha ambayo ni kinyume na kipato anachoingiza kila siku. Hali hii inaweza kutafsiriwa kama tamaa.

 

Hali hiyo imewasababishia hali fulani ya kujikuta wakigeuka kero katika jamii. Hivi karibuni nilikuwa naangalia katika mitandao ya kijamii nikawa naangalia jinsi wasanii wanavyojivinjari katika mitandao hiyo kwa baadhi yao kuamua kuweka habari zao binafsi zisizokuwa na faida yoyote kwa jamii.

 

Sijui ni tabia ya kuiga? na kama ni kuiga kuna haja ya mtu kuiga mambo mabaya ambayo yanamtia aibu? Siyo nia yangu kujua kwanini hili linatokea, ila ni wazi kabisa kuwa wasanii wetu wameendekeza tabia ya kuiga ambayo itawapeleka pabaya. Kama kuna jambo ambalo linawakera baadhi wa wadau wa burudani, ni pale ambapo wasanii wetu wamekuwa na tabia ya kufanya mambo yao binafsi, alafu wanayaweka bayana katika mitandao ya kijamii.


Hii ina maana gani na inafundisha nini? Tatizo kubwa walilonalo wasanii wetu ni utumwa wa vitu vya kigeni. Na hii imetawala karibia kwa kila kitu wanachofanya.

 

Kuna haja ya wasanii wetu kutambua umuhimu wao katika jamii na hivyo kuitumia mitadao ya kijamii kwa kuelezea mambo ambayo yanajenga mwonekano wao wenye mfano wa kuingwa. Imekuwa jambo la kawaida wasanii kuweka picha za mavazi ambayo hayaendani na utamaduni. Mbaya zaidi ni pale baadhi yao wanapoamua kuanzisha mijadala ambayo haina kichwa wala miguu.

 

Kazi ya mwandishi wa habari ni kuelemisha, kufikisha ujumbe, lakini pia kuirekebisha jamii pale inapopotoka. Kwa hili wasanii wanatakiwa kujiangalia upya juu ya suala zima la mawasiliano kupitia njia ya mitandao ya kijamii. Kama hali inatendelea hivi kuna wakati baadhi yao watajipunguzia mashabiki kutokana na ule upuuzi wanaouandika katika mitandao ya kijamii.