Watanzania wanne wamehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kila mmoja, au kulipa faini ya Sh 5,000,000 kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la usafirishaji binadamu. Pamoja na adhabu hiyo, gari lililotumika kwenye biashara hiyo haramu limetaifishwa na litapigwa mnada.
Waliohukumiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Longido mkoani Arusha, ni Romani Tarimo (dereva), Samweli Mwashinga (dereva), Taritoi Laizer (kiongozi wa msafara) na Petro Kisima aliyekuwa kondakta.
Watu hao walifikishwa mahakamani hapo Desemba 17, mwaka jana, kwa kosa la biashara haramu ya usafifishaji wa binadamu chini ya Kifungu cha 5(2) (e) cha Sheria inayoharamisha biashara ya usafirishaji wa binadamu ya mwaka 2008 – The Anti-Trafficking Act of 2008.
Ingawa baada ya kusomewa kosa watuhumiwa hao walikanusha kuhusika, waliporejeshwa mahakamani Januari 2, mwaka huu, wote walikiri makosa yao na ndipo walipotiwa hatiani na kuamuriwa kutumikia kifungo cha miaka mitano au kulipa faini ya Sh 5,000,000 kila mmoja. Wote walilipa faini.
Wahamiaji haramu 96 waliokuwa wakisafirishwa walishitakiwa katika mahakama hiyo hiyo kwa kosa la kuingia nchini isivyo halali, chini ya kifungu cha 31(1) (i) na (2) cha Sheria ya Uhamiaji ya 1995.
Wote walikiri makosa yao na hivyo wakatiwa hatiani na kati yao wawili waliokuwa na umri wa chini ya miaka 18 waliachiliwa huru. Wengine 94 walipewa adhabu ya kulipa faini ya Sh 100,000 kila mmoja au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela. Wote walishindwa kulipa faini na hivyo wanatumikia kifungo.
Mahakama iliamuru gari lililokuwa limewabeba wahamiaji hao haramu litaifishwe, na kwa sasa lipo katika Kituo cha Polisi cha Longido. Baada ya siku 30 kupita tangu tarehe ya kutolewa hukumu, gari hilo litauzwa kwa mnada.
Awali, ilielezwa mahakamani hapo kuwa Desemba 14, mwaka jana, Watanzania hao wanne walikamatwa katika maeneo ya vijiji vya Tingatinga na Ngereyani wilayani Longido, wakiwa katika gari aina ya Fuso lenye namba T264 APV.
Walituhumiwa kwa kosa la kujihusisha na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu. Gari hilo lilikuwa limewabeba wahamiaji haramu 96 raia wa Ethiopia, na matenga kadhaa ya nyanya ili isigundulike kirahisi kuwapo kwa wahamiaji hao haramu ndani ya gari hilo.