*Jaji abariki wosia uliomweka pembeni mke wa ndoa, watoto 15

*Upande wa mlalamikaji washangaa Mahakama kudharau ndoa ya Kikatoliki

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutotambua cheti cha ndoa ya Kikristo umeacha maswali mengi na kuuduwaza upande wa walalamikaji; JAMHURI linaripoti.

Februari 7, mwaka huu, Jaji wa Mahakama Kuu, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Sharmillah Sarwatt, alitupilia mbali hoja za walalamikaji katika kesi ya mirathi ya mfanyabiashara maarufu wa Dar es Salaam, Joseph Mfugale, aliyefariki dunia Julai 31, 2021.

Sakata la warithi wa Mfugale kufika mahakamani linatokana na wosia alioundika mwaka 2015 kuhusu mgawanyo wa mirathi; wosia ambao haumtambui mke wake wa ndoa, Maulicia Mfugale, na sasa watoto wa mama huyo ambaye pia amekwishatangulia mbele za haki, wanataka apewe thamani yake walau tu kwa kutamkwa wazi.

Mfugale, ambaye pamoja na biashara nyingine alikuwa akimiliki Hoteli ya Peacock iliyopo Kisutu jijini Dar es Salaam, mwaka 1964 alifunga ndoa ya Kikristo ya madhehebu ya Kikatoliki na Maulicia.

Ni kwa sababu ya wosia huo, ndiyo maana Kalvarina Mfugale, msimamizi wa mirathi ya Maulicia, mke wa ndoa wa Mfugale, aliiomba Mahakama Kuu kusitisha utekelezwaji wa mirathi ya marehemu Mfugale.

Katika wasilisho lake kwa maandishi mbele ya Mahakama Kuu, wakili wa Kalvarina, Rabin Mafuru, aliiomba Mahakama itamke kuwa wosia wa Mfugale wa Septemba 16, 2015 ni batili na unapaswa kuwekwa pembeni kwa kuwa umeshindwa kukidhi matakwa ya kisheria.

“Kwamba Mahakama iridhie kusitisha mgawanyo mwingine au utekelezaji wa mirathi hadi uamuzi wa shauri hili utakapotolewa,” amedai Wakili Mafuru.

Shauri hilo Namba 24851/2024 lilifunguliwa na Kalvarina Joseph Mfugale dhidi ya Titus Mfugale, msimamzi wa mirathi upande wa marehemu Mfugale anayetetewa na Wakili Antipas Lakam.

Mwenendo wa kesi

Akiwasilisha maombi mahakamani hapo, mbali na hoja kwamba wosia husika haukidhi matakwa ya kisheria, Mafuru aliongeza kusema kwamba masharti huufanya wosia kuwa batili, akirejea kifungu cha 114 cha ‘Indian Succession Act, 1865’ kinachosema utekelezaji wa mirathi iliyoachwa kwa masharti ni kinyume na sheria na maadili.

Mafuru anadai kuwa katika wosia, Mfugale amewarithisha watoto wake watatu hisa za Peacock Hotel Limited kwa sharti kwamba watoto hao watawapa gawio wenzao (watoto wa mama wengine) litakalotokana na faida. Mfugale ameacha watoto 18.

Anasema hisa, kwa mujibu wa Ibara ya 24(1) ya Katiba, zinatambuliwa kama mali halisi, hivyo iwapo mtu atazipata kwa kurithi, anakuwa mmiliki halali mwenye haki na mamlaka ya kufanya atakavyo; na kwamba kuwapo kwa sharti la kugawa faida kwa wengine ni kinyume cha kifungu tajwa cha Katiba.

Katika pingamizi jingine, Mafuru amedai kuwa aya ya 11 ya wosia inaamuru kwamba wale waliorithishwa hisa lazima wazilipie ili watambulike kuwa ni wanahisa (wa Peacock Hotel).

Katika hilo, wakili Mafuru anasema linaingilia taratibu za ndani za kampuni zinazosimamia hisa na kwamba, maelekezo yaliyomo kwenye wosia yanakiuka sheria inayozisimamia kampuni; Companies Act, Cap 212.

Anaendelea kueleza ubatili wa wosia wa Mfugale akidai kuwa umeficha taarifa muhimu kuhusu hali yake ya ndoa.

Anasema wakati mtoa wosia anafariki dunia, alikuwa na ndoa halali aliyofunga na Maulicia Oktoba 14, 1964, na kuficha ukweli kunaweza kutumiwa na msimamizi wa mirathi kumnyima haki mke huyo ya kurithi mali za mume wake; kitu ambacho ni kinyume cha sheria, maadili, na taratibu za Tanzania.

Mafuru anaendelea kuishawishi Mahakama kubatilisha wosia wa Mfugale akisema umekwenda mbali kiasi cha kutoa maelekezo hata kwa mali ambazo si zake.

Anasema kisheria hakuna mtu anayeweza kutoa kitu ambacho si chake (nemo dat quod non-habet) na katika mkondo huo huo, hakuna mtu anayeruhusiwa kutoa maelekezo ya namna ya kutumia mali zisizomuhusu.

Mafuru anasema mtoa mirathi katika aya ya 12, 13 na 14 ya wosia ametoa maelekezo ya namna warithi wake wanavyopaswa kuiendesha Peacock Hotel Limited, akisema maelekezo hayo hayatekelezeki kwani yatasababisha kuingilia uendeshaji wa kampuni (hoteli).

Sababu ya nne ya ubatili wa wosia kwa mujibu wa Wakili Mafuru ni ubaguzi wa wazi uliowaacha kando warithi wengine, akisema mtoa wosia alikuwa na watoto 18; lakini ni watoto watatu tu ndiyo waliorithishwa hisa za Hoteli ya Peacock.

Hoja za utetezi

Akijibu hoja za Mafuru, wakili wa upande wa utetezi, Antipas Lakam amenukuu kifungu cha 89(1)(a) na (c) cha Sheria ya Uthibitisho na Usimamizi wa Mirathi (Probate and Administration of Estate Act) akiungana na upande wa walalamikaji kwa kusema, kwa kuwa marehemu alikiri imani ya Kikristo, basi mirathi yake inapaswa kuongozwa na Indian Succession Act.

Akijibu hoja kwamba wosia ni batili kwa kuwa umeweka masharti ndani yake, Lakam anasema wakili wa mlalamikaji amejiongoza vibaya katika kunukuu kifungu cha 114 cha Indian Succession Act kwani kifungu hicho kinahusika na urithishaji chini ya masharti haramu au ya kinyume cha maadili.

Anasema maneno yaliyopo kwenye aya ya 10 na 11 ya wosia hayamfanyi mrithi kuwa haramu na kwamba si masharti yote yanayowekwa kwenye wosia yanayoubatilisha au kumbatilisha mrithi.

Kuhusu hoja kwamba wosia unawaelekeza warithi kuwapa gawio watoto wengine wa marehemu hivyo kukinzana na Katiba, Lakam ananukuu kifungu cha 126 cha Indian Succession Act kwamba iwapo wosia utakuwa na masharti yatakayomkwaza mrithi, kinachopaswa kufanywa ni kutozingatia sharti hilo.

Anasema hata hoja kwamba masharti yaliyopo kwenye wosia yataingilia uendeshaji wa Peacock Hotel Limited, haina mashiko kwa kuwa wosia wa Mfugale haujaweka masharti ya malipo ya hisa.

Hoja ya wosia kuficha ukweli wa hali ya ndoa ya marehemu, Wakili Lakam anasema kwa kuwa ndoa ilifungwa kabla ya wosia kuandikwa, haiwezi kuathiri chochote kwani mtoa wosia aliandika akifahamu fika kuwa ana ndoa (mke) halali.

Akijibu hoja kwamba wosia unaminya haki (msimamizi wa mirathi anaweza kuutumia kupora haki) ya mke halali kurithi mali za mumewe, wakili wa utetezi anasema nayo haina mashiko kwa kuwa wosia huo umempa Maulicia urithi wa mali nyingine kadhaa.

Lakam anapinga hoja kwamba wosia umetoa maelekezo hata kwenye mali ambazo hazimilikiwi na mtoa wosia, akisema wakili wa mlalamikaji hakuzitaja mali hizo.

Lakam anaendelea kutoa utetezi akisema masharti yaliyopo kwenye hisa za Peacock Hotel Limited yamewekwa kwenye zile hisa tu zilizokuwa zikimilikiwa na Mfugale, na si vinginevyo.

Hukumu

Akitoa hukumu, Jaji Sarwatt amekubaliana na takriban hoja zote za upande wa utetezi akisema kwamba ukiupitia wosia kwa makini utaona kwamba haujambagua yeyote kwa kuwa warithi wote wamepewa urithi fulani miongoni mwa mali za marehemu na kwamba wakili wa mlalamikaji ameshindwa kutaja mtoto yeyote aliyebaguliwa.

Kuhusu ubatili wa wosia kwa misingi ya marehemu kuwa na ndoa ya Kikatoliki, Jaji anasema kitu muhimu cha kuzingatia katika suala hilo ni mwenendo wa maisha ya mtu kabla ya kufikwa na mauti.

Anatoa mfano wa hukumu ya kesi ya mirathi namba 39 ya 2019 ya ‘Benson Benjamin Mengi and others vs Abdiel Reginald Mengi and Another’; na ya Innocent Mbilinyi (1969) HCD No. 283.

Anasema lilikuwa ni jukumu la mlalamikaji kuithibitishia Mahakama kwamba marehemu alikuwa akiishi maisha ya kimila badala ya kuendelea kuleta madai, hasa kwa kuwa hakuna anayepinga suala la imani ya Kikristo ya marehemu, kwani aya ya tatu ya wosia wake inaeleza kwamba Mfugale alikuwa mkristo wa madhehebu ya Katoliki.

Anakubaliana na mawakili wa pande zote kwamba shauri hili linapaswa kuongozwa na Indian Succession Act ili kutanabaisha ubatili au uhalali wa wosia wa Mfugale.

Akitoa uamuzi kuhusu masharti yaliyomo kwenye wosia yanayodaiwa kuufanya uwe batili, Jaji Sarwatt anakubaliana a hoja ya Mafuru kwamba kifungu cha 114 cha Indian Succession Act kinaelezea hilo.

Hata hivyo, hana shaka na sharti lililopo kwenye wosia, akisema ni lazima sharti hilo lionyeshe kwamba lipo kinyume cha sheria au maadili.

Ananukuru kielelezo (a) cha kifungu cha 114 cha Indian Succession Act kinachosema:

“A bequeaths 500 rupees to B on condition that he shall murder C. The bequest is void.”

(‘A’ anamrithisha ‘B’ rupia 500 kwa sharti kwamba lazima amuue ‘C’. Urithishaji huo hauna nguvu kisheria/ni batili.”

Jaji Sarwatt anasema kwa maoni yake masharti yaliyowekwa kwenye wosia hayavunji sheria yoyote.

Kuhusu kuficha ndoa yake, Jaji Sarwatt anasema: “Kwa kuwa mtoa wosia amemrithisha mke mkubwa mali kadhaa, kwa mtazamo wangu ukweli kwamba kwenye wosia hakueleza kwamba ana mke (wa ndoa) hauwezi kubatilisha wosia.

“Hali ingekuwa tofauti kama ingeelezwa kwamba mtoa wosia hakuacha mali yoyote kwa mke wake. Lakini pia mlalamikaji hakuonyesha sheria yoyote inayomlazimisha mtoa wosia kueleza hali yake ya ndoa.”

Hatimaye Jaji Sarwatt akatoa hukumu akisema kwamba Mahakama haioni sababu ya kubatilisha wosia, na kumalizia kwa kusema:

“Maombi haya yanatupiliwa mbali kwani hayana mashiko. Kwa kuwa suala hili limetokana na mashauri ya mirathi, sitoi amri yoyote kuhusu gharama.”

Wakili: Tunakata rufaa

Akizungumza na JAMHURI baada ya maombi yao kutupiliwa mbali, wakili wa mlalamikaji, Mafuru, anasema tayari wamekata rufaa kwenda mahakama ya juu zaidi.

“Tumekata rufaa kwa kuzingatia mambo makubwa mawili. Kwanza, haki ya mke wa ndoa haikuzingatiwa. Pili, hata cheti cha ndoa nacho hakikuzingatiwa,” anasema.

Mafuru anasema ndoa aliyofunga Mfugale mwaka 1964 ni ya Kikristo ya mke mmoja, haina talaka na hadi anafariki dunia ilikuwa haijavunjwa.

Anasema cheti cha ndoa kinachotambulika RITA kinastahili kukubalika mahakamani.

Akizungumzia shauri hilo, mlalamikaji, Kalvarina ambaye ndiye mtoto mkubwa wa Mfugale, anasema anachotamani ni Mahakama imtambue mama yake kama mke wa ndoa na mwanzilishi wa familia.

“Mzee hakuwa na wake watatu. Alikuwa na mke mmoja tu, wengine walikuwa ‘wazazi wenzake’,” anasema.

Kalvarina anasema wazazi wake walifunga ndoa Wasa Misheni mkoani Iringa na anamkumbuka Padri Bora kwamba ndiye aliyewafungisha ndoa.

Anasema mama yake aliishi maisha magumu akiteswa na wanawake hao wengine.

“Lakini kinachosikitisha zaidi ni kutojumuishwa kwenye wosia ilhali ni yeye ndiye aliyeanza maisha na kuweka msingi wa mali za baba,” anasema Kalvarina.

Anashangaa Mahakama kutotambua ndoa ya Kikristo na namna ya kusimamia mirathi wakati wosia umethibitisha kuwa Mfugale ni Mkristo wa Katoliki.

Msimamizi wa mirathi upande wa Mfugale, Titus Mfugale, hakuwa tayari kuzungumza kwa kina uamuzi huo wa Mahakama.

Kwa habari mbalimbali zaidi za kiuchunguzi soma gazeti la Jamhuri kwa sh. 1,000 kila Jumanne