MPAKA Jumamosi ya Oktoba 4, mwaka huu, Bunge Maalumu la Katiba Mpya litakuwa limetumia zaidi ya Sh 100 bilioni bila kupatikana kilichotarajiwa.
Fedha hizo, ni hesabu kuanzia Mei mosi, 2012 siku ambayo Tume ya Marekebisho ya Katiba ambayo ilikuwa na kazi ya kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi kuhusu katiba mpya ilipoanza kazi rasmi.
Tume hiyo iliyoongozwa na Jaji (mstaafu) Joseph Sinde Warioba ilimaliza kazi yake Desemba 31, 2013 na kukabidhi Rasimu ya Pili ya Katiba kwa Rais Jakaya Kikwete. Tume hiyo peke yake ilitumia Sh 76 bilioni.
Baada ya hapo, Rais aliteua Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ambalo liliketi kwa siku 67-kuanzia Februari 18, mpaka Aprili 25, mwaka huu.
Mbali ya mabilioni hayo yaliyotumika kwenye tume, matumizi mengine ni posho kwa wajumbe hao wakianza na kutunga kanuni kabla ya kuingia kwenye mjadala wa sura ya kwanza na ya sita ya Rasimu ya Warioba. Kila mjumbe alikuwa akilipwa Sh 300,000 kwa siku ambako liliahirishwa kutoa nafasi kwa viongozi kuungana na wananchi katika kusheherekea miaka 50 ya Muungano na pili ni maandalizi ya Bunge la Bajeti lilianza Mei 6, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Bunge hilo ilikuwa liongezewe siku 20, mara baada ya kumalizika kwa Bunge la Bajeti, lakini Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta aliomba kwa Rais Kikwete siku 60. Akakubaliwa.
Mpaka Bunge hilo linaahirishwa lilikuwa limetumia zaidi ya Sh. 12.5 bilioni. Ukiacha gharama za shughuli za kiutawala bungeni zikiwamo vile za ukarabati wa ukumbi kabla ya nyumba za makatibu.
Taarifa ambazo gazeti hili imezipata ni kwamba kabla ya kuanza kwa bunge hilo, ukarabati wake ulitumia Sh. 8 bilioni, huku fedha zingine zikitumia kukarabati nyumba 10 za makatibu.
Baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba waliozungumza na gazeti hili walionyeshwa kusikitishwa na kitendo cha Serikali kuamua kutumia fedha za walipa kodi ili hali walijua wazi kuwa msimamo wao ni Serikali mbili, na hawakuwa tayari kukubaliana na maoni ya wananchi.
Julius Mtatiro, ambaye ni mjumbe wa Bunge hilo, alisema fedha za wananchi zimepotea bure huku Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilikuwa inajua inaweza kupata katiba bila kupoteza fedha nyingi kiasi hicho.
“CCM kama walikuwa wanajua msimamo wao ni Serikali Mbili na hawakuwa wanataka maoni ya wananchi kwa nini waliunda tume ambayo leo hii wanaiponda, wangeweza basi kukaa na kuleta katiba ambayo kwa mawazo yao waliona inafaa kwa wananchi,” alisema Mtatiro.
Mtatiro ambaye ni Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa zamani wa wa Chama Cha Wananchi (CUF), alisema kama walikuwa na nia ya kupata maoni ya wananchi ambayo yamekusanywa na tume ya Jaji Warioba ambayo imeteketeza Sh 76 bilioni za wananchi, walitakiwa kuyazingatia na kufuata walichokipendekeza wananchi.
Alisema fedha hizo ni nyingi na kwamba zingeweza kutumika kwenye sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, maji, kilimo na mambo mengine ambayo yako hoi kutekelezwa.
Mtatiro ambaye ni mmoja wa wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), alisema Serikali ingeweza kukaa na kutunga katiba bila kuashirikisha wananchi ambapo wamepuuza maoni yao.
Ugumu wa kupatikana kwa katiba hiyo ulionekana mapema hasa baada ya wabunge zaidi ya 200 wa UKAWA kususia vikao vya Bunge hilo.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema: “ilikuwa ni ngumu kupatikana kwa katiba hii. Walichokuwa wanakifanya ni dhuluma dhidi ya wananchi kwa kupitisha katiba ambayo ni kinyume cha matakwa ya wananchi.”
Profesa Lipumba yumo pamoja na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia ambao kwa pamoja waliwashawishi wajumbe wao kutoka nje ya Bunge.
UKAWA wakiwa bado wamesusa, bunge hilo liliendelea kuanzia Agosti 5, mwaka huu ambako Kamati zake 12 zilifanya kazi ya kujadili na kuchambua Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kabla ya kuifanyia mabadiliko makubwa tofauti na ilivyokuwa awali.
Kamati ilifanya kazi ya uchambuzi wa sura 15 za Rasimu ya Katiba kwa zaidi ya wiki tatu, huku wakifanya mabadiliko kuondoa mambo makubwa yaliyokuwa yakiifanya rasimu hiyo kuonekana mpya.
Bunge hilo limepangua mapendekezo ya Warioba ambako tume yake ilitaka mfumo wa Serikali tatu, Bunge la Muungano la watu 75 na mabunge ya nchi washirika, Makamu rais anayetokana na mgombea mwenza, madaraka ya wananchi kuwawajibisha wabunge, ukomo wa vipindi vitatu vya ubunge, kufuta vyeo vya wakuu wa mikoa, Rais wa Tanganyika na kuondolewa nafasi ya waziri mkuu na ardhi kubaki katika katiba za nchi washirika.
Mapendekeo ya kamati mbalimbali ni muungano wa Serikali mbili, muundo wa bunge kubaki kama ulivyo, makamu wa rais wawili; wa kwanza ambaye ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wa pili ni Waziri Mkuu wa Tanzania, wananchi wasiwajibishe wabunge wao, kusiwemo vipindi vya ubunge, wakuu wa mikoa wamerejeshwa, waziri mkuu wa muungano na kumeingizwa sura mpya ya ardhi.