Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji (mstaafu) Joseph Warioba, amekemea vyama vya siasa vinavyoelekea kutafuta Katiba mpya kwa njia ya maandamano na kuwagawa Watanzania.
Ametahadharisha kuwa dhana hiyo inaweza kusababisha kupatikana kwa Katiba ya kikundi cha kisiasa kinachotafuta maslahi binafsi kinyume cha matakwa ya wengi.
Jaji Warioba ametoa tahadhari hiyo katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam wiki iliyopita, huku akivitaka vyama vya siasa kuacha kasumba ya kujitazama vyenyewe, badala yake visaidie kujenga umoja wa kitaifa.
“Hatutapata Katiba kwa maneno ya majukwaani na maandamano, hatutaki Katiba ya kikundi cha watu, tunataka Katiba ya nchi,” amesisitiza Jaji Warioba na kuongeza:
“Huu utaratibu wa kuzungumza kwenye majukwaa, vyama vya siasa vinazungumza kwa kujitazama vyenyewe, kinachofanyika sasa kinaweza kuwagawa wananchi badala ya kuwaleta wananchi pamoja.”
Ameeleza kusikitishwa kwake pia na hatua ya baadhi ya vyama vya siasa kuingilia shughuli za Mabaraza ya Katiba, wakati mwingine vikibeza kazi za Tume hiyo na kutaka kubadili utaratibu wa utoaji maoni uliowekwa kisheria.
Hata hivyo, Jaji Warioba amesema Tume hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, na kwamba kwa sasa inachambua maoni yaliyotolewa na Mabaraza ya Katiba.
“Kwa kufuata mwongozo ambao Tume ilijiwekea, uchambuzi huu unafanywa kwa kuzingatia uzito wa hoja zilizotolewa na wananchi katika maeneo tofauti ya Rasimu ya Katiba,” amesema na kuendelea:
“Baada ya uchambuzi huu, Tume itaandaa ripoti itakayojumuisha Rasimu ya Katiba iliyoboreshwa kutokana na maoni ya Mabaraza ya Katiba, ambayo itawasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.”
Matarajio ya Tume hiyo, kwa mujibu wa Jaji Warioba, ni kukamilisha kazi hiyo ndani ya muda uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83. Kwa upande mwingine, Jaji Warioba ametumia nafasi hiyo kuwapongeza wananchi wote, asasi, taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana kwa jinsi walivyoshiriki kutoa maoni yao kupitia Mabaraza ya Katiba.
“Tume imefarijika sana na maoni yao [wananchi], na tunaamini yatatusaidia sana katika kuboresha Rasimu ya Katiba kwa maslahi ya nchi yetu,” amesisitiza. Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wananchi wengi wametoa maoni yanayopendekeza maboresho katika mihimili ya utawala na haki za binadamu.
Shughuli ya mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepangwa kukamilishwa kabla ya Aprili 26, 2014.