Waraka wa Mihale kwa Watanzania
Amani iwe kwenu wapenzi wasomaji wa Gazeti la JAMHURI. Karibuni katika safu mpya ya ‘Waraka wa Mihale kwa Watanzania’ itakayokuwa ikijadili mambo mbalimbali yahusuyo mustakabali wa nchi yetu.
Leo katika safu hii nitaanza kwa kujadili amani kuwa ndiyo msingi wa maisha kwa mtu mmoja, kikundi au taifa lolote duniani.
Kwa mujibu wa Kamusi iliyotolewa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) toleo la pili la mwaka 2004, neno amani linatueleza ni hali salama isiyokuwa na ghasia au fujo au vita; tulivu.
Niliwahi kuzungumza na Afisa Mwandamizi Jeshi la Polisi, Makao Makuu ya Jeshi hilo yaliyopo Mtaa wa Ohio na Ghana jijini Dar es Salaam.
Katika mahojiano yetu ya saa moja ofisini kwake, mkuu huyo alichonieleza ni kuwa amani imetoweka nchini, hakuna kuaminiana kati ya viongozi na wananchi, hakuna upendo wala heshima. Hii ni kutokana na ubinafsi uliopo kati yetu.
Watu wamepoteza imani kwa viongozi wao, hawataki kusikia wala kuambiwa na hii inawapa kazi kubwa katika utendaji wao wa kazi katika jeshi hilo, hasa inapotokea maandamano au vurugu mahali.
Alinieleza sheria za jeshi lolote kuwa unapopewa amri na ‘Boss’ wako hutakiwi kuuliza kwa kuwa kuuliza tafsiri yake ni kukusudia kugoma, ambayo adhabu yake ni kupigwa risasi.
Alinieleza kuwa kuna matukio mengi yametokea, ambapo polisi wamekuwa wakitakiwa kutuliza ghasia, akatolea mfano wa jambo lililotokea katika Wilaya ya Tandahimba. Huko wananchi walifunga barabara kuishiniza Serikali kuwalipa malipo ya nyongeza ya zao la korosho.
Polisi walituma kikosi katika tuko hilo kikafanya kazi yake na kutuliza ghasia hizo, lakini baada ya Polisi kufyatua mabomu na kuumiza wananchi hao, siku ya pili Serikali ilitoa fedha hizo na lawama ikabaki kwa jeshi hilo. Akahoji siku zote wahusika walikuwa wapi kutoa fedha hizo hadi amani inatoweka katika eneo hilo? Jibu likaja ni kutokana na ubinafsi.
Pamoja na kuzungumza mengi na kiongozi huyo mwandamizi, binafsi nilitoka ofsini hapo nikiwa natafakuri nyingi na nzito kuhusu mustakabali wa nchi hapo baadaye hususan katika suala linalohusu amani.
Nikarejea mafundisho ya Mwalimu Nyerere nikakumbuka kauli yake aliyowahi kuitoa katika Baraza la Kutunga Sheria, Oktoba 22, 1959 akiwaambia wakoloni wa Kiingereza:
‘Sisi watu wa Tanganyika tungependa kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro ili umulike nje ya mipaka yetu, ukalete matumani penye kukata tama, upendo kwenye chuki na heshima kwenye dharau.
Maneno haya ya Mwalimu yalikuwa na maana ya kuwa Mwenge umulike na kubaini wapi haki inatendeka, wapi palipokosa matumani ya kupata haki ili ishughulikiwe na amani ipatikane.
Mwalimu alichukua maneno haya kutoka kwa Mtakatifu Francis wa Azizi ambaye alipenda amani alipotembea sehemu mbali mbali duniani. Alimini kuwa hakuna amani bila haki. Na haki ni kichocheo cha amani.
Hata hivyo, katika hotuba yake aliyoitoa katika Ukumbi wa Kizota mwaka 1987, alisema amani haipatikani bila haki pasipo na haki amani hutoweka. Kwa kauli hizi zilizotolewa na Mwalimu zinanifanya niungane na kauli ya afisa wa huyo mwandamizi wa Jeshi la Polisi, kuwa sasa amani nchini imetoweka kutokana na kutoweka kwa haki.
Imetoweka kutokana na viongozi wengi kujifanya hawajui umuhimu wa haki na kuhubiri amani katika majukwaa ya kisiasa na nyumba za ibada, ilhali hawaienendi kwa vitendo kama Mwalimu Nyerere.
Wamejaa dhuluma kutokana na ubinafsi, miongoni mwao wamesahau utaifa wameweka maslahi yao binafsi mbele. Hali imeacha kundi kubwa nyuma likiwa limejaa katika lindi la umasikini uliokithiri kwa sababu ya kukosa haki, tumerudi katika zama za usultani wa kuitana huyu bwana na yule mtwana.
Kundi la watwana limejaa chuki dhidi ya mabwana, hakuna heshima wala upendo miongoni mwetu, watwana hawataki kuwasilikiza mabwana na kama watawasililiza ni kwa sababu fulani. Tanzania ya leo si kama ile ya zamani, watu walisoma bure na kupewa madaftari bure. Sasa ni ya fedha mbele kwa kila kitu. Imebaki kuwa ya wasionacho na walionacho, wenye kisu ndiyo walao nyama.
Sasa watwana wamebaki na silaha moja tu ya maangamizi ambayo ni kupiga kura, ikishindikana hiyo amani itatoweka tutashikana mashati na kuuana.
Tumeshuhudia vurugu za wa wamachinga wakipambana na polisi, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Jiji la Mwanza, Mbeya na zile za kudai gesi kule Mtwara – yote mikoa mingine haya ni sababu ya ukosefu wa haki, heshima kwa wananchi hakuna.
Lakini pamoja na matukio yote haya, viongozi hawayaoni wanahubiri amani majukwaani na kwenye nyumba za ibada, wanasahau kuwa amani ilitengenezwa na Mwalimu Nyerere kwa vitendo.
Tanzania ya sasa si ile ya zamani iliyofuta misingi ya Azimio la Arusha, kila anayepata madaraka anafikiri kuwadhulumu wananchi, haoni kuwa wana thamani kwake.
Katu hatuwezi kuwa na amani wakati kuna wananchi wanaendelea kudhulumiwa haki, wanakosewa heshima na kunyanyaswa.
Nachukuwa nafasi hii kuwaasa viongozi wa Serikali na wa dini kutengeneza amani kwa vitendo, wasiihubiri katika majukwaa ya siasa na nyumba za ibada kwa maneno wakati wameajaa dhuluma.
Mungu ibariki Tanzania.