Mkulima wa korosho, Hassan Yakub kutoka Tandahimba, Mtwara.

Natanguliza shukrani kwako Rais wetu mpendwa kwa utendaji kazi wako uliotukuka na ambao watu wa mataifa mengine wanatamani ungekuwa rais wao. Nchi nyingi zinakupigia mfano japo umeiongoza Tanzania kwa miaka mitatu tu!

Naamini si wote watakaoukubali utendaji wako hasa waliokatiwa mirija ya kutunyonya sisi wananchi, lakini ingepitishwa kura ya maoni leo ndipo ungeshuhudia watu wanaokukubali. Hivyo kwa msemo wako wa “Hapa Kazi Tu”, piga kazi baba kwa kiwango chako na uwezo wako wote hadi utakapofikia ukomo wa uongozi wako.

Umetunyooshea nchi kwa wastani wake kiasi kwamba wananchi kwa sasa robo tatu wamekuwa na nidhamu ya fedha. Hata ile pesa waliyokuwa wanaidharau na kuiita ‘jero’ sasa wanaiita kwa jina lake halali – Shilingi mia tano.

Rais Magufuli, napenda nikupongeze kwa kutetea masilahi ya wakulima wa korosho nchini na umesema utawatetea wakulima wote Tanzania bila kubagua kundi lolote.

Kuanzia siku zile kwenye mkutano wako, shukrani sana kwa hatua uliyochukua. Hii ni baada ya kuona mawaziri wa wizara husika ‘hawajiongezi’ na kuchukua hatua. Hii ilikuwa ni baada ya kuona bodi za mazao nazo hazichukui hatua yoyote, bila shaka ni kwa vile walikuwa wanapata masilahi binafsi kupitia ukandamizwaji wa wakulima.

Rais wangu, wakulima wa korosho hali bado ni tete kuliko mnavyofikiria, pia ninahisi ni tofauti na hata unavyofikishiwa taarifa mzee wangu.

Yaani ukipita kwenye vijiji, majina ya mabango ya wakulima yamebandikwa kwenye kuta za vyama vya msingi lakini benki hakuna fedha iliyoingia rais wetu. Nakupa taarifa ulijue hili. Imenichukua muda kufikiria ni jinsi gani nikufikishie kilio hiki, nimeona njia hii ni bora zaidi kwani hata wewe mwenyewe tunajua unapata taarifa kupitia mitandao ya kijamii, vyombo vya habari vya kielektroniki na magazeti. Hata watu wako uliowapa nafasi ya kukujuza habari muhimu wakikuficha utazipata tu kwa njia hizi mbadala.

Rais wetu mpendwa, unafahamu fika asilimia kubwa ya wakulima wengi wa Kusini korosho ndio uhai wao wa kuendesha maisha.

Hii ni kwa kuwa mashamba yao mengi yapo chini ya ile miti (mikorosho), hauwezi kulima mazao mengine kibiashara kwani hayapati hewa ya kutosha. Hayapati jua la kutosha. Vilevile mikorosho inapuliziwa dawa kali sana. Zile sumu zinazopigwa kwenye mikorosho kwa dawa za maji na dawa za unga bado zinarudi chini ya ardhi hata wakilima mihogo, karanga, njugu wanajikuta wanakula sumu ile ile. Watafanyaje na hakuna ardhi ya wazi kupanda chakula chao?

Kutokana na hali hiyo, korosho (dhahabu nyeupe) ndio uhai wao, ndiyo kipato chao na ndiyo muongoza maisha yao.

Rais wangu mpendwa, watu wa Kusini wanapopata fedha za korosho ndipo hununua vifaa vya ujenzi, kodi ya serikali inalipwa kupitia biashara, wanawalipa mafundi wa ujenzi, pia wanachimba visima vya maji. Nayo hiyo ni ajira kwao. Wananunua pembejeo, wananunua sare za wanafunzi, madaftari, viatu na kadhalika.  Tena wamekuwa na mwitikio mkubwa tangu utangaze Sera ya Elimu Bure.

Wanatakiwa wawalipe vibarua watifue mashamba yao ili kuyaandaa kwa msimu ujao na hiyo ni ajira pia. Kule vijiji vingi havina umeme. Wengi wananunua solar panels, yaani umeme wa jua ili wapate mwangaza. Hiyo ni kodi inapatikana kupitia mzunguko wa kibiashara na yote hayo ni kuendesha maisha yao kupitia fedha za korosho.

Mheshimiwa Rais wangu, naandika haya kwa uchungu mkubwa kwa kuwasemea wale wasioweza kufikisha taarifa ofisini kwako na kwa kuwa wewe ni mpenda haki, mpenda ukweli, japo taarifa hii ni chungu, lakini siku zote unatusihi tuwe wasema ukweli kwa kumuogopa Mungu.

Rais wangu mpendwa, wakulima wa korosho wengi wanaishi kwa mikopo kwenye maduka ya watu vijijini na wengine wenye korosho zilizomo ndani wanauza ‘kangomba’ kwa wenye fedha ili waweze kuendesha maisha yao, huku bado wengine wenye korosho wanafanya ‘barter trade’ na wenye mchele.

Wengine wanabadilishana korosho kwa mikate ili maisha yasonge mbele. Huu ni ukweli mweupe kwa sisi tunaoishi vijijini tunayaona haya. Baba, nayaandika haya kwa dhati bila ushabiki wowote na bila chuki binafsi.

Ninapata uchungu sana unavyotupigania wananchi wako kwa kuona dhuluma za wazi kwa watu wako na dhuluma zinafanywa na watu uliowaamini.

Naumia moyoni ila nimeona haisaidii kama sitaandika haya ili kuwasemea wakulima wa korosho kwako ili ujue machungu wanayoyapitia mkuu.

 Rais wangu umeweka utaratibu mzuri wa uhakiki wa mkulima wa korosho mwenye kilo nyingi. Tume iliyoundwa na Waziri wa Kilimo ikijiridhisha ndipo ilipe. Lakini Rais wangu, wakulima wengi wenye kilo chache nao hawajapata fedha zao.

Kama hautaamini hili, uunde tume yako ya intelijensia ifike kimya kimya ikiwezekana itembee na sisi vijijini, ipeleleze kwa wananchi na pia ikiwezekana iende hata benki kuomba statement uone je, majina yaliyobandikwa kwenye kuta za vyama vya msingi na waliolipwa benki yanaendana? Hapo ndipo utaona tatizo liko wapi mzee wetu.

Kama hawakupi ukweli na wanakuongopea kwa kusema “tunalipa, tunalipa”, baba huku hali ni mbaya sana.

Ripoti inasema zaidi ya Sh bilioni 200 zimelipwa kwa wakulima wa korosho, lakini ni fedha chache kuliko kiasi tunachopaswa kulipwa wakulima wa korosho.

Rais wangu, mwambie Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, huku chini wizara husika na tume zao walizounda wanawaangusha sana. Kusema ukweli wamekuja kuchuma fedha na si kufanya kazi waliyoagizwa.

Sasa hivi kwenye uhakiki wanachukua rushwa, tena wanazidai kwa nguvu Rais wangu, naomba nikujulishe kero hii. Mheshimiwa Rais wangu, tume ya uhakiki imekuwa ‘slow’ sana kuliko inavyotarajiwa. Kingine ni kwamba zile safari za mashambani hazipo. Huo ndio ukweli.

Rais wangu mpendwa, nakuambia ujue yaani ni ‘majipu’ huku kwenye hizi tume. Uhakiki wao ni wa kwenye makaratasi tu. Nenda – rudi; nenda – rudi na kumaliza mafuta na vipuri kwenye magari wanayozunguka nayo vijijini ubavuni yameandikwa TASAF. Kwa kweli kumekuwa na usumbufu mkubwa badala ya msaada.

Nionavyo ni bora hizi tume mngechukua watu kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, wengine Kanda ya Kaskazini wasiojuana waje waifanye kazi hii kuliko hizi tume ambazo mmechukua watu huku huku Kusini, wengine wanafanya kazi kwa kujuana na chama fulani cha msingi na pia wanajuana na wafanyabiashara wa korosho.

Tumechunguza kimya kimya na kugundua kuwa wengine katika tume hiyo hiyo baadhi yao na wanunuzi wa kangomba wanajuana na kwa mwendo huu rushwa wanapokea, hivyo Mheshimiwa Rais, unachokitaka hautafanikiwa kwa asilimia 100.

Ikiwezekana mwaka huu msimu wa korosho (2019-2020) chukua tume kutoka huko. Mheshimiwa Rais wetu mpendwa, huu ni ushauri tu, ikikupendeza uchukue uutumie ili ufanikishe lengo lako la kukomesha kangomba, ambalo kwa hakika ni kukomesha uhujumu uchumi wa nchi na pia uhujumu wa malipo stahiki kwa wakulima.

Rais wangu, kuna baadhi ya maofisa tarafa wanaoongoza misafara ya tume ya uhakiki wa korosho wamekuwa wakichukua rushwa ili kusaidia kazi iende haraka kwa wenye kilo nyingi za korosho.

Mimi pia nimeombwa rushwa ya Sh 100,000 kwa nguvu na katibu tarafa ili asaidie uhakiki wangu uwe mwepesi nipate malipo ya korosho watakapoanza kulipa.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, anafahamu hili kwa kuwa nilimshtakia na akasema atalifanyia kazi na kunirudishia majibu. Lakini hadi sasa hajashughulikia ingawa nilimkumbushia. Makatibu tarafa hawa wanakuchafua, wanakufanya uonekane hauna nia njema na zao la korosho kwa wananchi wako wa Kusini.

Mimi rushwa sikutoa ingawa nilimuahidi kumpa. Rais wangu mpendwa, pembejeo nimezinunua bei ghali sana kuanzia dawa za maji mpaka za unga.

Sulphur kulima korosho imekula muda wangu usiku na mchana, maana muda mzuri wa kupuliza dawa za korosho ni usiku. Mchana ni kulimia na kufagilia mikorosho. Nimeteseka kusomba maji shambani, nimeingia gharama kubwa kuhudumia ‘dhahabu nyeupe’ kwa uchumi wa nchi yangu na kipato changu, leo niteseke pia kwenye kulipwa kwa sababu ya hawa tume ya uhakiki?

Ukitaka majina nitakutajia na ushahidi unapatikana. Nipo tayari kuwa mhanga kwa ajili ya wakulima wa korosho ili uwawajibishe huku chini kwa wanayoyafanya.

Tangu tufanyiwe uhakiki wa korosho kwa kujaza fomu na kujibu maswali waliyotuuliza, hadi leo [wiki iliyopita] hawajarudi kwa safari za kwenda kwenye mashamba tunayomiliki wakulima ili tuweze kulipwa fedha zetu ili tufanye maendeleo.

Wakulima wengi wa hali ya chini shule zinafunguliwa Januari hii, wengi wao hawana fedha za kununua mahitaji ya watoto. Kama mtu ugali wa kula na familia yake ni shida, hayo maandalizi ya mtoto kwa ajili ya shule atawezaje?

Rais wangu, tunaomba hawa wenye korosho kilo chache walipwe kama agizo lako ulivyotaka ili waokoe familia zao, tubaki sisi wakulima wenye kilo nyingi tuhakikiwe mashanba yetu kwa wakati ili tupate stahiki zetu kama ulivyoagiza.

Roho za kwanini hizi ndizo zinasababisha hadi ofisa tarafa ananiambia nina korosho nyingi sana nitalipwa fedha nyingi sana, kwa nini ninakuwa bahiri kumpa Sh 100,000? Ninayo mashamba manne ya korosho. Leo hii nitoe rushwa kupata haki yangu, hili jambo mbele yako na mbele ya Mungu halikubaliki.

 Wakulima tuko radhi kukesha mguu kwa mguu kutembelea mashamba yetu wajiridhishe. Waliotoa pesa wameshindwa kujua rais wetu anataka nini. Wakulima wa korosho tunayo mengi ya kusema kwako ila nafasi haitoshi. Kwa machache haya utakuwa umepata picha kamili hali ikoje.

Imeandikwa na mimi kijana wako mkulima mtiifu, Hassan Yakub wa Hayate Organic Farms,

Tandahimba

Simu: 0716 508 848