Waheshimiwa Wabunge,
Hii ni sehemu ya pili ya masimulizi juu ya ukweli wa ufisadi wa akaunti ya Tegeta Escrow.
Baada ya IPTL NA TANESCO kutiliana saini hapo Mei 26,1995 mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura, umeme huo wa dharura ulizalishwa miaka saba baadaye huku TANESCO ikiendelea kulipa kila mwaka kwa IPTL malipo ya uwekezaji (capacity charge).
Wakati huo huo katika utekelezaji wa mkataba huo, IPTL ilikosa kabisa uaminifu. Ilibadilisha kinyemela mtambo wake wa aina ya SSD uliokuwamo katika mkataba ikaweka mtambo hafifu wa aina ya MSD huku ikitoza TANESCO gharama kubwa zaidi ya mtambo ule mzuri wa SSD. Kitendo hicho cha ulaghai na udanganyifu cha IPTL kikasababisha gharama halisi za mradi huo kuwa mara tatu!
TANESCO ikajikuta inatozwa kiwango cha juu mno cha fedha kuliko ilichopasa kulipa. TANESCO ikagundua kuwa ilikuwa inaibiwa na IPTL. Kitendo hicho cha mwekezaji huyo mwenye historia ndefu ya wizi na udanganyifu kikazusha mgogoro mkubwa kati ya TANESCO na IPTL.
Mwezi Aprili, 1998 akatokea Mtumishi wa Serikali mzalendo kwa jina la Patrick Rutabanzibwa. Alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini.
Wakati IPTL ikitambua vyema kwamba haitakiwi na wananchi wazalendo kampuni hiyo ya kifisadi ilimpa Rutabanzibwa rushwa ya dola 200,000 za Kimarekani ili aiunge mkono. Lakini hakupokea.
Ukweli huo ulibainishwa na Rutabanzibwa katika kiapo alichoapa mbele ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). IPTL haikukanusha. Lakini haikuchukuliwa hatua.
Baada ya hapo Rutabanzibwa alimshauri Rais Benjamin Mkapa mgogoro kati ya TANESCO na IPTL upelekwe Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji iliyoko London, Uingereza. Rais Mkapa akaukubali ushauri huo. TANESCO ikafungua kesi Agosti, 1998.
Krismasi ya mwaka 1998 Rutabanzibwa aliporejea nyumbani akitokea kanisani alikuta bahasha ambayo ilikuwa na Sh 500,000 na maelezo kwamba hiyo ilikuwa soda yake kutoka IPTL. Rutabanzibwa akawarudishia wenyewe fedha yao.
Hapa ni muhimu izingatiwe kwamba si Rutabanzibwa peke yake aliyepambana na rushwa ya IPTL.
Umoja wa Nchi za Ulaya ulisononeka kufahamu kwamba IPTL ilikuwa ikitoa rushwa kwa viongozi wa chama tawala na Serikali bila serikali kuchukua hatua.
Kwa hiyo haikushangaza kuona kwamba mwaka 2014 umoja huo uliamua kuinyima msaada Tanzania baada ya kuivumilia kwa muda mrefu Serikali ya Tanzania iliyokuwa ikiendelea kuikumbatia IPTL.
Nayo Benki ya Dunia ilipinga IPTL. Kadhalika na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Gazeti la Daily Mail toleo la Julai 15, 1998 liliripoti kwamba IMF ilikuwa imesema, “Watanzania ni wanyonyaji wakubwa sana wa Tanzania wenzao.”
Na hiyo ndiyo hali halisi ya Tanzania.
Katikati ya kelele hizo za Umoja wa Ulaya, Benki ya Dunia na IMF juu ya kushamiri kwa rushwa Tanzania Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI) zilishirikiana katika kuandaa ripoti iliyojaa ushahidi uliothibitisha kwamba IPTL ilikuwa ikitoa rushwa kwa viongozi wa chama tawala na wa serikali. Lakini Serikali ilitupa ripoti hiyo. IPTL ikaendelea kutoa rushwa.
Mahakama ya Kitaifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya uwekezaji ilitoa uamuzi wake wa kesi ya TANESCO na IPTL Julai 12, 200. Mahakama iliridhika kwamba IPTL haikuwa imefanya jambo la halali kubadili kinyemela mtambo wake mzuri wa SSD na kuweka badala yake mtambo hafifu wa MSD kisha kuitoza TANESCO gharama kubwa zaidi badala ya kupunguza gharama.
Mahakama ikaagiza gharama ziwe dola milioni 123.6 badala ya dola milioni 163.0 iliyokuwa imekwishatozwa TANESCO.
Vile vile Mahakama ilibaini kwamba bei ya senti 13 kwa uniti moja ya umeme iliyokuwa inauziwa TANESCO na IPTL ilikuwa kubwa mno na kwamba haikuzingatia thamani halisi ya uwekezaji. Mahakama ikaagiza ufanywe ukokotoaji mpya.
Kwa hiyo TANESCO na Tanzania kwa jumla ilishinda kesi yake. Basi kwa kufuata hukumu ile ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi TANESCO na Taifa kwa jumla ingeweza kuokoa fedha zake kama tu serikali ingesimamia utekelezaji wake.
Lakini Serikali haikufuatilia chochote mpaka leo miaka minane baadaye taifa linaambiwa fedha zote katika akaunti ya Tegeta Escrow zilikuwa za IPTL. Hata ukweli kwamba kulikuwa na kodi ya Serikali ndani ya fedha za IPTL umetajwa mwishoni. Serikali imelinda maslahi ya IPTL.
Lakini pia ukweli unabaki palepale kwamba mgogoro kati ya TANESCO na IPTL haukumalizika mpaka leo kwa sababu hakuna mahakama iliyomaliza mgogoro huo kwa kutamka kwamba katika mgogoro uliokuwapo TANESCO ilikuwa na fedha kiasi gani na IPTL fedha kiasi gani katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Mgogoro kati ya TANESCO na IPTL ukazaa Akaunti ya Escrow. Ilikuwa Julai 5, 2006 Serikali (kupitia Wizara ya Nishati na Madini), IPTL na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) waliingia makubaliano ya kufungua Akaunti maalumu (Escrow Account).
Chini ya makubaliano hayo fedha za Akaunti ya Escrow zingeendelea kuwa chini ya mamlaka ya wakala wa Akaunti ya Escrow (Escrow Agent) ambaye alikuwa BoT.
Ilikubaliwa kwamba fedha hizo zingeweza kutolewa tu iwapo ama ingetolewa hukumu ya mahakama ya kutolewa fedha hizo BoT au kama pande mbili za mgogoro (TANESCO na IPTL) zingewasilisha BoT makubaliano yaliyoridhia kutolewa kwa fedha hizo zilizokuwa na mgogoro.
Kwa kuwa mpaka leo hakuna jambo moja kati ya yote mawili lilofanyika basi ilitazamiwa kwamba fedha za Escrow ziko BoT mpaka leo.
Wakati ule ilitokea Kampuni iliyojiita Piper Link ambayo ilifanya jaribio la kununua hisa ambazo Mechmar walikuwa wakizimiliki katika IPTL. Ikagundulika kuwa ni Harbinder Singh Seth aliyekuwa akimiliki kampuni ya Mechmar pia alikuwa mmiliki wa kampuni mpya ya Piper Link iliyotaka kununua hisa za Mechmar.
Katikati ya utata na udanganyifu huo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, aliitisha kikao hapo Agosti 7, 2013.
Kikao hicho kiliamua kutuma wanasheria Malaysia kwenda kuchunguza kampuni ya Mechmar na mmiliki wake, Harbinder Singh Sethi.
Wakati Serikali ilipokuwa inawaandaa wanasheria kwenda Malaysia tayari Harbinder Singh Sethi wa IPTL na Mechmar alikuwa ameunda kampuni mpya ya Piper Link na nyingine ya Pan African Power Solution (T) Limited (PAP).
Ikatokea kwamba Harbinder Singh Sethi ndiye IPTL, Mechmar, Piper Link na PAP!
Wakati hayo yalipokuwa yakitokea kampuni ya VIP ya James Rugemalira iliamua kuuza hisa zake katika IPTL kwa kampuni ya PAP ya Harbinder Singh Sethi. Baada ya hapo VIP Engineering ilikwenda mahakamani kuomba kufutwa mgogoro wake na TANESCO. Mgogoro ukabaki kati ya IPTL na TANESCO.
Septemba 5, 2013 Mahakama Kuu chini ya Jaji John Utawa iliridhia mali na shughuli zote za VIP na IPTL ziende kwa kampuni ya PAP. Lakini mahakama hiyo haikusikiliza mgogoro wa TANESCO na IPTL wala haikuamua fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow wapewe PAP au IPTL. Hili ni jambo la msingi kuzingatiwa kwa sababu ndilo linalothibitisha kwamba fedha za Akaunti ya Escrow ilitolewa BoT isivyo halali. Maana Mahakama Kuu chini ya Jaji John Utawa haikukaa kusikiliza mgogoro wa TANESCO na IPTL.Ilikaa kusikiliza mgogoro wa VIP Engneering na IPTL.
Kwa kuwa mahakama hiyo haikukaa kusikiliza mgogoro wa TANESCO na IPTL wala TANESCO haikuwakilishwa kwanye mahakama hiyo basi mahakama isingeweza kuamua fedha za Akaunti ya Escrow zitolewe BoT.
Tukiwarudia wanasheria waliotumwa na Serikali kwenda Malaysia wanasheria hao wawili waliondoka nchini Septemba 13, 2013, walikuwa Mwanasheria Mkuu wa TANESCO, Godwin Ngwilimi na mwanasheria mwingine kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wanasheria hao walipokuwa nchini Malaysia walibaini kwamba kampuni ya Mechmar ilikuwa imefilisika na ilikuwa imewekwa na Mahakama Kuu ya Malaysia chini ya mufilisi tangu Mei 12, 2010. Hatua hiyo ilikuwa imechukuliwa baada ya kampuni hiyo kushindwa kulipa mikopo iliyokuwa ikidaiwa.
Wanasheria hao wariarifiwa pia kwamba kampuni ya Piper Link ya Harbinder Singh Sethi ilifanya nchini humo jaribio la kuiba cheti cha hisa saba za kampuni nyingine ya Mechmar iliyokuwa imefilisika.
Wanasheria hao waliambiwa maovu mengi juu ya kampuni ya Mechmar na mmiliki wake. Waliporejea nchini wakaandika ripoti iliyoanika kila kitu kuhusu kampuni hiyo. Lakini kama ilivyokuwa kawaida, pamoja na gharama zote ambazo Serikali ilitumia katika kuwatuma wanasheria hao Malaysia, Serikali ilitupa ripoti hiyo. Ikaendelea kuikumbatia IPTL.
Katika toleo lijalo la gazeti hili tutaangalia fedha za akaunti ya Tegeta Escrow ilivyotolewa BoT na Serikali ilivyotekeleza maazimio ya Bunge kuhusu kashfa ya Tegeta Escrow.