Wanaosoma Ujerumani wamlilia Kikwete
Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, kwanza naomba niombe msamaha kwa kutumia forum hii badala ya kukuandikia binafsi. Hii ni kwa sababu ya dharura ya jambo lenyewe linalohitaji hakika hatua za haraka sana ili kuokoa haya yanayotokea. Hivyo, naomba unisamehe kwa kuweka bayana hili hapa.
Mheshimiwa Rais, baada ya msamaha wako, sasa naomba nieleze kwa ufupi kuhusu ni kwa namna gani unahitajika kuingilia kati, kwani ni karibia watu (Watanzania) 50 bila kuhesabu familia zao. Hawa ni wanafunzi wanaofanya masomo yao ya Uzamivu katika vyuo mbalimbali nchini Ujerumani kupitia mkataba wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania (kupitia TCU na MOEVT) na Serikali ya Ujerumani (kupitia DAAD). Hawa Wanafunzi, kwa hapa Tanzania ni wahadhiri katika vyuo vya umma kama SUA, UDSM, Mzumbe, SUZA, n.k.
Katika ufadhili huo, hawa wanafunzi wanapaswa kulipwa asilimia 80 ya pesa ya kujikimu kutoka Tanzania (MOEVT) na Serikali ya Ujerumani kupitia DAAD inatoa asilimia 20. Pamoja na hayo, DAAD inasimamia pia Bima ya Afya, gharama za supervisors wa hao wanafunzi, n.k.
Mheshimiwa Rais, hao wanafunzi, baadhi yao wako mwaka wa tatu, wengine wako mwaka wa pili, wengine mwaka wa kwanza, na wengine bado wanajifunza lugha kwa miezi sita ili wakaanze masomo yao rasmi kwenye vyuo husika. Ni mpango endelevu, kwani ulilenga kuwapa capacity building kwa muda wa miaka mitano na kila mwaka ilitakiwa kuwe na wanafunzi 20. Hata hivyo, hiyo idadi ya watu 20 haijawahi kufikiwa hata mwaka mmoja kwa sababu mbalimbali ambazo nitazieleza hapa, kwani si kusudio la waraka huu. Huu mpango au tuuite mkataba ni renewable kila baada ya miaka mitano.
CHANZO CHA TATIZO KWA HAO VIJANA UJERUMANI
Kama nilivyoeleza kwamba kwenye mkataba wao, Serikali yet ya Tanzania (kupitia MOEVT/TCU) wanapaswa kuwalipa asilimia 80 ya pesa ya kujikimu kila mwezi, na Serikali ya Ujerumani (kupitia DAAD) wanapaswa kulipa asilimia 20; hali imekuwa nzuri siku zote kwa upande wa Wajerumani, kwani haijawahi kutokea wakashindwa kukidhi matakwa ya mkataba kwa wanafunzi hawa.
Hali ikiwa hivyo kwa upande wa Serikali ya Ujerumani, upande wa Serikali yetu pendwa imekuwa tofauti. Serikali ya Tanzania kupitia MOEVT na TCU wameshindwa kukidhi matakwa ya mkataba na sasa Watanzania hawa wenzetu wanataabika na kudhalilika sana huko Ujerumani.
Miezi miwili sasa wanafunzi hawajapata pesa kutoka Tanzania kwani TCU walipaswa kuwatumia pesa mwishoni mwa Mei 2013 kwa ajili ya kujikimu. Lakini hali imekuwa tofauti, kwa sababu mpaka sasa hawajatumiwa pesa yoyote.
Mheshimiwa Rais, pamoja na jitihada zote walizokwishafanya ili wapate haki yao, hali ya giza imeendelea kutanda kwa ndugu zetu hawa, kwani hawapati jibu linaloeleweka kutoka TCU wala MOEVT. Jitihada walizokwishafanya hadi sasa ni pamoja na;
1. Kuwasiliana na TCU tangu Mei mwishoni mpaka jana, lakini wameendelea kuambiwa tu kusubiri na wala hawaambiwi kwamba ni lini pesa zitapatikana.
2. Kuna baadhi yao wako field jijini Dar es Salaam, nao wamejaribu kwenda TCU pamoja na wizarani lakini bado hakuna ufumbuzi hadi sasa.
3. Wamejaribu kuwapigia simu wahusika, lakini matokeo yake simu nyingi hazipokewi na wahusika hasa baada ya kuona code za simu za Ujerumani, kwani tayari wanajua tatizo ni nini japo hawataki kutoa ufumbuzi. Hata zile simu zinazopokewa nazo hazina majibu ya kuridhisha.
4. Wamejaribu kuwasiliana na DAAD ambaye naye ni sehemu katika udhamini wao, nao pia inaonekana wamesimamia kwamba wao wanatimiza sehemu yao bila shida, hivyo ni jukumu la Serikali ya Tanzania kukidhi matakwa ya mkataba kama walivyokubaliana tangu mwanzo.
Mheshimiwa Rais, kwa msingi huo, hawa wananchi wako wana hali mbaya sana kiasi kwamba hawana uwezo tena wa kula, kulipa gharama za kodi za vyumba, gharama ya dawa, n.k. Hali hii inawaathiri hawa Watanzania kisaikolojia, kwani badala ya kuzingatia zaidi masomo hali zao za maisha zimekuwa za taabu sana kiasi kwamba wengi wao wamekata tamaa. Hakika wanahitaji hatua za haraka kwani kuna hatari baadhi yao kama si wote na familia zao wakatolewa ndani ya vyumba kwa kushindwa kulipia pango miezi miwili mfululizo. Pia hata pesa ya kujikimu, ikiwa ni pamoja na nauli ya kwenda vyuoni hawana.
Mheshimiwa Rais, nimefahamishwa kwamba, wapo baadhi yao wanafikiria kusitisha masomo pamoja na kwamba baadhi yao wako hatua za mwishoni kuhitimu. Hii hali ikifikiwa hakika halitakuwa jambo jema kwa hawa vijana, vyuo wanakofanyia kazi, Serikali yetu ya Tanzania, na hata uhusiano wetu na nchi rafiki kama Ujerumani. Kwa msingi huo, kuna mahitaji ya haraka sana kwa ofisi yako kuchukua hatua za mapema ili kuokoa maisha ya Watanzania hawa na taswira ya nchi yetu kwa ujumla mbele za nchi rafiki kama Ujerumani.
Habari hii ni ya kweli, kwani mimi kuna kaka yangu naye ni mmoja wa wanaotaabika huko Ujerumani kwa sasa. Sisi kama familia tumejaribu kumtumia kile kidogo tulichokuwa nacho tangu Juni, na sasa hatuna uwezo tena.
Natanguliza shukrani, na kukuombea hekima za Suleimani zikujae, na huruma zake Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema akutie nguvu abadan Mheshimiwa Rais wangu ili upate ufumbuzi na kuokoa maisha ya vijana hawa.
Wako katika Ujenzi wa Taifa,
Director Tanzania.
Julai 4, 2013