Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia amani na afya njema. Yote tunayaweza kwa sababu yupo aliye Mkuu kuliko vyote. Ni wajibu wetu kumshukuru na kulihimidi Jina lake Takatifu.

Tanzania imejaliwa kuwa na maliasili ya kutosha ya wanyamapori, misitu, samaki, maji, madini, ardhi ya kutosha na pia rasilimali watu.

Haya yote ni muhimu kwa maendeleo yetu na Taifa kwa ujumla. Kitu cha msingi tunachotakiwa kukifanyia kazi ni kwa jinsi gani tunazilinda na kuzitumia rasilimali hizo kuweza kujiletea maendeleo. Vilevile tujiulize tunafanya nini kuhalikisha tunalinda maliasili zetu hasa misitu ya asili na wanyamapori ili zinufaishe kizazi hiki na vizazi vitakavyokuja?

Inasikitisha mno tunaposikia kwamba watu kutoka nje ya nchi au hata Watanzania wenyewe wanafanya wanavyotaka kwa kuvuna rasilimali misitu au wanyamapori na kuzisafirisha nje ya nchi kinyemela.

Wapo pia wafanyabiashara wa ndani wanaopora rasilimali zetu za asili bila kufuata utaratibu na kulipa ushuru unaotakiwa kulipwa, lakini hawafanyi hivyo na badala yake wanatuibia kwa sababu usimamizi wetu ni mdogo.

Hii ni dhuluma kwa Watanzania maana urithi wetu wa asili ni mali yetu sote. Mtu akikamata au kuua mnyama bila kujali taratibu au sheria zilizowekwa huyo ni mwizi anayestahili kuadhibiwa vikali. Januari 8, mwaka huu  katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) polisi kwa kushirikiana na askari wanyamapori walikamata kenge 149 wakiwa tayari kusafirishwa kwenda ng’ambo hasa sehemu za Mashariki ya Mbali.

Tuliwapongeza sana kwa kitendo hicho cha kuwakamata hao kenge wengi kiasi hicho wakiwa hai. Isitoshe, walikuwa wemefungwa vizuri kwa kutumia mifuko maalumu iliyowawezesha kupumua na pia wakawahifadhi kwenye masanduku.

Hii ilidhihirisha kuwa wahusika kutoka nje ya nchi walikuja wakiwa wamejiandaa wakijua wamekuja kupora maliasili zetu. Kama wasingekamatwa kenge hao 149 wangeondoka bila ya sisi kufahamu isipokuwa watu wachache ambao hushirikiana na waporaji hao.

Juni 24, mwaka huu kwenye uwanja huo huo wa JNIA walikamatwa kobe 173 nao wakiwa tayari kusafirishwa kwenda nje ya nchi. Walikuwa wamefungwa vizuri kwa kutumia mifuko maalaumu kwa misingi kwamba waliohusika walikuwa wamejiandaa kuja kuchukua walichokitaka bila kujali umuhimu wa viumbe hao kwa maendeleo ya Taifa letu.

Matukio haya na mengineyo ambayo pengine hayajaripotiwa yanaifanya nchi yetu kuwa eneo la kupora maliasili zetu waziwazi bila kujali maslahi yetu. Kwa mara nyingine tena usiku wa Novemba 16, mwaka huu kwenye uwanja huo huo walikamatwa kobe wengine 201 wakiwa wanatoroshwa kwenda nje ya nchi. Kobe hao walikuwa pia wamefungwa kwenye mifuko maalumu na wakipelekwa nchi za Asia.

Vitendo hivyo ni hatari sana kwa uhai wa uchumi wetu. Hali hii inaonyesha kuwa uporaji au wizi upo na unafanyika kwa kasi kubwa. Nathubutu kusema kuwa pengine wanaokamatwa ni kwa bahati mbaya tu pengine wapo waporaji wengi wanaotoroshwa bila ya kukamatwa. Gazeti la Majira toleo namba 7986 Vol.II/6086 la Alhamisi, Novemba 19, 2015 lilitoa taarifa kuwa mzigo huo ulikuwa umeishapita katika mashine za kukagulia mizigo na kukamatwa baada ya kunuswa na mbwa wa usalama muda mfupi kabla ya kuingizwa kwenye ndege!

Hii ina maana kama hao mbwa wa usalama wasingekuwapo, basi mzigo huo wenye kobe 201 ungesafirishwa bila ya sisi kujua maana ulishapita kwenye mashine za ukaguzi.

Je, hizo mashine haziwezi kung’amua viumbe hai ndani ya sanduku au kifurushi? Isitoshe, inawezekana kuwa hata hao waliohusika na hujuma hiyo si mara yao ya kwanza kupitisha viumbe kama hao.

Inawezekana wamefanya hivyo mara kadhaa kutokana na ukweli kwamba hata mbwa wa usalama hawatakuwapo kila siku na kila wakati au hata kama wapo wasilazimike kunusa mizigo yote kabla ya kuingizwa ndani ya ndege.

Hata hivyo, nichukue fursa hii kuwapongeza wote waliojitahidi kuwakamata waporaji hao waliokuwa tayari kuwatorosha kobe wetu bila kujali maslahi ya Taifa.

Polisi, askari wanyamapori na hata maafisa wengine kama wa Usalama wa Taifa kwa pamoja nasema asante sana na hongera sana kwa kazi nzuri mliyoifanya kwa faida yetu wote. Nadhani kuna haja ya Serikali kuweka mkakati mzuri wa kuwazawadia watumishi wa umma ambao kupitia juhudi zao nchi inaokoa rasilimali zake.

Iwapo kobe hao wangeondoka Taifa lingepata hasara kiasi gani? Hata kama wanaookoa hasara kama hiyo isitokee wangepewa robo tu ya thamani yake ingeongeza ari na motisha kwa watumishi wa umma kuweza kuwa na uchungu wa masuala kama hayo na kuongeza juhudi za kudhibiti hasara isitokee.

Ni mara ngapi tunaambiwa meno ya tembo kutoka Tanzania yamekamatwa nje ya nchi? Inakuwaje meno ya tembo haramu yatoke nchini mwetu na yakamatiwe mbali? Hiyo ni ishara kuwa baadhi hawajali maslahi ya Taifa.

Wakati mwingine huwa nasikia tetesi kuwa baadhi wa wahusika iwe ni polisi au maafisa wengine ndani ya taaluma zetu ikiwamo ya misitu na wanyamapori; husindikiza majangili ili mradi wao wanufaike! Tabia kama hiyo mi mbaya sana na kama watumishi wa umma wa aina hiyo wapo, basi wakae wakijua kuwa “za mwizi ni arobaini”- iko siku tutawakamata na watakiona cha mtema kuni na hasa wakati huu wa “Sasa Kazi Tu”. Hakuna kufanya mchezo dhidi ya maslahi ya Taifa letu. Kila mtu atimize wajibu wake ipasavyo na isiwe kinyume cha hapo.

Sheria ya Misitu inazuia kusafirisha magogo ya aina yoyote kwenda nje ya nchi. Iwapo kitu kama hicho bado kinafanyika ni ulegevu katika kusimamia utekelezaji wa sheria husika. Niliwahi kuambiwa kwamba kuna magogo yanasafirishwa kwenda nje ya nchi kwa madai kuwa yanatoka Zambia. Kama kweli hilo linafanyika, basi kunatakiwa kuwepo usimamizi wa kutosha maana watu wenye nia mbaya watatumia mwanya huo na kujifanya wanasafirisha magogo kutoka nje ya nchi na hasa wale wanaojihusha na biashara ya mazao ya mistu kwenda China.

Vilevile, tunakataza mkaa kusafirishwa kwenda nje ya nchi, lakini suala hilo linafanyika kutokana na kutokuwapo udhibiti wa kutosha katika baadhi ya maeneo ya mipakani.

Nitoe rai kwamba Watanzania- ni vema tukawa na uchungu na maliasili zetu. Tusiruhusu watu wachache wakapora rasilimali asilia na kuzipeleka nje ya nchi kwa faida yao binafsi. Kila mtanzania awe mlinzi na msimamizi wa maliasili zetu. Vijiji viwe vitovu vya kulinda na kusimamia rasilimali za asili ikiwamo mistu na wanyamapori.

Nichukue fursa hii kuungana na viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Serikali katika ujumla wake kwa hatua walizodhamiria kuzichukua kupambana na watu wote wa ndani na nje ya nchi ambao nia zao ni kupora maliasili zetu katika sekta za misitu na wanyamapaori.

Hapa ni “kukaza buti” tu na wala hakuna kulegalega. Ni vita kama ilivyo aina nyingine ya vita. Tena vita ya kupambana na majangili ni vita ngumu sana; hivyo inahitaji ujasiri na ukakamavu wa hali ya juu sana.

Uzalendo wa kitaifa ni muhimu sana, la sivyo wahusika wa utekelezaji wa sheria wasipokuwa wazalendo kikamilifu watarubuniwa kirahisi na hivyo kusababisha rasilimali zetu ziporwe na sisi kubaki maskini wakati kirasilimali sisi ni matajiri kuliko nchi nyingi duniani. 

Ndiyo maana baadhi yao wanakuja wachukue kirahisi wakijua tumelala usingizi. Sasa “sauti ya mtu aliaye nyikani” imepulizwa na mwenye masikio na asikie. Hakuna kulala usingizi tena. Ni wakati wa kila Mtanzania kuwa macho. Yeyote atakayetusaliti, basi ajue kitakachompata itakuwa ni halali yake.

Kama sheria zilizopo zina upungufu, basi ni wakati wa kufanya marekebisho ili ziwe kali zaidi. Watu wa kutoka nje ya nchi wanaokamatwa wakiwa wamepora maliasili zetu ni wahujumu wa uchumi wetu. Wasiwe watu wa kuishia kulipishwa faini tu, bali ikibidi tuwatie kitanzi liwe fundisho kwa wengi kuwaw Tanzania si mahali pa kwenda kuchezea na mtu kufanya anavyotaka.

Tuwafilisi ki-kweli kweli na wajue pia kuwa mtu apandacho ndicho atakachovuna. Ukipanda wema utavuna wema, lakini ukipanda udhalimu utavuna udhalimu tu.

Tusiwachekee eti wanatoka nchi rafiki. Hakuna cha nchi rafiki. Mhalifu ni mhalifu tu hata atoke wapi, atabaki kuwa mhalifu. Kama anatoka nchi rafiki, basi urafiki wao tuuone kwa matendo yao mazuri na kuwa na malengo yaliyokaa kirafiki, na si kinyume cha hivyo.

Bado najiuliza kwa mfano, hao waliokamatwa na kobe 201 hatima yao ni nini? Je, ni kuwanyang’anya hao kobe na baadaye kuwaambia wapande ndege waondoke? Watu kama hao walitakiwa warudishwe huko porini wakawe walinzi wa hao kobe bila kujali wametoka wapi. Kwa hali kama hii suala la haki za binadamu halipo.

Haiwezekani wahalifu wakatetewa kwa kutumia ubinadamu wakati wanaliangamiza Taifa letu. Tuwe na moyo mkuu tulinde utaifa wetu na rasilimali zetu. Haki ya Taifa na watu wake kwanza; mengine yatafuata.

 

Dk. Felician Kilahama, ni  Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, mstaafu. Anapatokana kupitia namba: 0783 007 400