Ingawa vyama vya ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi na CUF kwa nyakati tofauti vimebainisha haja ya vyama vya upinzani kuungana na kusimamisha mgombea mmoja katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu, hilo bado linaonekana kuwa jambo lililo mbali sana kuafikiwa.

Hiyo inatokana na tamaa ambayo baadhi ya vyama ambavyo vinaamini kuwa vina nguvu, hivyo vinastahili kupata nafasi kubwa na kutanguliza hilo kama sharti lao.

Mathalani, ACT-Wazalendo kimekwisha kubainisha kuwa kingependa kutoa mgombea urais iwapo vyama vya upinzani vitakubali kuungana na kuwa na mgombea mmoja.

Lakini hilo linaweza kuwa jaribio kwa vyama vingine ambavyo navyo vinajiona kuwa vina nguvu ya kutoa mgombea urais.

Akizungumza ofisini kwake, Katibu wa Kampeni na Uchaguzi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Mohammed Massaga, amelieleza JAMHURI kuwa ifikapo mwezi Juni mwaka huu wataweka wazi jina la mgombea wao wa urais, na kwamba endapo vyama vingine vitaridhia jina hilo kuna uwezekano mkubwa wa upinzani kushika dola baada ya Uchaguzi Mkuu.

Aidha, anasema uhakika wa kushika dola unatokana na ukweli ulio wazi kwamba katika uchaguzi ujao watashinda kwa kishindo viti vyote vya ubunge na kiti cha urais katika visiwa vya Zanzibar.

Anadokeza kuwa ushindi wao Zanzibar utatokana na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, kujiengua na kujiunga na ACT-Wazalendo na kukifanya chama hicho kuimarika maradufu.

Anasema wakati anahamia katika chama chao, Hamad amehama na mtaji mkubwa wa waliokuwa wanachama wa CUF na wanasiasa waandamizi wa chama hicho.

“Iko wazi Zanzibar tutachukua dola mapema tu. Wiki iliyopita viongozi wa chama walikuwa na ziara huko, hali waliyoiona inatupa uhakika wa kuchukua dola,” anasema Massaga.

Anaongeza kuwa kwa takwimu za mwaka jana chama hicho kina wanachama zaidi ya laki tisa na kwamba hadi kufikia Uchaguzi Mkuu idadi hiyo itakuwa imeongezeka.

Aidha, anasema chama hicho kiko kwenye hatua za mwisho za maandalizi ya Mkutano Mkuu unaotarajiwa kufanyika Machi mwaka huu, hatua anayosema inakwenda sambamba na kuandaa majina ya wagombea katika majimbo yote.

“Malengo ya chama chochote cha siasa ni kushinda uchaguzi na kushika dola, kwa sasa tunafanya mikakati yetu kwa kufanya vikao vya chini chini.

“Tumeviandikia barua vyombo vya dola viruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara, pia vitazame hali ya usalama wa nchi yetu,” anasema Massaga.

Hata hivyo, anasema chama chao kwa miaka minne kimeweza kuwatetea Watanzania wanyonge kwa kuyasemea mambo ya msingi kama kuwepo kwa bima za afya, masuala ya bei za vyakula na mengine mengi yanayohusu maisha ya wananchi wanyonge moja kwa moja.

“Kiongozi wa chama chetu na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, anawapigania sana wanyonge na kutetea demokrasia hapa nchini. Nadhani katika mitandao ya kijamii sisi tunaongoza kwa kuwasemea wananchi wa hali za chini,” anasema Massaga.

Hivyo, kupitia mambo ambayo kiongozi wa chama hicho amekuwa akipigania, Masaaga anaamini wananchi wamekielewa na ukifika muda wa uchaguzi watakuwa tayari kukipa ridhaa ya kuwaongoza kwa ajili ya kuwaletea maendeleo.

Kwa upande wake, NCCR-Mageuzi kimebainisha kuwa nacho kimeanza maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ingawa suala la kuungana na vyama vingine bado halijawa na muafaka ndani ya chama.

Florian Mbeo, Mkuu wa Oganaizesheni na Utawala wa NCCR-Mageuzi, anasema: “Sisi tunachojua mikutano iliyozuiliwa ilikuwa ya hadhara, lakini mikutano ya ndani ya chama chetu tuliendelea nayo hadi sasa tunafanya.

“Siasa zinaendeshwa kwa mbinu kama ivyoendeshwa vita yoyote ile, sisi NCCR-Mageuzi tulichagua mkakati wa kuendesha siasa zetu kwa mfumo tulioupa jina la ‘kimya kimya’.”

Anaeleza kuwa yatari wmeshapata wagombea katika majimbo 227 kati ya majimbo yote 264 kwa ajili ta Uchaguzi Mkuu ujao.

“Zanzibar tuna majimbo 18 ambayo yameshapata watu wanaotaka kugombea kupitia tiketi ya chama chetu kati ya majimbo 50 yaliyoko huko, sasa unaweza kuona tulivyojizatiti,” anasema Mbeo.

Anasema idadi hiyo ya wagombea inatoa picha na mwanga jinsi chama hicho kilivyo na ushawishi.

Akizungumzia idadi ya wanachama, anasema hadi kufikia Oktoba mwaka jana chama chao kilikuwa na jumla ya wanachama 2,813,000 na kuongeza kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka kadiri siku za uchaguzi zinavyokaribia.

Hata hivyo, anadai kuwa wananchi wanatakiwa kuzisoma sera na ilani za vyama vyao ili wapate muda wa kufanya uamuzi sahihi huku akieleza kuwa sera ya elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano imeasisiwa ndani ya chama hicho.

“NCCR tukichaguliwa tunawaahidi Watanzania kuboresha sekta ya elimu ili iwe bora zaidi. Tutawekeza kwenye kutengeneza watu ili wajitambue kwanza, na kupitia uwekezaji kwenye taaluma tutaweza kupata vitu vingi vizuri,” anasema Mbeo.

Anasema chanzo cha maendeleo duni kwa Watanzania ni mfumo wa siasa nchini kuwa juu ya taaluma huku akiahidi kuwa chama chao kitauvunja utamaduni huu pindi kitapopewa ridhaa ya kuongoza nchi.

“Kinachosababisha haya yote ni katiba tuliyo nayo, kwani inawapa madaraka makubwa viongozi wa kisiasa na kuwaacha nyuma wataalamu. Sisi tukipewa nchi tutaanza na kipengele cha taifa kupata katiba mpya,” anasema Mbeo.

Aidha, anasema suala la vyama kuungana ili vitoe mgombea mmoja atakayepambana na chama tawala ni jambo muhimu, na anabainisha kuwa chama hicho nacho kina mpango wa kusimamisha mgombea urais.

“Kuanzia Mei tutaanza kuchuja majina ya watu wanaotaka kugombea urais kupitia chama chetu. Tutazingatia sifa ya kujenga hoja na mtu anayeuzika na kupendwa na watu,” anasema Mbeo.

Naye, Abdullah Kambaya, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chama cha CUF anasema chama hicho kimejiandaa kutwaa majimbo katika mikoa minane katika majimbo ya Tanzania Bara na majimbo yote ya Unguja na Pemba ambako ni ngome ya chama hicho.

“Mpaka sasa tunajiandaa kutwaa majimbo yote katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga, Morogoro, Dar es Salaam, Mwanza, Tabora na Kigoma. Hii mikoa ni mikoa yetu kimkakati,” anasema Kambaya.

Anaeleza kuwa Januari 15, Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, ataanza ziara katika mikoa sita ya Tanzania Bara.

Anaitaja mikoa itakayotembelewa na mwenyekiti huyo kuwa ni Arusha, Tanga, Singida, Dodoma, Manyara na Morogoro kwa ajili ya kuzungumza na wanachama wa chama hicho.

“Mkakati wa CUF ni kusimamisha mgombe wa kiti cha urais wa Muungano na Zanzibar. Kama mpango wa vyama vya upinzani kuungana tukatoa mgombea mmoja upo, tukishirikishwa kwenye mchakato wa kumpata tutashirikiana,” anasema Kambaya.

Anasema wameandika barua kwa Jeshi la Polisi kuomba kufanya mikutano ya hadhara katika wilaya zote tano za Dar es Salaam na kwamba mikutano italenga kuuza sera na kaulimbinu yao ya ‘Haki sawa na furaha kwa Watanzania’.

Aidha, anasema wanalenga kufanya mikutano nchi nzima ili kuwaeleza wananchi kwa nini taifa linashika nafasi ya 153 katika nchi 156 zenye watu wasio na furaha duniani.

“Haiwezekani nchi yenye rasilimali za kila aina watu wake wakose furaha. Hapa kuna tatizo la sera, sera zinazoongoza nchi ni mbovu, tunataka kuwaambia Watanzania nini cha kufanya ili tujikwamue hapa tulipofikia,” anasema Kambaya.

Anaongeza kuwa demokrasia imeyumba kwa sasa nchini, hivyo CUF inalenga kuirudisha nchi katika misingi yake ya kidemokrasia kwa kuondoa mifumo yote kandamizi.

“Kuna msigano wa fikra, sisi tunataka demokrasia izingatiwe na uwepo umoja wa kitaifa. Haya mambo ya viongozi wa serikali za mtaa kupita bila kupingwa wanapata uhalali wa kuongoza kwa utashi wa sheria wala si kwa mapenzi ya raia, hii ni hatari. Tunatakiwa kupingana nayo, kwani huko mbeleni tuendako huenda tukazalisha viongozi wa juu waliopita bila kupingwa,” anasema Kambaya.