Tanzania hatujawahi kushuhudia kumangamanga ndani ya medani ya siasa kama wakati huu. Nasita kutamka kuwa wote wanaomangamanga ni wanafiki wa kisiasa, lakini ukweli ni huo kwa baadhi yao.

Kigeugeu nje ya siasa hawezi kuathiri majaliwa ya watu wengi, lakini anaposhika dhamana ya uongozi anapata fursa ya kuhatarisha maslahi ya wengi.

Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kutamka baada ya kustaafu uongozi kama Rais wa Kwanza wa Tanzania kuwa amelipitia Azimio la Arusha mara kwa mara kubaini kama lina kasoro zozote, lakini mara zote hakubaini hitilafu yoyote kwenye sera iliyopo ndani yake ya Ujamaa na Kujitegemea.

Mwalimu amekosolewa kwa mengi, lakini jambo moja ambalo wakosoaji wake hawatapata nguvu kulitaja ni imani yake, msimamo wake, na utetezi wake wa sera zake za siasa na uchumi. Alibaki mjamaa maisha yake yote na hakuona aibu hata siku moja kutetea msimamo wake.

Alikuwa na msimamo unaojulikana wakati wote na aliutetea kwa kadiri alivyoweza. Na hali hii kwangu ni sifa mojawapo ya msingi ya kiongozi: kuwa na msimamo thabiti wa jambo fulani hata kama ulimwengu mzima unakupinga.

Lakini hiyo pekee haitoshi; uwe msimamo ambao watu wengi wanaamini unajali na kuzingatia masilahi yao ya muda mrefu. Bila shaka kiongozi anayezingatia masilahi ya wananchi wengi ya muda mrefu atakuwa pia anazingatia masilahi ya nchi yake ya muda mrefu.

Leo tunashuhudia nini? Misimamo ni fasheni. Leo kiongozi anaweza kuvaa asubuhi shati la kijani na manjano, jioni akavaa shati la rangi nyekundu, bluu, na nyeupe. Kesho atarudia kijani na manjano, na mchana wa kesho akavaa gwanda la khaki. Cha ajabu wakipandishwa kwenye majukwaa ya siasa kukabidhi kadi za zamani mashabiki wa siasa tunawashangilia bila kuhoji lolote.

Wanachama wa vyama vya siasa, ambao kwa desturi za siasa kwenye nchi nyingi, ambao wao huwa mstari wa mbele kuwaadabisha viongozi vigeugeu ambao hawana msimamo wowote unaotetea kuhamahama kwa aina hii zaidi ya kutafuta nafasi za kugombea uongozi; wangeweza kujifunza mengi ya manufaa kutoka kwa mashabiki wa timu zetu za mpira wa miguu.

Sijawahi kusikia shabiki wa klabu ya Simba au Yanga kuhama timu kwa sababu mchezaji maarufu au kocha kuhamia timu nyingine na kusababisha matokeo mabaya, au kufungwa mfululizo. Siku zote wanachama wa klabu za mpira wa miguu hubaki walipo, lakini huwafungisha virago viongozi wao wanaochangia kudhoofisha timu.

Nadra kusikia shabiki wa timu kuhama kumfuata mchezaji, kocha, au kiongozi aliyetimkia timu nyingine. Ushabiki wa timu ni wa kudumu. Anayethubutu kugusa masilahi mapana ya wanachama na timu anahama yeye. Wachezaji wanafahamu hivyo, makocha wanafahamu zaidi, na viongozi wao wanatambua balaa linalowakuta pale wanapohitilafiana na masilahi ya wanachama wao. Masilahi ni ya timu, hayawi ya mtu mmoja mmoja.

Mashabiki wa mpira wanatufundisha na kutuangazia kuwa ipo nguvu kubwa ya wanachama ambayo ikitumika ipasavyo inalinda, siyo tu hadhi ya timu nzima – iwe ya timu ya soka au ya chama cha siasa – bali pia inawajibisha viongozi ambao wanasahau wajibu wao kwa wanaowaongoza. Ni pale mwanachama anaporuhusu viongozi kupora hiyo nguvu au anaposahau kuwa anayo hiyo nguvu ndipo inajitokeza fursa kwa viongozi kusahau wajibu wao kwa timu na kujijengea nguvu binafsi ambayo inadhoofisha nguvu ya wanachama.

Mwanachama, hata kama ni hai kwa mujibu wa kanuni za timu au chama chake, anabaki mwanachama butu asiye na nguvu zozote za kuuadabisha uongozi ambao anaamini unasahau masilahi mapana ya timu au chama chake.

Yanayotokea sasa kwenye siasa yanatufundisha kuwa hata wale vigeugeu wanaohama kutoka upande mmoja kwenda mwingine wanayo nguvu kubwa na ushawishi wa kuwabeba mashabiki wao kule waendako.

Na muda unavyozidi kujongea ndani ya hali hii wanachama wanakuwa wanyonge, waoga, na siyo waelekezaji wa wale wanaosimamia masilahi yao na masilahi ya wengi; badala yake wanakuwa waelekezwaji wanaoyumbishwa kwa kusikiliza zaidi wale wanaopaswa kuwasikiliza.

Shabiki wa soka ana msimamo thabiti. Tunatarajia kuwa hata rangi ya vuvuzela yake itakuwa ina rangi za timu yake. Hatutarajii awe anabadilisha rangi za vuvuzela kila kukicha.

Masilahi ya timu, masilahi ya chama, au masilahi ya Taifa yanalindwa na wanachama wa timu, wa chama, au raia wa Taifa hilo. Viongozi wanapaswa kuakisi masilahi ya wengi. Ni pale tu wanapobaini udhaifu katika misimamo ya wale wanaowaongoza ndipo wanapopata nafasi ya kupenyeza masilahi yao.

Kukosekana kwa dhamira madhubuti ya wanaoongozwa katika kusimamia masilahi yao – na viashiria vipo kuwa hali hiyo ipo sasa – ndiyo tunashuhudia kutokea kwa hali ya viongozi kuwa na nguvu kubwa ambayo hawastahili kuwa nayo juu ya wanaowaongoza.

Misimamo ya viongozi na wapenzi wa klabu za soka siyo ya kufikirika, ni ya kweli. Nilishuhudia misimamo hiyo thabiti siku viongozi na wazee wa Klabu ya Yanga walipotembelea Butiama miaka kadhaa iliyopita kumsalimia Mama Maria Nyerere. Wakati wa kuwatambulisha kwake ulimi uliteleza nikawatambulisha kuwa ni viongozi na wazee wa Klabu ya Simba.

Wale wazee walihamaki na kunisahihisha mara moja. Mimi nilicheka kwa kutambua kosa langu. Wao hawakucheka na wala hawakuona sababu ya kucheka kwa kosa kubwa kama lile. Waliniambia wao ni Yanga, siyo Simba. Naweza kuongeza leo kuwa wangepata muda zaidi wangenifahamisha kuwa wasingeweza kuwa Simba hata siku moja. Walipotembelea viongozi na wachezaji wa Wekundu wa Msimbazi sikurudia kosa lile.

Nilijifunza wakati huo kuwa shabiki wa mpira wa miguu ana msimamo mkali na siyo wa mzaha. Hatetereki, habadiliki, na hayumbishwi. Na kama kuna tatizo kwenye timu yake anatafuta suluhisho akiwa humo humo.

Naamini msimamo wa aina hii wa mashabiki wa mpira wa miguu ukiwekwa kwenye siasa tutakuwa na vyama imara na wanachama watatafuta mabadiliko wanayoyataka ndani ya vyama hivyo badala ya kuhamahama kunakoonekana sasa.