Wiki iliyopita katika Safu hii ya Fasihi Fasaha, nilizungumzia kupata rais safi inawezekana Watanzania watapotimiza wajibu wao. Nilikusudia kuzungumza na Watanzania ambao ndiyo wapigakura wenye uamuzi wa kupata rais safi.
 Makala ile imechangiwa na wasomaji wengi wakiunga mkono na kuhoji watamjuaje rais, mbunge au diwani safi? Baadhi yao wameeleza katika chaguzi kuu zilizopita walihamasishwa na kushawishiwa na viongozi wa vyama vya siasa, Serikali na dini kuwapigia kura hao ambao walionekana safi. Lakini matokeo yake ikawa theluthi moja safi na theluthi mbili chafu!
 Nikiri kusema hilo si lengo la kupata theluthi moja. Nia ni kupata kitu kizima kwa maana ya kupata viongozi wote safi. Kama hapakuwa na budi, tungepata sudusi tano ya viongozi safi! Wala pasingekuwa na mjadala.
 Baadhi ya wachangiaji wameonesha mashaka yao makubwa kuhusu rais safi atapatikanaje? Naomba kurejea maelezo yangu kwa njia ileile ya kukumbusha kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
 Mwalimu Nyerere anasema; “Mpeni mgombea ambaye atakidhi matarajio ya wananchi. Watanzania wanataka mabadiliko, wasipoyapata ndani ya CCM watapata nje ya CCM. Tunataka kiongozi atakayesema rushwa kwangu mwiko.”
Ni ukweli Watanzania na hasa wananchi wazalendo tunahitaji rais atakayesema rushwa kwake mwiko, kwa sababu leo nchi yetu inanuka rushwa na rushwa hiyo imeshakuwa ni tabia kwa viongozi na wananchi.
 Baadhi ya migogoro mingi inayotokea nchini kati ya viongozi na wananchi, wakulima na wafugaji, wanafunzi na walimu, watabibu na wagonjwa, polisi na raia, mahakimu na watuhumiwa na kadhalika inasababishwa na watu kuendekeza rushwa kama jibu la mahitaji na tiba ya shida zao za kimaisha.
 Hayo tunayaona wakati tunapotafuta elimu, tiba, haki, ajira na usalama. Angalia uporaji wa ardhi, utoroshwaji wa wanyamapori kwenda ughaibuni, ujangili kwa wanyamapori, ujahili katika vituo vya usalama kuvamiwa na kuporwa silaha, ukabila na chuki ni matokeo ya kutoa na kupokea rushwa.
Umaskini umejaa mifukoni hadi kuwa ni mazoea yanayomfanya mwananchi wa hali ya chini kukosa malazi safi, mavazi mazuri na chakula bora kuwa huduma hizo si haki yao na kuwaona mafisadi na watoa rushwa ndiyo wenye haki ya huduma hizo muhimu.
 Udini umekuwa kinyume na imani ya dini hata kuwavaa baadhi ya viongozi wa dini kufanya ghilba kwa waumini wao na kuonesha sura mbili ya utakatifu na ya ubazazi. Leo tunashuhudia viongozi hao wakiuza mali za wakfu na kushiriki kwenye ufisadi. Mambo yote hayo mama yao ni rushwa.
Ndiyo maana tunahitaji kiongozi au rais safi atakayesema rushwa kwake mwiko. Awe na uwezo na uthubutu wa kumwambia ndugu na marafiki zake kuwa rushwa kwake ni haramu na atawasulubu hao jamaa zake watakaohalalisha rushwa.
 Kwa maelezo hayo ndipo anapoingia Rais Kikwete anaposema kuwa wananchi watoe viongozi safi kwa sababu watu safi wanawajua kutokana na kauli na vitendo vyao ni vya ukweli vya kila siku huko mitaani na vijijini.
 Leo, wananchi tunawajua viongozi wetu. Baadhi yao wamepata madaraka kwa kutoa rushwa, na wapigakura walipokea rushwa, ima kwa kujua au kutojua. Nakiri kusema matendo mengi ya rushwa yalifanywa kwa kujua.
 Wapigakura wa Tanzania kama mnaweza kuwafahamu na kuwaonesha hadharani walevi, washarati, wezi, majambazi na majahili, vipi mshindwe kumjua rais safi au kiongozi safi kwa kunusuru maisha ya wananchi?
 Watanzania wapigakura tuacheni purukushani zetu, nchi inakwenda arijojo na huo utakuwa mwisho wa Tanzania kuwa kisiwa cha amani, nchi yenye rutuba na rasilimali kedekede. Ni vyema tukaiona rushwa ni sawa na saratani kwani tunapoibaini saratani na mwisho wa uhai umefika. Tuiogope.
Nakumbuka kati ya miaka ya 1960-1990 tulikuwa na msemo mmojawapo uliojinadi kwa maneno yafuatayo;  "Kufanya kosa si kosa bali kosa kurudia kosa.” Msemo huu uliamsha hamasa na kuwafanya Watanzania kuacha kufanya makosa kwa makusudi. Nani kafuta msemo huu?
 Tujipime na kujitazama katika chaguzi zilizotangulia kama tulifanya makosa ya kuweka baadhi ya viongozi watoa rushwa na sisi kupokea rushwa, sasa tuache. Tukipokea na kutoa rushwa tutafanya kosa. Na mwenye kukosa hustahili adhabu.
 Ndiyo maana hivi leo, Watanzania tunasaga meno na kulia rushwa! rushwa! rushwa! Wakati mafisadi wanatabasamu na kutoa maneno yaliyojaa kejeli, kiburi na kupuuza mamlaka tulizojiwekea. Kura zetu zinatuangamiza! Tuseme basi, inatosha.
 0717/0787 – 113 542