Nilisoma katika gazeti moja la kila siku Jumatatu, Machi 16, 2020 lenye kichwa cha habari ‘WAPATATISHWE’ na chini yake palikuwa na maneno yalisomeka hivi: ‘Ni ushauri wa viongozi wa dini na wachambuzi kutokana na msuguanao baina ya wanasiasa na vyombo vya dola’. Hayo yaliandikwa ukurasa wa mbele kabisa.
Binafsi nilivutiwa kusoma ndipo nikataka kujua kwa undani habari ile ilikuwaje. Na kweli kwenye uk. 4 ndani ya gazeti lile yaliandikwa maelezo kwa kirefu chini ya kichwa kile kile – ‘WAPATANISHWE’ lakini kuliongezeka andiko lisemalo ‘MUSTAKABALI WA TAIFA’.
Baada ya kusoma maelezo yale kwa undani katika ukurasa ule wa nne ninafikiri mwandishi wa kichwa hiki cha habari kwa kweli hakuwatendea haki viongozi wa dini.
Mwandishi alidiriki kuandika: ‘Ni ushauri wa viongozi wa dini na wachambuzi kutokana na msukumo baina ya wanasiasa na vyombo vya dola’.
Jambo hili si la kweli na halikustahili kuandikwa vile. Katika matamko yote ya wale viongozi wa dini katika habari ile hakuna palipoonyesha kuwa Kamati ya Amani yenye kujumuisha viongozi wa dini zote wamekaa, wametafakari na hatimaye wakatoa tamko la ujumla namna ile ‘WAPATANISHWE’. Hakuna tamko la namna hiyo kutoka BAKWATA, TEC au CCT hapa nchini.
Kinachoonekana pale ni matamshi ya kila kiongozi alivyoguswa. Mathalani Baba Askofu Shoo, ametamka: “Inasikitisha sana” na akawa anajiuliza: “Tunaelekea wapi kama taifa?” Mwishoni akashauri kuwa wanasiasa waache kutumia nafasi zao vibaya! Tofauti zao zisiwe sababu ya kuchukiana kiasi cha kuumizana. Huo ni ushauri wenye kulenga kuwepo kwa amani hapa nchini.
Yule Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum, alionyesha kinachotakiwa ni wananchi na wanasiasa kutii sheria bila kushurutishwa na vyombo vya dola. Kisha akaonya kwa kusema: “Tusiwekee ujeuri vyombo vya dola kwa sababu haviulizwi.” Papo hapo akashauri vyombo vya dola kutumia nguvu pale inapobidi kulingana na jambo lenyewe. Nguvu zisitumike kila wakati. Hapo ni wazi hakutamka suala la huko kupatanishwa.
Na Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, alisema ni muhimu viongozi waliopo madarakani watambue kuwa Watanzania wote wana haki ya kikatiba ya kuongoza taifa. Akashauri waache wapinzani nao wafanye siasa kupitia vyama vyao.
Basi kwa maoni hayo kutoka viongozi mbalimbali wa dini inawezekanaje mwandishi atokee na kuandika kiujumla jumla tu, ‘WAPATANISHWE’ eti ni ushauri wa viongozi wa dini?
Wapi viongozi hawa wa dini wametamka hilo? Kama mwandishi alikuwa na ajenda yake, basi alipaswa aiseme yeye mwenyewe waziwazi na si kupitia kwenye mgongo wa viongozi wa dini.
Lakini ni jambo la kawaida kwa waandishi kutafuta vichwa vya habari vinavyovutia wasomaji. Labda ndilo lilikuwa lengo la mwandishi yule. (Tazama Mwananchi toleo la 7162 la tarehe 16/03/2020)
Nielewavyo mimi viongozi wetu wa dini wako makini sana katika kutoa matamshi yao katika mambo nyeti kama ya kisiasa, ya kiserikali na ya vyombo vya dola.
Upo mwongozo katika maandiko matakatifu (Biblia) aliotoa Mtume Paulo kwa Warumi juu ya tabia mbele ya mamlaka ya serikali. Imeandikwa hivi, naomba ninukuu: “Kila mtu atii mamlaka iliyo juu; kwa maana hakuna mamlaka isiyo toka kwa Mungu. Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu. Nao washindanao watajipatia hukumu. Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi wataka usimwogope mwenye madaraka? Fanya mema; nawe utapata sifa kwake. Kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu kwako na kwa ajili ya mema. Lakini ufanyapo mabaya ogopa…” (Warumi sura ya 13, mstari 1-4). Mwisho wa kunukuu.
Kusema tu “WAPATANISHWE” mara moja kuna kuja akilini dhana ya kuwa pamekuwa na ugomvi kati ya mtu na mtu au kati ya kikundi na kikundi; au tu umetokea mtafaruku au msuguanao na wahusika wapo ndipo hoja hii ya kupatanishwa inaingia mahali pake.
Mwandishi wa habari ile alipaswa kuwa muwazi bila kufumbafumba au kutoa kichwa cha habari kwa ujumla namna ile. Nafikiri alishikwa na woga asije akazuliwa jambo asilolikusudia katika habari yake.
Hapa alipaswa kuchukua tahadhari wasomaji nao wasije kumwelewa vibaya ndiyo sababu ninasema haikuwa sahihi kuwataja viongozi wa dini kama nao wametoa tamko lile. Kumbe hawakutoa.
Waingereza wanasema si salama kutoa tamko la jumla jumla namna ile na wanaita tamko namna hii kuwa ni “SWEEPING STATEMENT”, yaani kauli ya jumla.
Kauli namna hii hazisaidii kulijua tatizo, pia kulitafutia ufumbuzi wake. Inafaa waandishi waweke wazi (pin point) yale wanayodhani yanaleta mtafaruku nchini kwa nia ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu.
Hebu tutafakari adha ya tamko la jumla la namna ile. Ni kweli tuamini kuwa wanasiasa wetu na vyombo vya dola wanamsuguano? Au hapa mwandishi ametumia ule usemi au ile methali isemayo: “Samaki mmoja akioza, basi tenga zima la samaki linanuka?” Ndiyo kusema mwanasiasa mmoja au chama cha siasa kimoja kinavurugana na chombo kimoja cha dola, tunaweza kweli kwa usalama kabisa tukajumlisha kimatamko, vyama vya siasa vyote au vyombo vyote vya dola?
Hiyo haitakuwa sawa sawa. Mwandishi anatakiwa aweke wazi mhusika na chombo cha dola husika na hapa kuomba ule ushauri wa kupatanishwa. Huo ni utata wa kimantiki na sisi Wangoni tunasema kilugha: ‘Iyi hinu NDINDANI’, tukimaanisha: “Huu sasa ni utata usioeleweka.”
Hapo wale wanaosuguana kwa kupishana lugha hata kufikia kutunishiana msuli ndio wawekwe pamoja na kupatanishwa.
Serikali kamwe haiwezi kusuguana na raia wake watiifu wa sheria. Na chombo cha dola chenye jukumu la kulinda raia na mali zao kamwe hakikamati raia wema na watiifu wa sheria.
Hapa mwandishi alitakiwa awe muwazi (be very specific) katika kuandika tukio au matukio ambamo umetokea msuguano kati ya wanasiasa na vyombo vya dola. Ndipo lile wazo la kutaka wapatanishwe lingestahili kutolewa lifanyiwe kazi. Hapo kingeeleweka na ushauri namna ile ungepongezwa na wananchi.
Historia ina tabia ya kujirudia yenyewe hapa ulimwenguni (history repeats itself or reoccurs). Enzi za TANU mwaka 1958, serikali ya mkoloni haikuiva na Chama cha upinzani cha TANU. Rais wa TANU wakati ule Mwalimu Julius Nyerere alikamatwa na kushitakiwa kwa UCHOCHEZI hapa nchini.
Rais yule wa TANU alipelekwa mahakamani na kushitakiwa kwa makosa matatu ya uchochezi. TANU iliweka mawakili watatu; Mwingereza mmoja kutoka Uingereza anaitwa DN Pritt QC na Wahindi wawili wa hapa nchini, Mahamoud Rattansey na K. I. Jhaweri.
Kesi ile iliunguruma kuanzia Julai 9, 1958 mpaka Agosti 13, 1958 ilipotolewa hukumu. Siku ile ya hukumu Wana TANU maelfu kwa melfu walikusanyika pale Mahakama ya Kivukoni Front kuja kusikiliza hatima ya kiongozi wao Rais wa TANU.