Watu wasiopungua 15 ikiwemo mwandishi habari mmoja wameuawa leo kwenye Ukanda wa Gaza kutokana na mashambulizi ya vikosi vya Israel na kufanya idadi ya Wapalestina waliouawa tangu Oktoba 2023 kupindukia 50,000.

Taarifa kutoka Ukanda wa Gaza zinasema vikosi vya Israel viliyalenga mahema yaliyofungwa nje ya hospitali mbili kubwa za ukanda huo alfajiri ya leo Jumatau na kuwaua watu wawili papo hapo akiwemo mwandishi habari.

Nje ya hospitali ya Nasser kwenye mji wa Khan Younis mahema yaliwaka moto uliosababisha kifo cha Yousef al-Faqawi, mwandishi habari wa tovuti ya habari iitwayo Palestine Today.

Mikanda ya video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii imemwonesha mwandishi huyo akiwa anawaka moto huku mtu aliyekuwa karibu naye akijaribu kumwokoa na kuuzima.

Hata hivyo muda mfupi baadaye matabibu kwenye Ukanda wa Gaza walitangaza kwamba Yousef na mtu mwingine mmoja walipoteza maisha. Mwandishi habari mwingine aliyeshuhudia mkasa huo Abd Shaat amesimulia kilichotokea

“Mnamo saa 9 alfajiri tuliamshwa na mlio mkubwa wa mlipuko. Tukatoka nje ya mahema ndiyo tukaona hema alimokuwemo mwezetu limelengwa. Lakini sisi tutaendelea kuripoti na kutoa taarifa za ukweli kwa ulimwengu mzima. Huo ni wajibu wetu wa kibinaadamu.”