Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia Dar es Salaam

Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya vitambulisho nchini (NIDA) James Kaji amewataka Waandishi wa Habari ,kusaidia kutoa elimu kwa jamii kwenda kuchukua vitambulisho vyao kwa wale ambao wamepata ujumbe kutoka NIDA.

Kaji ametoa wito huo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika ofisi za NIDA Makao makuu,amedai tangu kuanza kwa zoezi la ukusanyaji wa vitambulisho na kutuma ujumbe mfupi mwezi Januari 2025, hadi kufikia tarehe 23 Machi 2025, jumla ya wananchi 1,880,608, sawa na asilimia 157 ya wale ambao hawajachukua vitambulisho vyao, wameweza kupokea ujumbe huo.

Kaji amesema jumla ya sms 680,608 zilitumwa, na hivyo kufanya idadi ya sms zote kufikia 1,880,608, kwa waombaji wapya waliojiandikisha katika kipindi hiki na ambao vitambulisho vyao vimechapishwa tayari.

“Kulingana na takwimu hizo, idadi ya wananchi waliojitokeza kuchukua vitambulisho baada ya kupokea sms ni 565,876, ambayo ni sawa na asilimia 30 tu ya watu wote waliotumiwa ujumbe”Amesema.

Kaji amedai ingawa kuna jitihada nyingi zinazofanywa na NIDA , bado kasi ya watu kujitokeza kuchukua vitambulisho haijaridhisha.

Hivyo, inaonekana kwamba karibu watu wote ambao hawajachukua vitambulisho vyao wamepata ujumbe mfupi wa simu

Aliongeza kuwa wakati wa ukusanyaji wa vitambulisho kutoka ofisi za kata, vijiji, na mitaa, walikuwa na vitambulisho 1,200,000 ambavyo havijachukuliwa na wahusika.

“NIDA ilijitahidi kuhakikisha kuwa, vitambulisho vyote vinachukuliwa na wahusika, walipunguza masharti.

Kila mtu ambaye hawezi kufika katika wilaya aliyoelekezwa kuchukua kitambulisho chake, anaweza kumtumia ndugu au jamaa kumchukulia kitambulisho, kwa sharti tu amtumie ujumbe alioupokea kutoka NIDA”Amesema.

Katika mazungumzo yake, alisema kuwa moja ya sababu zinazochangia kuchelewa kwa wananchi kuchukua vitambulisho ni kwamba wanatumia Namba za Utambulisho wa Taifa (NINs) kupata huduma zote kama ilivyo kwa mtu mwenye kitambulisho, hivyo wengi hawana hamu ya kufuata vitambulisho vyao.

Kaji amesema kutakuwa na ukomo wa matumizi ya namba ,kwa kuzingatia kwamba tayari tumewatumia ujumbe wa SMS kwa watu wengi ,ambao vitambulisho vyao vilikusanywa kutoka kwa serikali za Vijiji, Mitaa, Vitongoji, Kata, na Shehia na walipokea ujumbe na hawajachukua vitambulisho vyao katika wilaya zao.

“Kuanzia tarehe 1 mei 2025, tutafunga matumizi ya nambari hizo, lengo letu pamoja na Serikali ni kuhakikisha kila kitambulisho kilichotengenezwa kinachukuliwa, kwani kimegharimu fedha nyingi katika utengenezaji wake.

Pia katika hatua nyingne NIDA wanatarajia kuzindua mpango wa Jamii namba katika mikoa mitatu

akizungumzia mpango huo ,Kaji amesema wanatarajia kuanzisha Mpango wa Majaribio wa Usajili wa Jamii Namba, kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18 kwenye wilaya tatu.

Amesema usajili huo utaanza kwa majaribio .katika mikoa mitatu ya Kusini Unguja, Kilolo Iringa, na Rungwe Mbeya, ambapo wanatarajia kusajili jumla ya watu 235,826.