WANUNUZI wa zao la pamba wameishukuru Serikari kwa kuweka mfumo mzuri wa ununuzi wa zao hilo, ambalo kwa mwaka huu linauzwa kupitia katika minada inayosimamiwa na Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS).
Hata hivyo wanunuzi hao wameiomba Serikali kuziwezesha AMCOS kuwa na maghala makubwa na ya kisasa ya kuhifadhia pamba, lengo likiwa ni kuhakikisha pamba inahifadhiwa kwenye maeneo salama na kuifanya isipoteze ubora.
Kauli hiyo imetolewa jana (Jumanne, Juni 12, 2018) na mmoja wa wanunuzi hao ambaye ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya NGS Investment LTD, Bw. Emmanuel Dandu alipokuwa akizungumzia kuhusu kuanza kwa uchambuaji wa pamba kwa msimu wa mwaka huu.
Alisema awali kabla pamba haijaanza kuuzwa kupitia AMCOS suala la ubora lilikuwa halizingatiwi sana na wakulima kwani pamba yake ikikataliwa na kampuni moja alikuwa na uhuru wa kuipeleka kwenye kampuni nyingine na, jambo ambalo lilichangia kuisha thamani.
Hata hivyo ameiomba Serikali kuwajengea uwezo viongozi wa Ushirika ili waweze kutekeleza majuku yao kikamilifu na pia isaidie kutoa elimu kwa wanachama juu ya umuhimu na faida za AMCOS ili wakulima wengi waweze kujiunga.
Bw. Dandu ambaye kampuni yao ya NGS Investment LTD, licha ya kujishughulisha na biashara nyingine, pia inamiliki kiwanda cha kuchambua pamba cha Majahida kilichopo wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, ambayo tayari imeshaanza zoezi ya uchambuaji pamba.
Alisema pamba inayochambuliwa katika kiwanda hicho wanainunua kupitia AMCOS walizopangiwa, ambapo alipongeza mfumo huo kwa sababu unawawezesha kupata malighafi kwa urahisi na kwa wakati.
“Wanunuzi wote tunanunua pamba kupitia AMCOS. Serikali imeweka mfumo mzuri unaotuweza wote kununua pamba kadiri ya uwezo wetu. AMCOS zimeagizwa kuuza pamba kwa wanunuzi wote bila ya ubaguzi, tofauti na miaka ya nyuma” alisema.
Akizungumzia kuhusu uwezo wa kiwanda hicho, alisema kina uwezo wa kuchambua tani 40,000 za pamba kwa mwaka, lakini wanalazimika kuchambua wastani wa tani tano hadi 12 kutokana na changamoto ya upatikanaji wa pamba ya kutosha pamoja na changamoto ya umeme wa uhakika.
Pia aliiomba Serikali iwasaidie wakulima kwa kuwapatia pembejeo kwa wakati pamoja na kuwapa elimu ya mara kwa mara juu ya kulima kwa kufuata kanuni bora za kilimo cha zao la pamba, ikiwa ni pamoja na kupanda kwa wakati ili waweze kujiongezea tija.
Alisema kwa sasa kiwanda hicho kina jumla ya wafanyakazi 300, ambao kati yao 62 ni wa waajiriwa wa kudumu na waliosalia ni vibarua.
Bw. Dandu alisema marobota yanayotengenezwa kiwandani hapo yanakuwa na uzito wa kilo 200 hadi 220, huku wateja wao wakubwa ni Cotton Distributors Inc (CDI) ya nchini Uswisi, Saurashtra Cotton and Agro Product PVT LTD ya nchini India.
Wengine ni Awatac Impex PTE LTD ya nchini Singapore pamoja na viwanda vya nguo vya ndani ya nchi kikiwemo cha Mwatex cha jijini Mwanza. Alisema matarajio ya kampuni hiyo ni kuanzisha kiwanda cha kutengeza nyuzi ili kuongezea thamani ya pamba kabla ya kuiuza.
Aidha, Meneja huyo alisema mbegu zinazopatikana baada ya pamba hiyo kuchambuliwa pamba zinapelekwa moja kwa moja katika kiwanda cha kukamua mafuta ya kula na mashudu huuzwa kama chakula ya mifugo.
Kuhusu mabaki yanayopatikana baada ya mafuta kuchujwa, alisema yanatumia kwa kutengeneza sabuni za kufulia, ambazo wanaziuza kwa wananchi.