Turudi enzi za Mzee Jumbe, Rais wa Awamu ya Pili, huko Visiwani. Utawala wake ulidhamiria kuleta mageuzi makubwa kule Visiwani. Kwanza alifikiria urais kamili hivyo aliotea nchi huru ya Visiwa vya Zanzibar. Katika azma hiyo alijikuta anawaingiza vijana wasomi katika medani ya uongozi wa nchi ile. Kumbe kwa kufanya vile alishtukia akishiriki kutenda DHAMBI ya kuwanyanyapaa na kuwanyanyasa waasisi wa Mapinduzi yale matukufu ya Januari 12, 1964. Kwa Kiingereza ningeweza kusema “he side-passed them, he neglected them completely”!

Kama siyo kwa busara za mwasisi mkuu. Mzee Karume, kuwalazimisha kila mmoja MBM wale kujengewa jumba kubwa, bila shaka enzi ya Jumbe wangefikia hatua ya kulala kwenye makuti, kingoni tunaita “masakasaka”. kumbe MBM wote wale waasisi wana majumba kabambe kule Mazizini, Kilimani hata Mtoni kwa rafiki yangu Mzee Edington Kisasi. 

Enzi za Jumbe baada ya kupata Katiba na Baraza la Wawakilishi wale wazee waasisi hawakuthaminiwa kamwe. Wazee wale mashujaa wa Mapinduzi ya 1964 wakajikuta wamo katika hali ngumu sana baada ya Katiba mpya ya Zanzibari 1984, hadhi ya Baraza la Mapinduzi ilizimuliwa uwezo wake (diluted its influence or powers) kwa kuundwa BARAZA LA WAWAKILISHI. Kisheria sasa waasisi hawa wa Mapinduzi hawakuenziwa, hawakuwa na nguvu zile walizojinyakulia mwaka 1964. Hili kwa usahihi kabisa liliweza kuwaathiri wazee wale waasisi kisaikolojia katika maisha yao. 

Matokeo ya hali hiyo vigogo waliotisha enzi za awamu ya kwanza kama akina Kanali Seif Bakari Omar, Saidi Natepe, Brigedia Yusuf Himidi, Kanali Hafidh Suleman, Mzee Edington Kisasi aliwatengua nguvu zao hata ilifikia wakati Kanali Seif Bakari alitiwa kizuizini na alimalizia maisha yake akiwa DC wa Kisarawe. Mzee Natepe na Yusuf Himidi walihamishiwa bara JWTZ, wengine walipuuzwa tu (merely reglected as such).

Inaonekana sana kwa mawazo ya Mzee Jumbe alianza kumjenga kijana Seif Shariff Hamad. Akamteua kuwa Katibu wake Maalum, kisha akampandisha cheo kuwa Waziri wa Elimu na kwa kumkomaza kisiasa akampendekeza kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, akaja kuingia katika Kamati Kuu. Hapo sasa akawa kamuandaa kuwa msaidizi wake mkuu. Akaja kuwa katika Sekretariati ya Idara ya Mipango na Uchumi ya Kamati Kuu ya CCM. 

Ulifika wakati Maalim Seif Shariff Hamad akateuliwa kuwa Waziri Kiongozi wa SMZ (kama sikosei miaka ile ya 1983-1984). Kuanzia hapo vijana wasomi wa Visiwani walishika hatamu za utawala wa SMZ. Ndipo Mzee Jumbe akamrudisha Bara Jaji Damian Lubuva na nafasi yake kama Mwanasheria Mkuu wa SMZ akaajiriwa Mnigeria akiitwa Bashir Swanz na kuanzia hapo Mzee Jumbe akatafuta njia za kupata mfumo mwafaka wa Muungano utakaowafaa Wazanzibari kuwafanya huru kuliko ilivyo katika Muungano wa sasa.

Inasemekana kuna wakati uamuzi mkuu kule SMZ ukifanywa na watu watatu tu; Rais, Waziri Kiongozi na huyo Mwanasheria Mkuu, Bashir Swanz; Mzee Jumbe alikuwa na mtazamo wa Zanzibar huru nje ya Muungano. 

Ndipo SMZ walipoanza kudai Bendera ya Taifa ya SMZ, wimbo wa Taifa na hatimaye huo Uhuru kamili wa kujiamulia mambo ya Kizanzibari. Basi wakati huu ndipo akajiwa na ile fikra ya kutaka Mkataba na Muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Ikaandaliwa ‘paper’ ya kupeleka Kamati Kuu ya CC na hatimaye NEC ya CCM ijadiliwe hiyo hali ya ‘antonomy’ ya Visiwani.

La haula Walaa Quwata illa billahil aliyul’Aaadhym – sijui ilitokeaje ikawa lile kabrasha au niseme waraka maalum ukavuja na kumfikia Mwalimu kabla Mzee Jumbe hajauwasilisha rasmi alivyotarajia. Mwandishi mmoja wa makala katika Raia Tanzania Toleo No. 0541 la Jumamosi tarehe 2 Januari 2016 Uk. 21 anauliza ilikuwaje Profesa Babu alikwepa kujiunga na CUF akasema, mwaka 1990 Profesa Babu aliwauliza hadharani uongozi wa CUF wakati huo Maalim Seif Shariff Hamad akiwa Makamu Mwenyekiti; Maalim Seif awaeleze wajumbe wa CUF kipi alichozungumza yeye na Mwalimu Nyerere wakiwa wawili tu faragha pale Msasani nyumbani kwa Mwalimu? 

Hoja ile ya Profesa Babu haikujibiwa na tangu hapo wanachama wa CUF wakasema Babu ee, itakuwaje mtu wa Unguja awe Mbunge wa Pemba na mwananchi wa Pemba awakilishe wa Unguja? Tangu hapo profesa hakuweza kujiunga na CUF ukawa mwisho wa uhusiano wake na CUF. 

Basi, kwa vile huko mwanzo nilisoma meseji ile iliyoniomba nitoe ushauri, ndipo sasa mimi katika udokozi wangu nimekusanya mawazo hayo kutoka waandishi mashuhuri wa makala kuhusu matatizo ya siasa za Wazanzibari. Hatimaye mmoja wa waandishi amesema, “Wazanzibari kataeni kuabudu mizimu” huyu ameeleza kwa ufasaha. Kwa kifupi ameonesha namna Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alivyowashauri wajumbe wa Baraza la Mapinduzi Oktoba 1987 wakati anaaga aking’atuka uenyekiti wa CCM ili kumpisha Mzee Mwinyi, namnukuu, “…kusema kweli Rais Abeid Amani Karume alikuwa kielelezo cha ukatili na ukandamizaji. Visiwani alitawala kwa mkono wa chuma. Nasema kilichotokea ni kile nilichobashiri kingetokea, kwamba Wazanzibari wakaanza kuuana wao kwa wao na baadhi wasio na hatia waliouawa kikatili na ambao hawakuwa wanachama wa HIZBU wala chama chochote bali ASP waliuawa mmoja baada ya mwingine, hivyo hivyo na kwa ukatili wa kutisha”. (Tazama Raia Tanzania Toleo No. 0438 Uk. 15).

Katika kikao kile cha kuwaaga Wazanzibari Mwalimu alisema, yeye binafsi hakuridhia ukatili ule wa Baraza la Mapinduzi siku zake za mwanzo mwanzo akawaambia namnukuu, “Hamuwezi kuepuka dhambiI ya umwagaji damu huu, vitisho na vurugu na wala Baraza hili haliwezi kuwatumia vyema Wazanzibari kwa kuwa limegubikwa na ukatili mkubwa dhidi ya baadhi ya Wazanzibari”. 

Hatimaye alimalizia hotuba yake ile kwa kuwaambia, “Mungu husamehe! ni wangapi kati yetu tutastahili kuwa na matumaini ya Paradiso kama Mungu atang’ang’ania dhambi zetu wakati wote? “Alihoji. Hapa mimi nasema Mwalimu alikumbuka ile Zaburi ya sura ya 130 aya ya 3-4, Mwalimu aliendelea kuwasihi Wazanzibari kwa maneno haya, “Leo watu wanakumbushwa kwa kuambiwa, “Wewe ulikuwa HIZBU na wengine wanakumbushwa “Baba yako, kama si pamoja na babu yako walikuwa HIZBU”. Sasa nizipeleke wapi dhambi za baba au babu yangu? 

Mwalimu aliwaasa Wazanzibari kuwa huu ni ubaguzi mbaya na wa kujinga. Vyama vya HIZBU, ZPPP sasa ni MFU. Kwa jina la mbingu kwa nini HIZBU mfu itughadhibu leo kana kwamba juzi ndiyo leo?” Usia huo wa Mwalimu unafuatwa? Sijui kama Wazanzibari wanaufuata huo usia wa Baba wa Taifa. 

Uwazi hapa ni huu; Wazanzibari wasahau yaliyopita wagange yanayokuja mbele yao katika mazingira ya wakati huu tunaoishi sisi wa leo. Kama tukifuata usia ule wa Baba wa Taifa ninaamini Wazanzibari wanaweza kabisa kumaliza uhasama wao wote. Hatua ya kwanza Upemba sasa katika uongozi wa juu ndiyo wao. Kiongozi wa CUF ni Mpemba na Makamu Mwenyekiti wa CCM Visiwani ni Mpemba hapo hakuna kabisa lile wazo la Wapemba kunyimwa urais wa Zanzibar. Kilichopo ni dhana potofu ya vyama mfu vya ASP na HIZBU ambayo Baba wa Taifa aliiongelea sana mwaka 1987. Basi upuuzi wa kuogopa vivuli vya mizimu ya vyama mfu ukisahaulika mwafaka utapatikana. 

Bado naona Mzee Lowassa aliyepata Tuzo la Amani kutoka madhehebu mbalimbali ya kidini ulimwenguni, anayo nafasi kule kumaliza hii ‘stalemate’ ya sasa kule Visiwani. Uwezo wake katika kusimamia amani ni mkubwa sana. Tunasoma kutoka Injili ya Matayo sura ile ya 5 mtari ule wa 9 maneno “Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu” (Mat. 5:9). Kwa imani yangu mimi naona Mzee Lowassa anaweza kusuluhisha mkwamo huu wa kisiasa ulioko Zanzibar. 

Akifanya hili, Mungu hadanganyi, atamfanya Lowassa kuwa mwana wa Mungu. Nchi yetu itasonga mbele moja kwa moja. Basi, niombe wasomaji wangu waungane nami kusema amani na suluhu huko Visiwani inaweza kabisa kupatikana. Hatupaswi kuwa wakosa rajua, Watanzania tuwe na imani ya ‘optimism’ jamani. Wazanzibari wapokee ule usia wa Baba wa Taifa aliotoa Oktoba 1987. Pili wamsikilize Mzee Lowassa akiamua kwenda kuwapatanisha. 

Mpaka hapa nafikiri tumeweza kusoma kuwa mtu ni kiumbe hatari sana. Mtu ni likoko, muonekano wa kuelewa Wazanzibari ni mkubwa lakini basi miongoni mwao wamo bado watu hatari kweli makoko. Wakiacha hali hiyo watadumisha uelewano, wataweza kuunda Serikali nzuri ya Umoja wa Wazanzibari wote. 

Kuna methali isemayo, “Meno ya mbwa hayaumani” basi Wazanzibari kamwe hawashindwi kuelewana na hatimaye kukubaliana. Ni wamoja na wana wasomi wa kutosha, wanachokosa ni ule moyo wa ‘Kusameheana na Kusahau’ yaliyopita enzi za mababu zao. Je, hilo kweli linawashinda kuliona? Sidhani. 

Naomba sana Wazanzibari wamuenzi mkongwe, mwanamapinduzi aliyesalia hai, Brigadia Jenerali mstaafu Ramadhani Haji Faki, Waziri Kiongozi mstaafu wa enzi za Vita ya Uganda aliyepachikwa jina la utani “One Man One Bom”. Bado anaweza kutamka mawazo na maoni yake hata leo hii. Waasisi wengine wote naona wameshatangulia mbele ya haki kwa Muumba wetu. Yeye amebaki, basi Mungu ana mpango naye. Wamwendee kwa ushauri na mawazo ya kusameheana zaidi.

Kwanini kizazi cha Wazanzibari wa leo wasimwombe ushauri?

Wale walioniomba nitoe ushauri wangu natumaini makala hii itawapatia jawabu. 

 

<<TAMATI>>