Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesononeshwa na idadi ndogo ya wanafunzi wa kike, katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST).
Taasisi hiyo iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha, imejengwa na Serikali kutokana na fedha za mkopo kutoka Mifuko ya Hifadhi za Jamii ili kutoa Shahada ya Pili-Uzamili (Masters) na Shahada ya Tatu -Uzamivu (PhD) katika Sayansi na Teknolojia.
Pinda alitembelea taasisi hiyo wiki iliyopita na kuelezea kutoridhishwa kwake na takwimu zinazoonesha kuwa NM-AIST ina jumla ya wanafunzi 135 wanaosomea shahada za uzamili na uzamivu, kati ya hao, wanaume 105 na wanawake 30.
Uchache wa wanafunzi wanawake unaonekana pia kwenye kozi za masomo, ambapo baadhi zina mwanamke mmoja na nyingine hazina mwanamke kabisa.
“Akina mama wanahitaji kuvutwa zaidi katika kujiunga na masomo hapa. Lazima tuone ni namna gani tuna mbinu za kuwapa nafasi,” alisema Pinda.
Awali, Mwenyekiti wa Baraza la NM-AIST, Profesa David Mwakyusa, alimweleza Pinda kwamba kwa sasa wanaandaa andiko la kuomba wanawake wapewe upendeleo maalumu katika taasisi hiyo.
“Tunategemea bajeti ya Serikali kwa asilimia 100, bado ni wachanga. Lakini wenzetu UDSM wakati wanatembea sisi tunatakiwa kuanza kukimbia na ili tukimbie tunahitaji nyenzo,” alisema Profesa Mwakyusa.
Naye Makamu Mkuu wa taasisi hiyo, Professa Burton Mwamila, alimuomba Waziri Mkuu kusaidia upatikanaji wa fedha za ujenzi wa awamu ya pili. Profesa Mwamila alisema kukamilika kwa awamu ya pili, kutaiwezesha taasisi hiyo kuagiza watafiti kutoka sehemu mbalimbali duniani.
“Upanuzi wa awamu ya pili pia utatupa nafasi ya kuongeza majengo kwa ajili ya watafiti. Lakini pia ujenzi wa ofisi za kutosha, maabara na kumbi za mikutano,” aliongeza Profesa Burton.
Alibainisha kwamba hadi sasa taasisi hiyo imeweza kupokea dola za Marekani milioni 3.1 zitakazosaidia kugharimia masomo kwa baadhi ya wanafunzi.
Aliongeza kuwa Canada nayo imetoa msaada wa dola za Marekani milioni 2.5 kwa kusaidia utafiti wa mama na mtoto.
“Lakini pia tumepata dola za Marekani milioni 1.3 zitakazosaidia Kituo cha TEHAMA (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano),” aliongeza.