Imeelezwa kwamba tatizo la wanawake wasiojua haki zao za mirathi limepungua kwa asilimia 50 kufikia mwaka huu.
Haya yameelezwa na taasisi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na utoaji elimu, ufahamu, haki za watoto, wanawake na utunzaji wa mazingira Tanzania (TABCO).
Katika mazungumzo na JAMHURI jijini Mwanza hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa TABCO, Irene Kyamba, amesema mafanikio hayo yametokana na elimu inayotolewa na taasisi hiyo.
Kwamba kuanzia mwaka 2005, zaidi ya asilimia 85 ya wanawake katika Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza hawakuwa na uelewa wowote kuhusu haki zao za kupata mirathi, lakini sasa kundi hilo la jamii limeondokana na tatizo hilo.
Kyamba amesema matarajio ya taasisi hiyo ni kwamba kufikia mwishoni mwa mwaka huu na mwanzoni mwa mwaka kesho, tatizo hilo litakuwa limekwisha kabisa. “Elimu na harakati nzuri zinazofanywa na TABCO juu ya kumwokoa mwanamke dhidi ya kutofahamu haki za mirathi, vimefanikiwa,” amesema.
Mafanikio hayo yamechochea upatikanaji mkubwa wa elimu na maisha mazuri, baina ya watoto waliokuwa wakiishi katika mazingira magumu na hatarishi kutokana na mama zao kudhulumiwa haki hizo.
Kwa sababu hiyo, Kyamba ametumia nafasi hiyo kuikumbusha Serikali kuongeza uwajibikaji kwa jamii, ikiwa ni pamoja na kuondoa gharama za kuendeshea kesi za mirathi kwa wanawake wajane na walioachika katika ndoa.
“Ipo haja sasa kwa Serikali kuangalia uwezekano wa kuondoa gharama za kuendeshea kesi pale mwanamama anapopeleka malalamiko ya mirathi mahakamani, maana wanawake wengi wanashindwa kupata haki zao kutokana na ukubwa wa gharama za kesi,” amesisitiza Kayamba.