Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

WANAWAKE Viongozi wa Vyama vya siasa nchini wamelaani kauli zinazotolewa na baadhi ya watu kuwa Taifa halina amani ambapo wamesema zinania ovu ya kuhatarisha usalama wa nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 17, 2024 jijini Dar es Salaam kuelekea maadhimisho ya siku Amani ambayo kufanyika kila mwaka ifikapo Septemba 21, Katibu Mkuu wa chama cha United Democratic Party (UDP) Swaumu Rashid amesema kauli hizo zinaweza kuchangia kuongezeka kwa hofu na kusababisha migogoro zaidi hali ambayo inahatarisha usalama wa umma.

“Ni muhimu kutambua kwa kauli hizi zinaweza kuchochea vurugu na kueleza hofu au taarifa zisizo sahihi zinaweza kuathiri utulivu. Hebu tujiulize ikiwa Amiri Jeshi Mkuu wa Nchi ameagiza uchunguzi ufanyike kwa kutumia vyombo husika, lakini kuna kundi linaloshinikiza vurugu na machafuko, je uchunguzi huo unaweza kufanyika kwa ufanisi ?.

“Hali hii inaweza kuleta athari kubwa kwa taifa letum…mfano vurugu na machafuko yanayohamasishwa na baadhi ya makundi yanaweza kuvuruga juhudi za uchunguzi, kupoteza rasilimali na kuongeza hali ya wasiwasi katika jamii,” amesema.

Aidha amesema kundi hilo linaweza kuwa na malengo ya kisiasa au binafsi, kama vile kujiongezea umaarufu au kupinga uongozi uliopo.

“Vurugu hizi zina madhara makubwa kwa Uchumi wa Taifa zitasabisha upotevu wa rasilimali, uharibifu wa mali za raia na kuleta hali ya wasiwasi wa kiuchumi,” amesema Swaumu.

Naye Mwenyekiti wa Wanawake kutoka Chama Cha Tanzania Labour Party (TLP,) Nuru Kimwaga amewaasa wanawake kutokutumika vibaya katika kuivunja amani ya Nchi.

“Niwaombe wanawake wenzangu tukemee kwa pamoja vitendo hivi na tumuunge mkono Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kuijenga amani ya Nchi yetu,” amesema Nuru.

Kwa upande wake Mwakilishi wa watu wenye ulemavu, Amina Mafita amewaomba wanawake kutokukata tamaa na badala yake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

“Haya mambo yanayotokea yasitukatishe tamaa, tuendelee Kupambana na kuhakikisha tunashiriki katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi,” amesema Amina.

Please follow and like us:
Pin Share