Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
KUELEKEA Siku ya Wanawake Duniani wanawake kutoka Tume ya Madini wamefanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kulipia gharama za matibabu kwa wagonjwa wenye uhitaji maalum ikiwemo vifaa tiba, dawa, operesheni pamoja na kugawa baadhi ya vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuwatia moyo wagonjwa hao.
Meneja wa Utawala na Rasilimali Watu, Fatma Chondo amesema kuwa ziara hiyo ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika tarehe 08, Machi 2024 ambapo wameamua kuwatembelea wagonjwa wenye uhitaji, kuwapatia msaada na kuwatia moyo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi misaada mbalimbali jana hospitalini hapo amesema wanatambua kila mtu ana mahitaji mbalimbali hivyo kwa michango iliyotolewa na Tume ya Madini itafanikisha baadhi ya matibabu ikiwemo kulipia baadhi ya gharama kwa wagonjwa 13 ambao wamekuwa wakipatiwa matibabu lakini wamepata changamoto ya kulipia gharama.
“ Natoa wito kwa wanawake wengine kuwa sisi kama walezi tunategemewa na tuendelee kuwasaidia watanzania wenzetu wenye mahitaji zaidi lakini wanakosa msaada, ambapo kutoa ni akiba ya baadae pamoja na familia zetu, “amesema.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Tegemea Jassel ameshukuru wanawake wa Tume ya Madini kwa umoja huo na kusisitiza wanawake wengine kujitokeza ili kuondokana na matatizo yanayowakabili wagonjwa.
Naye Muuguzi Mfawidhi Msaidizi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Mariam Lyimo ameshukuru kwa jitihada zilizofanywa na wanawake na kusisitiza kuendelea kujitokeza katika kuwasaidia wenye mahitaji maalum na walioshindwa kupewa matibabu kama wanawake wa madini.
Mmoja kati ya wagonjwa walionufaika na msaada huo, Daudi Muna ameushukuru uongozi wa Tume hiyo na kueleza kuwa msaada huo ni muhimu kwa kuwa utasaidia kuleta unafuu wa gharama za matibabu.
“Mmefanya jambo zito sana,tunawaombea Mungu awaongoze zaidi katika kazi yenu,niwaombe pia wengine wanaojiweza kuwasaidia wenye uhitaji katika kukidhi gharama za matibabu, ” Amesema