Wakati fulani nilikuwa nikisikiliza wimbo ulioimbwa na mwanamuziki nguli, Luck Dube, na ukatokea kunivutia sana kutokana na maudhui yake.
Ndani ya kibao hicho, Dube anaeleza namna wanawake wanavyopambana na maisha kupitia kujituma kuhakikisha familia zao zinastawi vizuri. Hata hivyo, Dube anaulaumu ulimwengu kwa kutomtangaza mwanamke kama shujaa, lakini pia kutompa usaidizi unaotakiwa.
Katika ghani za shairi mojawapo, Dube anasema maneno yafuatayo: “…kila siku tunawasifu mashujaa, lakini wapo tunaowasahau; nao ni wanawake wa ulimwengu huu. Wanawajibika na kusimama imara katika majukumu yao. Mungu wabariki wanawake!”
Katika zama hizi za ujasiriamali, kwa hakika hatuwezi kumweka kando mwanamke kutokana na nafasi yake katika jamii. Hili linatokana na vuguvugu la ukombozi wa mwanamke linaloendelea duniani pote, ambapo mwanamke anahitaji kuwa huru katika nyanja zote zikiwamo za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Katika kuelekea ukombozi kamili wa kiuchumi, mazingira na hali zinamlazimisha mwanamke kuwajibika kikamilifu katika harakati za ujasiriamali.
Iwe mwanamke ameolewa ama hajaolewa, lazima kutambua kuwa ni vigumu kuwa huru katika maeneo mengine ikiwa hatakuwa huru kiuchumi. Na ifahamike kuwa uhuru wa mtu haushikwi na mwingine. Maana yake ni kuwa wanawake wasitarajie kuwa huru kiuchumi kama hawatajishughulisha kikamilifu, au kama watatarajia uhuru wao uwe mikononi mwa waume zao.
Na kwa wale ambao bado hawajaolewa (iwe ni wasomi ama wasio wasomi), nao wanatakiwa kuzichanga vyema karata zao na kuhakikisha wanakuwa na mipango madhubuti ya kujikomboa kiuchumi, ikibidi hata kabla hawajaingia katika ndoa. Kwa sababu huko kwenye ndoa ni wanaume wachache wanaoruhusu wake zao kufanya ujasiriamali!
Mara zote nimekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wanawake kutopuuza nafasi yao ya utii kwa waume zao, kwa namna na katika mazingira yoyote yale. Pamoja na hilo, mwanamke kamwe hatakiwi kufyata mkia na kuruhusu ndoto zake kufutwa na kile kiitwacho ‘ndoa’.
Kama mwanamke ana ndoto ya kujiendeleza kimasomo, kuwa mjasiriamali, ama kupata mafanikio mengine yoyote, hana budi kushikilia na kushughulikia ndoto yake hadi aone ikitokea bila kukwama kutokana na vikwazo vya mazingira ya ndoa, ama mume wake.
Ninapoongelea ujasiriamali kwa wanawake ninafahamu kutakuwa na ukinzani mkubwa kama sitatengenisha wanawake kwa makundi. Kwa uthubutu, kundi la kwanza ninawaweka wanawake ambao hawajaolewa na la pili ninaweka kundi la wanawake walioolewa.
Ninasukumwa kufanya hivi kwa sababu ninafahamu kuwa kundi la wanawake walioolewa uamuzi wao unafungwa na matakwa ya waume zao, wakati kundi la wanawake ambao hawajaolewa lenyewe lipo huru zaidi.
Nimesema wanawake wenye ndoa uamuzi wao unadhibitiwa sana na wanaume, kwa kuwa kuna wanaume ambao wanawaunga mkono wake zao kufanya ujasiriamali, lakini wapo wanaume ambao hawako tayari kuruhusu wake zao kujishughulisha na ujasiriamali. Kwa hawa, mbali na changamoto nyingi za kijasiriamali, pia wanakumbana na dubwasha jingine, liitwalo ‘kunyanyaswa na waume zao’.
Kiukweli asilimia kubwa ya wanaume wengi wana matatizo katika fikra zao, kutokana na namna wanavyouchukulia uwezo wa wanawake katika ujasiriamali. Wengi wanaona mwanamke kuwa mjasiriamali, atakuwa na kiburi, wanahisi atachukua nafasi yao katika familia, na kubwa linalowaogopesha ni kudhani kuwa mwanamke mjasiriamali ni mhuni.
Ujinga wa baadhi ya wanaume ni kudhani kuwa hulka hasi wanazokuwa nazo wao katika ujasiriamali, zipo pia kwa wanawake wajasiriamali. Upo ukweli kuwa baadhi ya wanaume wanapofanikiwa kiujasiriamali (na hata katika maeneo mengine) huwa na mtindo wa kuanza kiburi kwa wake zao, kusaliti ndoa zao na kusahau michango ya wake zao kwa hatua wanayokuwa wamefikia. Kutokana na hili, wanaume ni kama wanaogopa vivuli vyao wenyewe, katika kuwapa uhuru wake zao kujishughulisha kikamilifu na ujasiriamali.
Dhana hii imesababisha wanaume wengi kuwanyanyasa wake zao wanaojishughulisha na ujasiriamali na hata kuwakatisha tamaa. Na hili linatokea sana pale ambapo, ama mwanaume si mjasiriamali, au ikiwa wote ni wajasiriamali lakini wanafanya biashara tofauti. Inamhitaji mwanamke kujifunga kibwebwe ili kuendelea mbele.
Mara nyingi inapofika hapo (manyanyaso kuzidi) wanawake wengi husalimu amri na kuuacha ujasiriamali. Ni wachache wanaoamua kujitoa katika ndoa na kujikita katika ujasiriamali. Ndiyo maana takwimu na uzoefu vinaonesha kuwa idadi kubwa ya wanawake waliofanikiwa kiujasiriamali ama hawakuolewa kabisa, au walitalikiana na waume zao, ama wanavumilia kuishi katika ndoa zenye migogoro mikubwa.
Kwa wale wanaume waliooa na wanafanya ujasiriamali pamoja na wake zao, nao bado wameendelea kuwa wagumu katika kuwashirikisha wake zao kikamilifu. Kama ni duka, mwanamke anabaki kuwa muuzaji tu, hajui ni wapi mali zinakonunuliwa, hajui mfumo kamili wa mapato na matumizi, hajui hata mipango na mikakati ya biashara.
Wapo wanaume ambao huwa wanadiriki hata kuchukua mikopo katika benki kwa kutumia rasilimali za familia bila kuwashirikisha wake zao. Hili ni tatizo kubwa! Ndiyo maana idadi kubwa ya wajane wa wajasiriamali huwa hawafiki mbali kibiashara mara baada ya waume zao kufariki.
Kwa wale wanaoendesha biashara katika mifumo rasmi, (kwa mfano kampuni), ni vema, tena ni njia rahisi kutoa kiwango unachodhani kinafaa cha ushiriki wa mke wako katika biashara zako. Kwa mfano, mke anaweza kuwa na asilimia fulani ya hisa katika kampuni. Hili litamwezesha kuingia katika vikao vya bodi ya wakurugenzi na kushiriki katika mipango na maendeleo ya kampuni, hata kama anaendelea na kazi yake nyingine.
Siku zote ninasukumwa kuamini kuwa suala la ukombozi wa mwanamke linahitaji sana kuhusisha ukombozi wa fikra za mwanaume, aweze (mwanaume) kuachia haki na uhuru wa mwanamke alioushikilia kwa karne nenda rudi kupitia mfumo dume.
Hata hivyo, naomba niweke sawa msimamo wangu katika hili kuwa sikubaliani na “baadhi ya wanaharakati” wanaotaka mwanamke abebe majukumu ya mwanaume. Tumkomboe mwanamke lakini tusithubutu kubadilisha uumbaji wa Mungu.
Ipo haja ya kuwekana sawa katika hili kwa sababu si busara kuona wanawake ‘wakizikacha’ ndoa ama wakikataa kuingia katika ndoa, kwa sababu ya ujasiriamali. Ujasiriamali haupaswi kuwa kiwanda cha talaka, haupaswi kutengeneza waseja (wanawake wasiotaka kuolewa) na katu hautakiwi kuwa kapu linalotunza migogoro ya ndoa.
Lakini tunapoongelea ujasiriamali kwa wanawake lazima wao (wanawake) na jamii kwa ujumla, waachane na kasumba ya kuwa na mitizamo hafifu. Kuna fikra zimemea za kudhani kuwa wanawake wanatakiwa kufanya biashara ndogo ndogo, kama kuuza maandazi, mboga, kushona vitambaa na vibiashara vingine uchwara.
Hayumkini hili ni tatizo lililopo hata katika fikra na mipango ya taasisi mbalimbali za fedha zinazotoa mikopo midogo midogo kwa wanawake. Taasisi hizi zimejizoesha kukopesha ‘vimikopo’ vya shilingi elfu hamsini, laki moja, ikizidi sana shilingi laki tano! Ni vigumu wanawake kupiga hatua kiujasiriamali kama hawataaminiwa na kupewa mikopo zaidi ya hapo (mikubwa). Tukitaka mabadiliko hatuna budi kuwaamini wanawake.
Wanawake wenyewe wanatakiwa kuachana na mawazo ya kujikunyata na unyonge, bali waanze kufikiria kiupana (thinking in big picture). Ni wasaa wa wanawake kuibuka na mawazo makubwa ya kibiashara, kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa, kuanzisha kampuni, kucheza na fursa za biashara za kitaifa na kimataifa.
Wanawake sasa wawatazame wanawake wenzao wachache waliofanikiwa kiujasiriamali duniani na katika mazingira ya Tanzania, halafu wainuke na kuanza kutenda. Hakuna maana ya kuwa na visingizio, kukata tamaa na kudhani kuwa mwanaume ana asilimia 100 za uhuru wa mwanamke kiuchumi.
Kama si kusimama peke yake kiujasiriamali basi mwanamke anatakiwa kushikana bega kwa bega na mume wake, ili thamani na mafanikio ya familia kupitia ujasiriamali yawe ni mchango wa nguvu, bidii na maarifa ya wanandoa wote kwa pamoja.
Faida iliyopo kwa wanawake ni kuwa wana hulka za uvumilivu na kujituma ambazo ni muhimu sana katika ujasiriamali. Kwa ‘added advantage’ hii kwa nini wanawake wabaki nyuma?
Haina ubishi kuwa wanawake wapo katika kipindi cha mpito katika kutokomeza mfumo wa kutoaminiwa. Kipindi hiki ni kigumu na kinahitaji kukilipia gharama ili kupata mafanikio likiwamo eneo hili la ujasiriamali. Ni kipindi cha mapambano, kutoka utumwa wa mwanamke kuwa ‘mama wa nyumbani’, ‘golikipa’, ‘tegemezi’ na ‘wa kuamuriwa hata kama ana kazi yake’ kuelekea katika uhuru wa kiuchumi.
Wanawake wasione taabu kukataliwa na jamii zao, wasirudi nyuma kwa kuachwa ama kunyanyaswa na waume zao, na wavumilie kutukanwa na kusemwa vibaya na wanajamii wanaowaona wanawake wanaouendea mstari wa mafanikio kupitia ujasiriamali, kana kwamba ni wahuni.
Lazima wanawake wajitahidi kushinda changamoto za kuhudumia familia, kukabiliana na vishawishi, kubaki wasafi kinidhamu, kimaadili na katika imani. Kwa kufanya hivyo, jamii itaendelea kushuhudia na kuyaheshimu mafanikio ya wanawake katika ujasiriamali nchini Tanzania na duniani kwa ujumla.
Wanawake wajasiriamali wanastahili ushindi.