Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Monduli
Wanawake wa Jamii ya kifugaji ya kimasai wilayani Monduli mkoa Arusha,wametajwa kuwa waathirika wakubwa ya mabadiliko ya tabia nchi, hali ambayo imefanya maisha yao kuwa duni huku wakieleza adha ya waume zao kuhama majumbani kwenda kusaka malisho na maji muda mrefu.
Akiwasilisha utafiti juu ya hali ya mabadiliko ya tabia nchi, athari zake na fursa wilayani Monduli,Mkurugenzi wa Taasisi ya Kesho Trust ,Peter Lubambula katika warsha iliyoandaliwa na Shirika la utafiti maendeleo na huduma kwa jamii [CORDS] ya
uwezeshaji,uongozi,ustahimilivu kwa ushirikiano kwa maendeleo ya watu wa asili, alisema zinahitaika jitihada za wadau kusaidia uendelevu wa maisha ya jamii za asili.

Lubambula alisema katika utafiti ambao umefanyika mwaka jana katika vijiji 7 kati ya 11 vilivyopo katika mradi wa uwezeshaji wananchi unaotekelezwa na shirika la CORDS, kwa ufadhili wa serikali ya Ujerumani kupitia shirika la Karl Kubel Stiftung alisema,wamebaini wanawake ndio waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabia nchi.
Alisema wanawake wanakabiliwa na shida ya maji kupatikana umbali mrefu,kuwa na upungufu wa chakula lakini pia kuendelea kupungua maeneo ya nyanda za malisho,kuendelea kusambaa mimea vamizi na kuharibika miondombinu mingi.
Lubambula alisema ili kukabiliana na baadhi ya changamoto hizo,ni muhimu kuendelezwa jitihada za kusaidiwa jamii hiyo kama ambavyo inafanywa CORDS kuwezesha wanawake kujikwamua na umasikini kwa kuwapa mikopo, kuanzisha vikundi vya ujasiriamali na kutoa elimu ya haki zao.
Hata hivyo, alisema umefika wakati jamii ya kifugaji kupewa elimu zaidi ya kupunguza mifugo ya asili ili kupunguza hasara ya mifugo kuendelea kufa kwa kukosa malisho na maji, lakini pia kuwezeshwa kuandaa mashamba ya majani kwa ajili ya malisho.

Meneja mradi huo wa CORDS wa kuwezesha wanawake, Ng’inai Lepilal Molloiment alisema mradi huo unalenga kuwawezesha wanawake kiuchumi kukabiliana na umasikini,kukabiliana na ukatili wa kijinsia ikiwepo Ukeketaji.
“hadi sasa tumewezesha kuanzishwa vikundi 11 vya akina mama vyenye watu 330, wanawake 150 mmoja wamepata mikopo kuboresha maisha yao”alisema.
Ngoijie Lemalali mkazi wa kijiji cha Engorika kata ya Naararami na Elizabeth Ngonina mkazi wa kijiji cha Elerendeni kata ya Engaruka, walisema mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa na madhara makubwa kwao.
Lemalali alisema mabadiliko ya tabia ya nchi yamesababisha wanyamapori hasa tembo kuhamia katika makazi yao na sasa Zaidi ya miaka 10 wameshindwa kulima na Tembo wanaingia hadi ndani ya makazi kutafuta maji.

“Tunashukuru CORDS kutupa mikopo ya kununua mbuzi na kuanza kunenepesha na kukopeshana walau inapunguza ukali wa maisha lakini tunaomba mikopo Zaidi kwani kila kitu ni cha kununua”alisema.
Ngonina alisema mabadiliko ya tabia nchi yameongeza umasikini kwani wanaume wengi wamekuwa wakihama muda mrefu kwenda na mifugo kusaka malisho.
Meneja miradi wa CORDS,Rogath Massay alisema shirika hilo katika mradi huo wa miaka mitatu linatarajia kuwanufaisha watu zaidi 2000 katika wilayani Monduli.
Awali mwezeshaji wa warsha hiyo Dk Miriam Zakaria alisema washiriki wanatarajiwa kubadilisha uzoefu juu ya masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia miradi mbali mbali.
Afisa maendeleo wa halmashauri ya Monduli Fauzia Omar alipongeza shirika la CORDS kuwa na mradi huo katika wlaya ya Monduli kwani inakabiliwa na changamoto nyuingi za mabadiliko ya tabia nchi.
Alisema wilaya hiyo imekuwa na ukame wa muda mrefu ,wanyama wengi wamekua lakini pia kumekuwa na mafuriko katika maeneo kadhaa ikiwepo mi wa Mto mbu.



