Karibu wanawake 200 wenye miaka 18-22 kutoka barani Afrika, wamekuwa wakisajiliwa kwenda kufanya kazi Urusi, katika kiwanda kinachohusika kuunda maelfu ya droni za Iran zinazotumika kuishambulia Ukraine.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti maalumu iliyotolewa na shirika la habari la Associated Press baada ya kukamilisha uchunguzi wake.

Wanawake hao kutoka barani Afrika wamekuwa wakifanya kazi kwenye kiwanda cha droni sambamba na wanafunzi wa vyuo vya ufundi wa Urusi.

Katika mahojiano ya shirika la habari la AP baadhi ya wanawake wamesema walilaghaiwa kuwa wangekwenda Urusi katika programu ya kufanya kazi na kusoma. Badala yake wameeleza kwamba wamekuwa wakifanya kazi kwa muda mrefu huku wakifuatiliwa muda wote.

Wamekutana na ahadi hewa kuhusu kiasi cha mishahara na programu za mafunzo huku wakifanya kazi zinazohusisha kemikali ambazo zimewasababishia athari katika ngozi zao.

Kulingana na shirika la habari la The Associated Press, lilifanya uchambuzi wa picha za satelaiti za jengo lililo katika eneo la Urusi linalofahamika kama Jamhuri ya Tatarstan sambamba na nyaraka za ndani zilizovuja. Pia lilipata mamia ya video zilizo katika programu ya usajili ya mtandaoni na kufanikiwa kufahamu maisha katika kiwanda kilicho katika kile kinachoitwa Kanda maalumu ya Uchumi ya Alabuga, kilometa 1,000 mashariki mwa Moscow.