Na Suzy Butondo, JamhuriMedia, Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme amewataka wanaume kuacha kuwaowa wanafunzi wa kike badala yake wawaache wasome na wavae magauni mawili ambayo ni sare za shule na joho la kuhitimu masomo .
Pia wazazi na walezi amewataka waache kuwafanya vitega uchumi watoto wa kike na tamaa ya kutaka mali kwa kuwaozesha wanafunzi wa kike atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria hivyo wawaache watoto waendelee na masomo ili kutimiza ndoto zao.
Hayo ameyasema leo Januari 10,2024 wakati akikagua wanafunzi wa shule ya awali na msingi katika shule ya msingi Mwenge, Ngokolo sekondari na Butengwa shule ya sekondari ya wasichana iliyoko manispaa ya Shinyanga Mkoani hapa, ambapo amewataka wazazazi wote kuacha tamaa ya kupokea mahali.
Mndeme amesema baadhi ya wazazi wanaingiwa na tamaa ya kupokea mahali mapema hata kabla hajamaliza shule mtoto wa kike, hivyo amewaonya wazazi hao kuacha tabia hiyo mara moja badala yake wasubiri watoto hao wavae mavazi mawili sare ya shule na joho la kuhitimu masomo.
“Nimeyasema haya kwa masikiitliko makubwa baada ya mzazi mmoja wa kijiji cha Iyugi kata ya Lyamidati halmashauri ya Shinyanga ambaye amemuozesha mtoto aliyefaulu kwa ufaulu mzuri wa A baada ya kupokea mahali ya ng”ombe 15 , nimshukuru mwenyekiti wa kijiji na mkuu wa wilaya kwa kuhakikisha mtoto ameondolewa kwenye ndoa hiyo”amesema Mndeme.
“Mtoto tumemuokoa kwakumuondoa kwenye ndoa hiyo na mzazi amekimbia tunamsaka ili tumchukulie hatua kali za kisheria ili liwe fundisho kwa wazazi wengine nasisitiza kwamba wanaume acheni kuwaowa wanafunzi subirini wavae magauni mawili ya sare za shule na joho ndio muwaowe”ameongeza Mndeme .
Aliwaomba wazazi wasiwatumie watoto kupata utajili kwa kumuozesha mtoto wa kike kabla hajamaliza masomo yake suala la kuwaozesha watoto na kuwafanya kitega uchumi halikubariki,.
Pia amewaomba walimu kuendelea kufundisha kwa bidii ili wanafunzi wapate kuelewa masomo na kufanya vizuri kwenye mitihani yao, kwani Shinyanga inahitaji wasomi waweze kuongezeka zaidi.
Kwa upande wake afisa elimu wa mkoa wa Shinyanga Dafroza Ndalichako amesema matarajio ya uandikishaji kwa darasa la kwanza na elimu ya awali yametokana na sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2022 awali walikuwa ni 75,079 na mpaka sasa wameandikisha wanafunzi 47,147 sawa na asilimia 62.
Kwa darasa la kwanza kwa mujibu wa sensa ni wanafunzi 69,792 lakini mpaka sasa wameandikisha wanafunzi 44,432 sawa na asilimia 64, katika kidato cha kwanza wanafunzi 38,963 wamefauli, hivyo wanatategemea kupokea taarifa mbalimbali kutoka maeneo mbalimbali ya shule katika mkoa wa Shinyanga ambapo katika shule ya Ngokolo sekondari iliyoko manispaa ya Shinyanga tayari wanafunzi 79 wameripoti shuleni.