Wanaume watakatifu wa Kihindu waliopakwa majivu waliingia kwenye mto mtakatifu zaidi wa India wa Ganges alfajiri ya siku ya kwanza ambayo ni muhimu katika ibada ya kuoga ya sikukuu ya Kumbh Mela kwenye Jiji la (askazini la Prayagraj.

Waumi hao waliimba nyimbo zao za kidini, wakiita miungu ya Kihindu walipokuwa wakitumbukia ndani ya maji yenye barafu.

Baada ya kutoka majini, wengine waliokota mchanga wa rangi ya fedha mkononi na kuupaka mwilini mwao.

Pia kuna waliobeba panga na mkuki wenye ncha tatu huku mkono mwingine ukishikilia juu fimbo ya fedha yenye kichwa cha nyoka.

Kando ya watu hawa watakatifu – wanaojulikana kama Naga sadhus – mamilioni ya mahujaji wa Kihindu kutoka kote ulimwenguni wako Prayagraj kushiriki katika tamasha ambalo linaweza kuonekana kutoka angani na linadaiwa kuwa mkusanyiko mkubwa zaidi wa wanadamu.

Wahindu wanaamini kwamba tambiko la kuoga mtoni litawatakasa dhambi, nafsi zao na kuwasaidia kupata uwokovu kwa kuwakomboa kutoka katika mzunguko wa kuzaliwa na kifo.