Wanaume wengi wanapitia matatizo mbalimbali yanayohusiana na ukosefu wa nguvu za kiume katika kipindi tofauti, hasa wanapofikia umri wa utu uzima unaokaribiana na uzee, hata hivyo matatizo haya mara nyingi husababishwa na magonjwa mengine.
Ukosefu wa nguvu za kiume ni hali inayompata mwanaume wakati ambapo uume haupokei damu ya kutosha ili mishipa iliyopo ndani ya uume iusaidie uume kusimama kama inavyotakiwa na kuleta uwezo wa kushiriki tendo la ndoa.
Kwa mwanaume mwenye tatizo la nguvu za kiume, hii humtokea mara nyingi na kuathiri uwezo wa kushiriki tendo la ndoa kikamilifu.
Wahanga wakubwa wa tatizo hili ni wale wanaume wenye umri unaokaribia uzee kwa sababu kisayansi, kadri umri unavyosogea, na mishipa midogo midogo ya damu iliyopo mwilini inaanza kulegea na kupoteza uwezo stahiki wa kusambaza damu kwenye sehemu mbalimbali za mwili, lakini ukosefu wa nguvu za kiume ni tatizo linalowakumba vijana kwa kasi sana.
Si rahisi kwa kijana yeyote kukubaliana na ukweli kuwa ni mwathirika wa tatizo hili pale inapogundulika kwake kutokana na ile dhana kuwa kukosa nguvu za kiume kwa kijana ni aibu kubwa! Na hasa ikiwa bado kijana husika ana umri mdogo ulio chini ya miaka 45.
Sababu zinazochangia
Wakati mwingine tatizo hili linaweza kuchangiwa na matatizo ya kisaikolojia, matatizo ya kiafya yanayoshambulia mfumo wa fahamu lakini pia hata mtindo wa maisha ya mtu husika.
Wanaume wanapopata dalili za kukosa nguvu za kiume ni vyema wakamuona daktari haraka ili kuainisha chanzo cha tatizo na kupatiwa tiba stahiki. Baadhi ya sababu za ukosefu wa nguvu za kiume kwa vijana ni kama vile:
• Magonjwa ya akili kama vile sonona (depression) ambayo yanachangia kupoteza hisia kwa vile vitu ambavyo awali vilikuwa vinakupa furaha.
• Magonjwa yanayoshambulia via vya uzazi mathalani magonjwa ya zinaa kama vile kisonono (gonorrhea), kaswende na mengineyo.
• Magonjwa ya kisukari ambayo yanaathiri kwa kiasi kikubwa sana usambazwaji wa damu sehemu mbalimbali mwilini hasa kwenye uume.
• ‘Hypogonadisim’. Hili ni tatizo la kiafya ambapo mwili unashindwa kuzalisha homoni zinazoleta hisia za kutosha.
• Baadhi ya utumiaji wa dawa mathalani dawa zinazotumika kutibu magonjwa mbalimbali ya akili (anti-depressants) yanachangia kwa kiasi kikubwa sana tatizo hili.
Lakini, hata hivyo, baadhi ya vijana wanapata matatizo ya ukosefu wa nguvu za kiume kutokana na sababu ambazo zipo chini ya uwezo wao na wangeweza kuzimudu. Kwa mfano, vijana wanaweza kupata tatizo hili kutokana na:
• Uzito uliopita kiasi
• Kisukari, mathalani, aina ya pili ya kisukari ambayo inasababishwa na mtindo wa maisha ya mtu husika.
• Ulaji wa mlo usio kamili, aidha kupendelea kula vyakula vilivyosindikwa kiwandani badala ya kupendelea kula vyakula vya asili.
• Kutofanya mazoezi ya mwili
• Uvutaji wa sigara
• Unywaji wa pombe kupita kiasi
• Msongo wa mawazo unaotokana na mahusiano na matatizo mengine yanayopoteza furaha kwa mtu.
Ikiwa tatizo la nguvu za kiume limetokana na moja ya sababu hizi, inawezekana kwa kijana kupunguza au kumaliza kabisa tatizo kwa kubadili mtindo wa maisha na vyakula. Hata hivyo, hata kama kijana anadhani anazijua sababu za tatizo, bado anashauriwa kumuona daktari kwa ajili ya vipimo.
Kijana anaweza kuziona dalili kadhaa kama vile uume kupoteza uwezo wa kusimama, lakini hata ukisimama, unashindwa kudumu kwa muda mrefu na hatimaye unasinyaa ndani ya muda mfupi na kushindwa kushiriki kikamilifu tendo la ndoa. Dalili hizi moja kwa moja zinasababisha kupoteza hamu ya kufanya tendo la ndoa na kwa dalili hizi, ni dhahiri kijana anakuwa tayari ni muhanga wa ukosefu wa nguvu za kiume.
Chukua hatua
Kwanza unahitaji msaada wa kisaikolojia na kutia moyo kuwa tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume ni la muda tu na litatoweka iwapo utachukua hatu na kukabiliana nalo. Vijana wapo kwenye nafasi nzuri ya kurudi kwenye uwezo wa nguvu za kawaida kama ilivyo mwanzo kuliko wazee.
Hii inawezekana endapo kijana husika atadhamiria kubadili mtindo wa maisha ambao kwa kawaida unasaidia kuboresha afya kwa ujumla na kwa kupata tiba stahiki. Ni kawaida na ni rahisi kwa kijana kupata nguvu za kiume kama mwanzo kwa kufuata utaratibu wa tiba na kufuata ushauri wa daktari pia.
Na Chris Peterson
Barua pepe: [email protected]
Simu: 0755-060 788