Kikosi Kazi maalumu kilichoundwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kimebaini ukwepaji kodi unaokisiwa kufikia Sh bilioni 10 katika kampuni sita za bilionea Mmarekani, Friedkin, zinazojihusisha na sekta ya utalii nchini, JAMHURI linathibitisha.

Kwa tuhuma hizo, wakurugenzi wa kampuni hiyo wanakabiliwa na uwezekano wa kufunguliwa mashitaka ya uhujumu uchumi, ingawa hawajakamatwa kama serikali inavyofanya kwa wakwepa kodi wengine.

Wakati Kikosi Kazi kikitaja kiwango hicho, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa kiwango cha kodi kilichokwepwa kwa miaka 30 ya kampuni hizo hapa nchini ni zaidi ya mara tano ya hicho.

Kwa miaka yote hiyo, wafanyakazi wataalamu kutoka nje walioajiriwa na kampuni za Friedkin wamekuwa wakilipwa sehemu kubwa ya mishahara yao kwenye benki zilizo ughaibuni kama njia ya kuficha ukweli na kuinyima serikali mapato ya mamilioni ya fedha.

Sehemu zinazotajwa kupelekwa fedha hizo ni Visiwa vya Bahamas kwenye taasisi za fedha za Adventure Services na AHIL Trust. Hayo yakiendelea, uchunguzi umeanza kwenye akaunti za Friedkin zilizoko Uswisi na Visiwa vya Cayman.

Wanaotajwa kuwa wanahusika kuidhinisha fedha kutoka ofisi kuu za Friedkin zilizoko Houston – Texas, Marekani ni Rais wa kampuni za Friedkin, Dan Friedkin; Mtendaji Mkuu, Marcus Watts; na Mwanasheria Mkuu, Kimberly Jacobson.

Tayari mamlaka za dola zimezuia hati za kusafiria za wakurugenzi sita wa kampuni hizo, lakini taarifa zilizopatikana mwishoni mwa wiki zinasema wakurugenzi hao wanahaha kwa viongozi wakuu wa serikali ili warejeshewe hati hizo.

Kampuni za Friedkin zimejikita zaidi kwenye utalii wa picha na uwindaji wa kitalii. Kampuni hizo ni Tanzania Game Tracker Safaris Ltd (uwindaji wa kitalii), Wengert Windrose Safaris (Tanzania) Ltd (uwindaji wa kitalii), Ker & Downey Safaris (Tanzania) Ltd (utalii wa picha), Northern Air Ltd (usafiri wa anga), Mwiba Holding Ltd (ranchi ya wanyamapori na utalii) na The Friedkin Conservation Fund (masuala ya uhifadhi na maendeleo ya jamii).

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa Oktoba 25, mwaka huu Kikosi Kazi hicho kilikutana na wawakilishi wa kampuni za Friedkin jijini Arusha. Kwa upande wa Friedkin, waliohudhuria ni Jean-Claude Mcmanaman, Lemmy Bartholomew, Wilfred Mawalla, Elibariki Lucas, Nick Stubbs, Russel Hastings na Alex Rechsteiner.

Taarifa kutoka kwenye kikao hicho zinasema kampuni za Friedkin zinatuhumiwa kwa makosa ya ukwepaji kodi kupitia malipo ya wakurugenzi; na ukwepaji kodi kwenye mikopo na uhamishaji fedha ndani ya kampuni.

Makosa mengine ni kuajiri wataalamu kutoka nje ya nchi wanaofanya kazi kama washauri, lakini wakiwa hawana vibali wala sifa za kitaaluma; na imebainishwa kuwa baadhi ya wafanyakazi –wamekutwa wakiwa na mishahara zaidi ya mmoja na kwa viwango tofauti, pia hakuna makato kwa ajili ya mifuko ya hifadhi ya jamii.

Jingine ni mikataba mingi kwa wataalamu kutoka nje ya nchi, hasa kwa Jean-Claude ambaye amekutwa akiwa na barua ya ajira, lakini ana mkataba mwingine kama mshauri.

Kwenye kikao hicho, Friedkin waliomba wapewe hati zao za kusafiria kwa kile walichodai kuwa baadhi yao wana masuala ya kifamilia huko kwao na wengine wanakwenda katika matibabu na masuala ya kibiashara.

Kiongozi wa Kikosi Kazi aligoma kutoa hati hizo kwa maelezo kuwa hilo litawezekana tu endapo watuhumiwa hao watakuwa tayari kuweka kiasi cha fedha kama dhamana.

Friedkin wakawa wako tayari kutoa Sh milioni 100 na baadaye Sh milioni 200 lakini Kikosi Kazi kikagoma kukubali ofa hiyo. Badala yake, wakaelezwa kuwa watapewa hati zao za kusafiria endapo wataweka dhamana ya Sh bilioni 5 kwenye akaunti maalumu ya serikali wakati majadiliano kuhusu kiwango halisi cha kodi kilichokwepwa kikikokotolewa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Friedkin Group Company Ker and Downey Tanzania Ltd., Jean – Claude McManaman, anatajwa kukiri baadhi ya tuhuma za ukwepaji kodi.

 “Amekiri mengi tu, na taratibu za kuweka bondi ya Sh bilioni 5 zinaendelea. Kiwango hicho ni dhamana. Wanatarajia baada ya uchunguzi kiwango huenda kikawa kikubwa zaidi ya Sh bilioni 10 kwa sababu wanapitia taarifa za siri za kampuni zao kwenye benki za nje,” kimesema chanzo chetu kilicho karibu na Kikosi Kazi. 

Baadhi ya wakurugenzi walipeleka ujumbe mjini Dodoma kuonana na waziri mkuu ili kumuomba kiasi walichopendekeza kipokewe kama dhamana wakati taratibu nyingine zikiendelea.

Kwenye majadiliano hayo, Friedkin walitaka mwezao, Alex Rechsteiner, aondolewe kwenye orodha ya wakurugenzi walionyang’anywa hati za kusafiria kwa maelezo kwamba yeye si mkurugenzi, bali ni meneja.

“Walisema Alex ni meneja, kwa hiyo arejeshewe hati yake ya kusafiria, hilo likaonekana kama mbinu ya kumnyofoa kwenye sakata hili la ukwepaji kodi. Kikosi Kazi kiligoma,” kimesema chanzo cha habari.

Friedkin Group wanamtumia Mwanasheria Lemmy Bartholomew wa Kampuni ya Mawalla Advocates ya jijini Arusha.

Wakati wataalamu na wakurugenzi wa Friedkin wakizuiwa kusafiri nje ya nchi, ‘mshauri’ mkuu wa Friedkin Group, Fabia Bausch, kutoka Chem Chem Safaris, naye anatafutwa.

Kwa wiki nzima JAMHURI limewatafuta bila mafanikio viongozi wa Friedkin wazungumzie sakata linalowakabili. Mmoja wa viongozi wa muda mrefu kwenye kampuni hizo, Abdulkadir Lutta Mohammed, alipotafutwa alipatikana, lakini akakataa kuzungumza kwa maelezo kwamba yeye si msemaji rasmi wa kampuni za Friedkin.

Badala yake alitaka mwandishi awasiliane na Msemaji ambaye ni Jean, lakini mara zote alipotafutwa hakupokea simu. Novemba 8, mwaka huu, JAMHURI lilimtafuta Jean-Claude kupitia mtandao wa WhatsApp. Licha ya ujumbe kuonyesha kuwa umefika na umesomwa, hata hivyo hakujibu. Alipopigiwa simu tena hakupokea.

JAMHURI liliwasiliana kwa mara nyingine na Mohammed kumweleza kuwa Jean-Claude hajatoa ushirikiano. Majibu yake yalikuwa: “Hii kampuni ni kubwa na ina utaratibu wake, ninachoweza kukuhakikishia ni kuwa nimeambiwa umepeleka ujumbe ukitaka maelezo ya kinachoendelea. Kwa hiyo ujumbe wako umefika. Subiri utapigiwa na kupewa majibu, maana tayari ujumbe wako umefika.” Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni hakuna majibu yoyote yaliyopatikana kutoka kwa Jean-Claude.

Kwa wiki nzima wakurugenzi hao wamekuwa wakihaha ili warejeshewe hati za kusafiria, lakini Kikosi Kazi kimekuwa kikigoma kufanya hivyo.

“Tuhuma za ukwepaji kodi zinazowakabili ni nyingi na kubwa. Ukiwarejeshea hati za kusafiria maana yake unasema hili suala limekwisha. Imani yetu ni kuwa kiasi cha kodi kilichokwepwa ni kikubwa kuliko hiki tulichokiona, kwa hiyo kuwaruhusu waondoke nchini maana yake ni kuharibu kazi yote iliyokwisha kufanyika,” kimesema chanzo chetu.

Wakati wakurugenzi wa Friedkin wakiwa huru licha ya kukabiliwa na tuhuma za ufisadi na uhujumu uchumi, wengine wenye tuhuma kama hizo wako rumande. Miongoni mwao ni Mkurugenzi wa Kampuni ya uwindaji wa kitalii ya OBC, Isaack Mollel, aliyeko rumande tangu Februari, mwaka huu.

Licha ya ombi la Rais John Magufuli ambalo lilikubaliwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) la kuingia makubaliano na washitakiwa ili waombe radhi, walipe fedha na waachiwe, Mollel na washitakiwa wengine wamefanya hivyo, lakini hadi sasa bado wako rumande.

Usuli

Kampuni za Friedkin zimekuwa kwenye migogoro mbalimbali na kampuni nyingine za uwindaji wa kitalii. Kumekuwapo tuhuma za kampuni hiyo kulindwa na baadhi ya viongozi wakuu katika Wizara ya Maliasili na Utalii.

Ugomvi wa vitalu vya uwindaji umetawala taarifa za uhusiano wa kampuni za Friedkin na kampuni nyingine za uwindaji wa kitalii. Tukio la karibuni ni la Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, kutangaza kuifutia leseni Kampuni ya Green Mile Safaris (GMS) inayomilikiwa na raia wa Tanzania. Kumekuwapo taarifa za wazi kuwa GMS inapokwa kitalu hicho ili wapewe Friedkin kwa madai kwamba kilikuwa chao.

Taarifa za ndani zinasema viongozi wa Friedkin wamo kwenye mvutano na baadhi ya viongozi waandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kile kinachodaiwa kwamba ni kushindwa kwao kuwapa kitalu kinachomilikiwa na GMS kama walivyokuwa wamewaahidi.

Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ni miongoni mwa wanaotajwa kuwa ni marafiki wakuu wa Friedkin. Mwaka 2015 akiwa na wadhifa huo, alitumia helikopta za Friedkin kwa shughuli binafsi zikiwamo kampeni zake za ubunge.

Nyalandu alihakikisha wanapata Hadhi ya Uwekezaji Mahiri (SIS) kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kutumia nyaraka zenye shaka. Hiyo SIS ilitolewa na TIC kwa Friedkin siku moja [Agosti 20, 2015] na kuridhiwa siku hiyo hiyo na Nyalandu [Agosti 20, 2015]; huku maofisa wa Idara ya Wanyamapori wakiwa hawana habari.

Kampuni za Friedkin zilipanua mgogoro kwa kuandika barua kwa wabunge wa Marekani zikidai kuwa wao wakiwa wawekezaji, wananyanyaswa na Serikali ya Tanzania na kuibeba GMS.

Baraza la Congress la Marekani lilimwandikia Rais Barack Obama wa Marekani barua likiituhumu Idara ya Wanyamapori ya Tanzania kwa kuinyanga’anya Kampuni ya Friedkin kitalu na eti kukitoa isivyo halali kwa kampuni nyingine ya kigeni, jambo ambalo halikuwa kweli, kwani GMS ni ya Kitanzania.

Upotoshaji huo uliwasilishwa kwenye Baraza la Congress baada ya Friedkin na WWS kushindwa kesi mahakamani, japo kwenye tuhuma hizo hawakueleza kuwa wameshindwa kesi.

Miaka kadhaa iliyopita Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitaka uchunguzi ufanywe na apewe ripoti kutokana na malalamiko ya wanakijiji juu ya vitendo vya unyanyasaji vilivyodaiwa kufanywa na Kampuni ya Mwiba Holdings iliyojimilikisha eneo la Mwiba mkoani Simiyu na kuliita Mwiba Ranch huku likiwa halikidhi kabisa vigezo vya kuwa ranchi ya wanyamapori.

Matakwa ya kampuni hiyo kupewa haki ya matumizi ya eneo hilo kama ranchi, awali yalikataliwa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki, kwa msingi wa kukosa vigezo, aliyekuwa naibu wake, Nyalandu akiwashinikiza wakurugenzi wa wanyamapori wakiuke amri ya waziri na kutoa haki hiyo kwa Mwiba.

Ni wakati huo wa Nyalandu ambapo aliamua kukigawa kitalu kilichokuwa kinamilikiwa na GMS kwa Friedkin na akaagiza wapewe Leseni ya Rais kwa rafiki zake hao kinyume cha sheria, akiruhusu waue wanyamapori 708 wakiwemo tembo na simba. 

Leseni hiyo ya siku 21 ilitolewa Agosti 01, 2014. Familia ya Friedkin ya watu wanane wakiwamo watoto ikaruhusiwa kuua wanyama hao bila malipo yoyote kwa serikali. Waliohusika ni Thomas Dan Friedkin, Thomas Hoyt Friedkin, Susan Fridkin, Debra Friedkin, Thomas Dan Friedkin Jr, Ryan Friedkin, Corbin Friedkin na Savannah Friedkin.

Hapakuwapo maelekezo ya rais ya kutoa leseni hiyo. Lakini pia mwaka 2014 hapakuwapo Leseni ya Rais, bali kulikuwa na Leseni Maalumu. Tangazo la Serikali Na. 273 la mwaka 1974 lilihusu uwindaji kwa mujibu wa Sheria Na. 12 ya mwaka 1974 ambayo iliruhusu uwepo wa Leseni ya Rais. Sheria Na. 12 ya mwaka 1974 ilifutwa na Sheria Na. 5 ya mwaka 2009. 

Katika Sheria Na. 5 ya mwaka 2009 hakuna Leseni ya Rais, bali kuna Leseni Maalumu.

Familia ya bilionea Friedkin ilianza kuwekeza nchini Tanzania mwaka 1987 baada ya kuinunua Kampuni ya Ker & Downey Safaris (Tanzania) Limited (KDT) na Tanzania Game Tracker Safaris Limited (TGTS). KDT inajihusisha na utalii wa picha na TGTS ni ya uwindaji wa kitalii. Mwaka 1994, taasisi isiyolenga kutengeneza faida ya Friedkin Conservation Fund (FCF) ilianzishwa kwa kile kinachotajwa kuwa ni kufanya miradi ya maendeleo ya jamii na kuendesha operesheni dhidi ya ujangili katika vitalu kwa niaba ya TGTS.

Familia ya Friedkin imewekeza kwenye biashara ya ndege chini ya TGTS kuanzia mwaka 1992 na baadaye walitenganisha na kuanzisha Northern Air (NA) kama kampuni ya kibiashara ya usafiri wa anga mwaka 2005. 

Mwaka 2002, Familia ya Friedkin iliinunua Wengert Windrose Safaris (Tanzania) Limited (WWS), ambayo ni kampuni ya uwindaji wa kitalii iliyoanzishwa mwaka 1985. Mwaka 2007, Mwiba Holding Limited (MHL) ilianzishwa. 

MHL ndiyo iliyoanzisha Mwiba Wildlife Ranch na kuibua kelele kutoka kwa wahifadhi kuwa kisheria wakati huo ranchi haikupaswa kuanzishwa umbali wa kilometa sifuri kutoka Hifadhi ya Taifa.