Msimu wa zao la pamba unakaribia kuanza, huku hali ya ubora na uzalishaji wake hapa Tanzania ukiwa hauridhishi. Kilimo cha Mkataba bado hakijafanya kazi.

Wakulima wa pamba katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara na sehemu nyingine nchini, wanasubiri kwa hamu kubwa kusikia bei ya zao hilo inatangazwa, na serikali kuona kama itakuwa na sura ya kumkomboa mkulima wa zao hilo la biashara.

Nimefanya ziara mkoani Simiyu, kama mkoa unaoongoza kwa kilimo cha zao hilo. Nimetembelea baadhi ya wakulima katika wilaya za Bariadi na Maswa na kuongea nao juu ya hali ya kilimo cha pamba msimu huu.

 

Nimezungumza pia na Mkuu wa Mkoa huo, Paschal Mabiti, kujua serikali inasemaje juu ya kilimo hicho msimu huu. Pia nimeongea na wafanyabiashara (wanunuzi) wa pamba.

 

Alliance Ginneries ni mfanyabiashara na mnunuzi wa pamba mkoani Simiyu. Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa Pamba Tanzania (TCA), Boaz Abiero, ambaye ni Meneja wa kampuni hiyo, anabainisha kuwa kuna hatari ya bei ya pamba kushuka msimu huu kutokana na kukosa mipango thabiti ya kuboresha uzalishaji wake.

 

Anasema hali hiyo inatokana na wakulima wengi kupulizia dawa mara moja, jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za kilimo cha pamba zinazotaka zao hilo lipuliziwe dawa mara tatu.

 

Abiero anasema utafiti uliofanywa na kiwanda chake umebaini kuwa wakulima wengi wa pamba mkoani Simiyu hupulizia mara moja, hali inayosababisha ubora wa pamba kupungua, kwani nyingi huharibika kutokana na kukosa dawa ya kutosha kuua wadudu waharibifu.

 

Chanzo cha tatizo hilo kinatajwa kuwa ni pamoja na kusitishwa kwa Kilimo cha Mkataba, hali inayowafanya wakulima wengi kulima kienyeji kutokana na kukosa pembejeo, mbegu bora na dawa.

 

Takwimu za uzalishaji wa zao hilo kwa msimu wa mwaka jana zinaonesha kuwa hekta 1,420,000 zililimwa na kuzalisha kilo 354,000 za pamba. Mwaka huu hekta 1,500,000 ndizo zinazotarajiwa kutumika katika uzalishaji wa zao hilo.

 

Abiero anatabiri kuwa ushindani wa kibiashara utakuwa mkubwa na viwanda vya kusindika pamba hapa Tanzania vinakabiliwa na hatari ya kupata hasara kutokana na zao hilo kukosa bora.

 

Mfanyabiashara mwingine, Jeremiah Malongo, mwakilishi wa kampuni ya Vitrex Oil, anakiri kuwapo kwa hali mbaya ya zao hilo.

 

Anasema uzalishaji wa pamba umepungua ikilinganishwa na mwaka jana, na kuongeza kuwa ukosefu wa ubora ndiyo kikwazo cha kupanda kwa bei ya pamba.

 

Je, wakulima wa pamba katika wilaya za Bariadi, Maswa wanazungumziaje kilimo cha pamba msimu huu?

 

Baadhi ya wakulima katika Kijiji cha Zanzui, Kata ya Zagayu wilayani Itilima, wamesema kuwa hali ya zao la pamba si nzuri sana wakitaja sababu kuwa ni kusitishwa kwa Kilimo cha Mkataba.

 

Wamesema msimu huu hawakupata dawa za kutosha kutokana na kuuzwa bei ghali wasiyoweza kuimudu, kutokana na uwezo mdogo wa kiuchumi walionao.

 

Wakulima hao wamesema kwa sasa baadhi yao wameanza kuuza pamba licha ya serikali kutotangaza kuanza kwa msimu huo. Wanauza kwa baadhi ya watu wanaoingia vijijini kununua pamba. Wanauza zao hilo ili kupata fedha za kujikimu na familia zao.

 

Wanabainisha kuwa kuuza pamba kabla ya bei husika kutangazwa na serikali ni tatizo, kwani hali hiyo inatoa mwanya wa wao kuibiwa katika mizani inayotumika kupima zao hilo.

 

Katika msimu uliopita, Kilimo cha Mkataba kilikuwa kinatekelezwa ambapo wakulima waliweza kukopeshwa pembejeo, dawa na mbegu bora za pamba. Hali hiyo ilisababisha kuongezeka kwa uzalishaji wa zao hilo na lenye ubora unaohitajika.

 

Inaelezwa kuwa Kilimo ch Mkataba kimesitishwa ghafla ili kurekebisha baadhi ya mambo katika mkataba huo, lakini pia kuangalia kama bei ya pamba itaongezeka na kuwanufaisha wakulima ipasavyo.

 

Kwa upande mwingine, inaelezwa kuwa Kilimo cha Mkataba kimesitishwa kutokana na ‘kelele za wanasiasa’.

 

Wakulima na wanunuzi wengi wa pamba wanakiri kuwa wanasiasa wanachangia kwa kiasi kikubwa kusitishwa kwa Kilimo cha Mkataba kwa lengo la kutaka kuonekana wanataka kutetea bei ya pamba iliyoshuka.

 

Baadhi ya wakulima wa pamba katika Wilaya ya Maswa wamezungumza hadi kutoa machozi, baada ya kukumbuka walivyodanganywa na wanasiasa kwamba wasitumie dawa wala mbegu kwa maelezo kuwa mbegu zile hazitaota na kwamba dawa zitaharibu ardhi.

 

Wanasema mbunge mmoja aliwakataza kuchukua mbegu hizo na dawa za pamba, na kwamba hata watakaojiunga na Kilimo cha Mkataba watapokonywa mashamba na ardhi yao na wanunuzi wa zao hilo.

 

Hata hivyo, baada ya kuzuiwa kutumia mbegu, dawa na Kilimo cha Mkataba, wakulima hao waliachwa bila kuelezwa njia mbadala kutoka kwa wanasiasa hao.

 

Inaelezwa pia kwamba wapo wanasiasa wanajiita watetezi wa wanyonge ambao walitoa maneno ya “No book no cotton” wakati wa sakata la kushuka kwa bei ya pamba msimu uliopita. Matamshi hayo yalikuwa yanamaanisha kuwa hakuna pamba kwa mnunuzi kama hana Sh 1,000. Hali hiyo ilisababisha baadhi ya wakulima kukasirika na kuchoma mavuno yao ya pamba.

 

Hiyo ndiyo aina ya wanasiasa tulionao katika Tanzania yetu. Hakuna mtu anayepinga siasa katika kutafuta haki au dhana nzima ya demokrasia, lakini siasa zisizo na tija katika masuala muhimu kama kilimo ambacho kinatazamwa kama uti wa mgongo wa Taifa letu lazima tuzikatae zote.

 

Kitendo cha wanasiasa kuingilia na kukwaza wakulima juu ya Kilimo cha Mkataba hakikubaliki kwani kinarudisha nyuma maendeleo ya wakulima nchini.

 

Binafsi ninamuunga mkono Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Paschal Mabiti, kwa uamuzi wake wa kupiga marufuku wanasiasa wanaowakwaza wakulima kuhusu masuala ya kilimo katika mkoa huo.

 

Mabiti amesema mwanasiasa atakayebainika kuwadanganya na kuwakwaza wakulima, atakamatwa na kufikishwa mahakamani ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia na tabia ya kutaka kuona wakulima wanaendelea kubaki maskini huku wakizungukwa na ardhi yenye rutuba ya kustawisha mazao mbalimbali.

 

Kauli hiyo ya Mabiti ni kama imeleta ahueni kwa wakulima na wanunuzi wa pamba mkoani Simiyu. Wakulima na wanunuzi wengi wa pamba wanaomba Kilimo cha Mkataba kirejeshwe haraka kwa manufaa ya wakulima.

 

Elimu inatajwa kuwa ni nyenzo muhimu inayohitajika kutolewa kwa wakulima kuhusu Kilimo cha Mkataba, kwani wengi wao hawajui manufaa ya mpango huo, jambo ambalo limewapa wanasiasa mwanya wa kuchombeza siasa zisizo na tija kwa wakulima.

 

Ni vyema sasa wanasiasa wakiwamo wabunge na madiwani wajenge tabia ya kutumia michango yao vizuri, ikiwa ni pamoja na kusaidia kuboresha kilimo nchini na kujiepusha na kasumba ya kujitafutia umaarufu wa kisiasa na maslahi binafsi.

Pamba ni dhahabu nyeupe.

 

[email protected]