Msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara umefungiliwa rasmi. Sasa, fitina, mizengwe, ujuaji, uamuzi mbovu wa waamuzi, upanguaji wa ratiba na mengi ya kero ndiyo tutakayoanza kuyashuhudia.

Msimu uliopita ulimalizika huku kukiwa na malalamiko kadhaa kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka, ambao mwisho walitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), pamoja na Bodi ya Ligi Kuu kujitathmini.

Zilionekana kasoro tatu kubwa nazo ni ligi kukosa mdhamini, ratiba kupanguliwa mara kwa mara pamoja na waamuzi kuchezesha chini ya kiwango.

Nilikuwa naitazama mechi ya Yanga dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa hivi karibuni katika Uwanja wa Kaitaba. Nikawaona mashabiki wengi ambao naamini wengi wao wanatoka katika wilaya za Mkoa wa Kagera na wengine ni kutoka mikoa ya jirani. Hakuna kocha ambaye hakulalamika, kila mmoja alipaza sauti yake.

Kuna maswali

Wakati mwingine unajiuliza, ni kwa nini Kagera Sugar wanapocheza na timu nyinginezo za Ligi Kuu ambazo hazina ushawishi kama wa Yanga au Simba, uwanja utakuwa na idadi ndogo sana ya mashabiki?

Hata mechi kati ya Simba dhidi ya Mtibwa itajaa mashabiki kutoka Jiji la Dar na wengine kutoka Morogoro. Mtibwa hao hao wakicheza na klabu nyingine isiyo na umaarufu kama ule wa klabu kongwe za Dar, idadi ya mashabiki itakuwa ni ile ya kukatisha tamaa.

Wakati tunaiachia TFF na Bodi ya Ligi Kuu juu ya hizo changamoto, lazima tukubali klabu nyingi za mikoani zinakumbana na uadui kutoka ndani ya sehemu zilipo. Shabiki wa soka anayeishi wilaya moja nchini anaona ufahari kiasi cha kujisifu ana kadi mpya ya Simba, wakati hapo hapo wilayani kwake kuna klabu yenye kuendeshwa kwa kutegemea michango ya mitaani.
Mara nyingi tu, vyombo vya habari vinaripoti jinsi ambavyo klabu kadhaa za ligi, zinavyokuwa kwenye mchakato wa kuhama kutoka sehemu zilipo, sababu hasa ikiwa ni ile hali ya kupingwa na wenyeji wa eneo husika. Mtu huyu huyu anayeanzisha fitina ili timu fulani ihame kutoka kwenye eneo analoishi, ni wa kwanza katika kuwapokea Simba na Yanga wanapokwenda kucheza mechi za Ligi Kuu.

Usipokipenda kile cha nyumbani kwako, sehemu ambayo unayojivunia kuiita nyumbani, utakipenda kipi kwa moyo wako wote? Muhimu kwa shabiki ni kutambua kwamba uhai wa soka la Tanzania hauwezi kuwa na ustawi mzuri ikiwa timu chache sana zitaendelea kuwa na uhakika wa kuendelea kuwepo kwa muda mrefu kwenye soka letu.

Klabu nyingi hasa kutoka mikoani zimeshindwa kudumu na kwa kiasi fulani ni kutokana na ile hali ya wadau wa mikoani kukosa kuzifanya timu hizo kama mali za kwao. Mchango wa uendelezaji wa klabu za wenzetu unahusiana moja kwa moja na uwepo wa timu, miaka na miaka.

Nitafurahi kuiona timu kama Mbeya City inaendelea kuwepo na kuzeeka kama ambavyo Simba na Yanga zilivyo. Nitafurahi sana kusikia Ndanda FC inaendelea kuimarika siku baada ya siku, huku ikizidi kupata wanachama wapya, ambao wataweza kutengeneza mtandao wenye nia ya kuiimarisha timu yao.

Simba na Yanga ziko kilometa zaidi ya mia saba kutoka kwenye wilaya kama Sumbawanga na Ileje, sasa kwa nini watu wa maeneo kama hayo waone fahari katika kuutunza uwepo wa timu mbili tena za mbali kabisa kutoka katika mikoa yao?

Tanzania inazidi kuzalisha wasomi wenye hadhi ya shahada za vyuo vikuu, karibu kila kona ya nchi hii kuna kielelezo cha ukuaji wa sekta ya elimu. Kwa hiyo wenye kuyafahamu mahitaji ya uendelezaji wa timu katika mtazamo wa kimenejimenti, wapo na wanazidi kuongezeka kadiri vyuo vinavyozidi kuzalisha wasomi.

Hili tulikubali

Sioni ni kwa nini jamii pana ya watu wa Kigoma iendelee kuona mkoa wenye historia nzuri ya kutoa wanasoka bora, unakuwepo bila ya kuwa na timu ya Ligi Kuu ambayo ni fahari ya wanamkoa?

Ni kichekesho kumuona mdau wa soka wa klabu za mikoani akihangaika kwa nguvu zake zote, eti kuhakikisha Simba na Yanga hazipotezi mechi kwenye uwanja wa ugenini, baada ya mechi kumalizika anageuka adui wa klabu ya mkoa ambao wazazi wake wamezaliwa na baadaye kumzaa yeye.

Mechi kati ya Yanga na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba ilijaza mashabiki, lakini subiri siku Kagera Sugar itakapocheza na Ndanda FC uone kama uwanja utajaa.

Wale wale waliotoka katika kila kona ya mkoa kwenda uwanjani kuwatazama Wabrazili, wataendelea na shughuli zao kama vile hakuna kinachoendelea pale Kaitaba. Simba na Yanga zinaendelea kuwepo na kustawi lakini ni kwa hasara ya kutoweka kwa klabu za mikoani.

Wadau wa soka nje ya Dar waseme sasa basi, hatuwezi kuendelea kufanya kazi ya mshumaa, wenyewe unateketea lakini wengine wanapata mwanga.