Kundi la watu wanaouguza zaidi ya wagonjwa 1,000 wanaoishi katika banda nje ya geti la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wamepanga kuandamana kwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kufuatia kitendo cha uongozi wa hospitali hiyo kuwanyima huduma za kibinadamu.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mwenyekiti wa wauguzi hao, Nasibu Khalifa, anasema uongozi wa hospitali hiyo umewafungia huduma za kujisaidia na kuwataka walipie huduma hiyo.
Khalifa anasema kutakiwa kulipia huduma za kujisaidia kunaongeza mzigo kwao, hasa ukizingatia kuwa wana jukumu la kulipia matibabu ya ndugu zao waliolazwa hospitalini humo.
“Tunachoomba ni kuwa tupewe huduma za malazi na kujisaidia bure kwa kipindi chote tunachokuwa tukiuguza wapendwa wetu, kwani hali zetu ni ngumu kimaisha,” anasema.
Anasema wengi wa watu waliopo katika eneo hilo ni wale waliotoka katika mikoa mbalimbali kuja kuuguza wapendwa wao na hawana uwezo wa kulipia huduma ya kujisaidia, kufua na kuoga muda wote wanapokuwa katika eneo hilo, kwani hata uwezo wa kujitafutia chakula chao wenyewe ni shida.
Anasema iwapo uongozi wa hospitali hiyo hautawasaidia, wamepanga kuandamana kwenda ofisini kwa Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutoa kilio chao kwa lengo la kumuomba awasaidie.
Khalifa anasema kuwa wameamua kuandamana kwenda kwa Mkuu wa Mkoa kwa sababu hawana uwezo wa kulipia huduma hizo kutokana na hali zao.
Anasema hatua ya uongozi kuwataka walipie huduma za vyoo ni kuwanyanyasa, kwani uongozi huo unaelewa fika kuwa wao hawana shughuli yoyote ya kujiingizia kipato jijini Dar es Salaam.
Banda hilo lilitolewa na uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kama sehemu ya watu wanaokwenda kuwaona wagonjwa kupumzika wakisubiri muda wa kuingia wodini.
Anasema hata hivyo, watu ambao wanatoka mikoani na ambao hawana ndugu Dar es Salaam wamekuwa wakilitumia banda hilo kujihifadhi katika kipindi chote wanapouguza ndugu zao.
Khalifa anasema kuwa utaratibu wa zamani, walikuwa na fursa ya kujisaidia, kuoga na kufua bure wakati wa jioni.
Anasema ingawa mazingira hayakuwa mazuri, lakini waliivumilia hali hiyo kwa sababu vyoo vinafunguliwa saa moja jioni ili wajisaidie.
Anaongeza kuwa aliyetaka kujisaidia wakati wa mchana alilazimika kutafuta huduma hiyo katika sehemu nyingine za kulipia.
Anasema kuwa walishangaa kuona huduma hiyo ya kujisaidia imekatishwa na mzabuni wa eneo hilo aliyewaeleza kuwa kuanzia sasa watatakiwa kulipia huduma hizo.
Anasema chini ya utaratibu mpya, mtu anayetaka kufua shati moja anapaswa kulipia Sh 1,000, wakati anayetaka
kujisaidia anapaswa kulipa Sh 200, huku yule anayetaka kuoga akitakiwa kulipa Sh 500.
Aidha, wamelalamikia kitendo cha mzabuni mpya anayeendesha huduma za kujisaidia ambaye amekusanya virago vyao na kuvitupa akidai kuwa ni takataka.
Godfrey Msungu, mmoja wa watu wanaouguza wagonjwa Muhimbili, anasema kwa sasa mazingira ya kuishi katika
makazi hayo si salama, kwani mvua ikinyesha mabanda hayo yamekuwa yakivuja sana.
Anasema hadi sasa hawaelewi iwapo eneo hilo linamilikiwa na mzabuni wa Hospitali ya Muhimbili.
Alfonce Maleba, anaitaka serikali iangalie umuhimu wa kuongea na mzabuni huyo kupunguza bei za vyakula na
vinywaji ili wamudu kununua kulingana na hali zao kuwa duni.
Akizungumza na JAMHURI, Grace Ndesamburo, aliyepewa zabuni ya kuendesha eneo hilo, anasema yeye ni mzabuni tu, aliyeshinda tenda ya kuendesha eneo hilo kwa mkataba halali na yupo hapo kihalali kuendesha huduma za choo, jiko na duka kwa ajili ya kufanya biashara na kutoa huduma kwa wateja wanaokuja katika eneo hilo.
Kuhusu wauguzi hao kulazimishwa kulipia huduma za choo, anasema hilo si kosa lake, kwani yeye anafanya biashara.
“Awali kulikuwa na mhudumu wa vyoo wa hospitali ambaye alikuwa akiacha vyoo wazi wakati wa usiku ili wajisaidie bure
mpaka asubuhi,” anasema.
Anasema kuwa aliposhinda zabuni hiyo alikabidhiwa eneo lote, na yeye anahusika kuhakikisha liko safi na salama.
Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Muhimbili, Sophia Mtakasimba, anasema kuwa uongozi wa hospitali haukuwa
na taarifa za malalamiko hayo na atayafuatilia.