Katika kukabiliana na wimbi la ujangili, Wizara ya Maliasili na Utalii imewataka watu wote wanaomiliki nyara za Serikali bila vibali, kujitokeza kueleza namna walivyozipata.

Msemaji wa Wizara hiyo, George Matiko, amesema uamuzi wa Serikali unalenga kuhakikisha kuwa wamiliki hao wanamiliki nyara kihalali au wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

Amesema, “Mtu yeyote haruhusiwi kumiliki nyara za Serikali, yaani mnyamapori au kipande chochote cha mnyamapori, bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori.

“Hii inatokana na Kifungu cha 86(1) na (2) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Sura Na. 283 ya mwaka 2009 kinachopiga marufuku kumiliki nyara kinyume cha sheria.

“Kwa mfano, mtu yeyote haruhusiwi kumiliki chui, simba, pundamilia, fisi au mnyama yoyote kwa sababu yoyote ile, bila kibali kinachotolewa kisheria. Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Sura Na. 283 inatoa tafsiri ya nyara za Serikali kuwa ni mnyamapori aliye hai au aliyekufa ikiwa ni pamoja na masalia yake. Masalia hayo ni pembe, mifupa, ngozi, kucha, kwato, nyama, nywele, manyoya, mayai au sehemu yoyote ya mnyamapori au nyara zilizotengenezwa.”

Wizara inawataka watu wote wanaomiliki nyara bila vibali, watoe taarifa na maelezo kuhusu namna walivyopata nyara hizo kwenye Ofisi za Idara za Wanyamapori za wilaya, mkoa, Mapori ya Akiba au Kikosi dhidi ya Ujangili.

“Baada ya uhakiki taarifa hizo zitawasilishwa Idara ya Wanyamapori Makao Makuu, ili uamuzi sahihi ufanyike kuhusu kuhalalisha umiliki huo au vinginevyo. Kutokana na Kifungu cha 87(1) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Sura ya 283, Wizara inamtaka mtu yeyote atakayeona nyara za Serikali zikimilikiwa na mtu asiyehusika, au asiyekuwa na kibali, kutoa taarifa kwenye ofisi za Maliasili, Wanyamapori au Polisi,” imesema Wizara ya Maliasili na Utalii.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwa mkoani Shinyanga, alipigwa na butwaa baada ya kuburudishwa na kikundi cha ngoma kilichokuwa na fisi. Watu wa jamii ya Kisukuma ni kawaida kuwafuga wanyamapori hao. Huwatumia kwa shughuli mbalimbali, zikiwamo za usafiri, ngoma na wakati mwingine kwa ushirikina.

Aidha, wimbi la watu kukamatwa na nyara hizo linaongezeka kwa kasi. Hivi karibuni kumekuwa na matukio ya kukamatwa kwa magari yenye namba bandia za miradi, yakiwa na shehena kubwa ya pembe za tembo. Tukio la karibuni limetokea mkoani Ruvuma.