*Mwenyekiti CCM atajwa, Serikali Kuu ndiyo inaongoza
*Takukuru, Usalama wa Taifa, wafanyabiashara wamo
SERIKALI na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa nchini, ndiyo wanaoelekea kuufilisi Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF). Mfuko unawadai Sh trilioni 6.4. Wafuatao ndiyo wadaiwa wakuu.
Mfuko ulitoa mkopo wa Sh bilioni 1 kwa riba ya asilimia 13 kwa mwaka kwa Kampuni ya TPI, Juni 2001. Kampuni hii ni mali ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida. Mkopo huo ulikuwa ni wa muda wa miaka mitano. Kampuni ilikuwa ikirejesha mkopo vizuri hadi kufikia mwaka 2005 ambako kampuni ilianza kusuasua kulipa mkopo huo. Hadi kufikia Juni 2005, kampuni ilikuwa ikidaiwa Sh 440,057,632.03.
Utendaji wa kampuni ulishuka kwa kiasi kikubwa na uzalishaji kusimamishwa mwaka 2008. Hata hivyo, kampuni hiyo iliingia makubaliano na Umoja wa Ulaya (EU) ambako Umoja huo ulitoa euro milioni 5 mwaka 2010, kwa ajili ya kuanzisha mtambo mpya mahsusi kwa ajili ya uzalishaji ARV (Dawa za kupunguza makali ya Ukimwi). Mtambo mpya ulikuwa uanze uzalishaji Julai 2012. Hata hivyo, kutokana na kashfa ya uzalishaji wa dawa bandia za ARV, Serikali iliamuru kiwanda hicho kifungwe, hivyo uzalishaji haukuweza kuanza.
Uongozi wa Mfuko ulifanya jitihada za kufuatilia kwa kina ili kuhakikisha deni hilo linalipwa, lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda. Hivi sasa Mfuko umeungana na Benki ya Barclays (T) Ltd kuanzisha hatua za kisheria dhidi ya TPI ambako kesi imepangwa kutajwa Mei 2, mwaka huu.
Hadi kufikia Machi, mwaka huu TPI ilikwishalipa Mfuko Sh 872,455,258. Kati ya hizo, Sh 564,942,368 riba ni Sh 300,409,559.2 na tozo ni Sh 7,103,330.8. Hadi kufikia Machi 31, mwaka huu, kiasi cha deni linalodaiwa lilifikia Sh 1,201,304,369.51 ambako Sh 440,057,632.03 ikiwa ni mtaji, riba Sh 628,517,965.90 na tozo ni Sh 132,728,771.59.
21st Century Textile
Mkopo wa Sh bilioni 10 wenye riba ya asilimia 11 kwa mwaka, ulitolewa kwa kampuni ya 21st Century Textle mnamo Septemba, 2006. Kiwanda hiki ni mali ya mfanyabiashara nguli, Mohamed Dewji. Mkopo huu ni wa muda wa miaka 10 wenye kipindi cha neema (grace period) cha miaka miwili na umedhaminiwa na Serikali kwa asilimia 75. Mkopo huu ni sehemu ya Sh bilioni 45 ambazo zilikopeshwa kampuni hii na mabenki pamoja na Mifuko miwili ya jamii.
Mwaka 2008 kampuni iliomba kuongezewa muda wa kipindi cha neema (grace period) kutokana na hali mbaya ya soko na kuzorota kwa hali ya uchumi duniani kwa jumla. Kamati ya Bodi ya Fedha na Uwekezaji iliridhia ombi hilo. Kampuni ilianza kulipa mtaji mwishoni mwa Septemba 2011. Hadi kufikia Machi 31, mwaka huu, kampuni ilikuwa tayari imekwishaulipa Mfuko Sh bilioni 9.64 ambako Sh bilioni 2.7 ikiwa kama mtaji na Sh bilioni 6.97 kama riba. Kufikia Machi 31, mwaka huu, jumla ya deni lililobaki kulipwa ni Sh bilioni 7.33. Kampuni inaendelea vizuri na inalipa madeni kwa wakati.
Kagera Sugar Ltd
Mfuko ulitoa jumla ya Sh bilioni 12 kama mkopo kwa kampuni ya Kagera Sugar Ltd kati ya Februari 2005 na Desemba 2005 ikiwa ni sehemu ya mkopo wa Sh bilioni 74.4 uliotolewa kwa kampuni hiyo. Mkopo huu umetozwa riba ya asilimia 10 kwa mwaka na umedhaminiwa na Serikali kwa asilimia 80. Kampuni hii ilishindwa kulipa mkopo wake katika miaka minne ya kwanza kutokana na changamoto za uzalishaji zilizosababishwa na ukame na ucheleweshwaji wa vitendea kazi kutoka nje.
Mipango mbalimbali ya kufufua na marekebisho vilifanywa ili kuhakikisha ahueni ya mkopo huu. Hatimaye, Desemba 17, 2008 wakopeshaji na wakopaji walitia saini makubaliano mapya ya marekebisho ya mkopo huo. Kampuni ilianza kulipa mkopo wake Septemba 30, 2008 chini ya utaratibu mpya wa ulipaji. Kufikia Machi 31, 2013 kampuni ilikuwa tayari imekwishalipa Mfuko Sh bilioni 7.21 ambako kati ya kiasi hicho mtaji ulikuwa ni Sh bilioni 2.2 na riba Sh bilioni 5.01. Hadi kufikia Machi 31, mwaka huu jumla ya deni lililobakia lilikuwa ni Sh bilioni 10.05. Kampuni inaendelea vizuri na inalipa madeni kwa wakati.
Kiwira Coal Mine
Mfuko ulitoa mkopo wa miaka saba wa Sh bilioni 5 kati ya Julai 2005 na Februari 2006 kwa kampuni ya mgodi wa Kiwira, yaani Kiwira Coal Mine. Mkopo huo wenye riba asilimia 11.7 kwa mwaka ulidhaminiwa na Serikali kwa asilimia 75. Kampuni hii ilishindwa kurejesha mkopo huu kutokana na kushindwa kupata fedha zaidi kwa ajili ya kufufua na kuongeza uzalishaji. Serikali iliamua kuichukua Kampuni ya Kiwira mwaka 2009 na kuahidi kwamba ingeulipa mkopo na wadeni wengine madeni yao.
Novemba 2012, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini iliulipa Mfuko kiasi cha Sh bilioni 8.64 kwa mkupuo. Kiasi hiki kilijumuisha ulipaji wa asilimia 100 ya mtaji wote na asilimia 66.2 ya malimbikizo ya riba. Serikali imeahidi kulipa kiasi cha riba kilichobaki na tozo cha Sh bilioni 4.9 katika mwaka wa fedha wa 2013/2014.
TANESCO
Mfuko ulitoa mkopo wa Sh bilioni 3 kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kati ya mwaka 2007 na mwaka 2009. Mkopo huo ulikuwa una malipo ya kipindi cha miaka sita chenye kipindi cha neema (grace period) miezi 18 kwenye malipo ya mtaji. Riba inayotozwa kwenye mkopo huu ni kati ya asilimia 0.5 kwa mwaka na asilimia 2 kwa mwaka juu ya riba kwenye dhamana ya Serikali ya siku 182. Kiasi hicho cha riba hulipwa kila baada ya miezi sita.
Kufikia Machi 31, mwaka huu, TANESCO walikwishaulipa Mfuko Sh bilioni 30.71 ambako kati ya kiasi hicho, mtaji ulikuwa Sh bilioni 20 na riba Sh bilioni 10.71. Hadi kufikia Machi 31, mwaka huu, jumla ya deni lililobaki lilikuwa Sh bilioni 10. Kampuni inaendelea vizuri na inalipa madeni kwa wakati.
MIKOPO KWA AJILI YA MIRADI YA SERIKALI
Chuo Kikuu cha Dodoma
Huu ni mradi maalumu wa Serikali uliofadhiliwa na Mfuko. Mfuko ulitakiwa kuwekeza katika ujenzi wa Chuo cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dodoma kwa riba ya asilimia 15 kwa mwaka. Jumla ya mkopo kwa ajili ya mradi huu ni Sh bilioni 109.4. Mradi huu ulimalizika Februari 2012 na kukabidhiwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma. Serikali imeudhamini mradi huu kwa asilimia 100. Hesabu za mwisho na ripoti ya kufungwa kwa mradi zimeshakabidhiwa kwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya malipo. Serikali inatarajiwa kuanza kurejesha mkopo katika mwaka wa fedha wa 2013/2014.
Mradi wa nyumba za polisi
Mfuko ulikubaliana na Serikali kujenga makazi kwa Jeshi la Polisi katika Kambi ya Kilwa Road, Dar es Salaam. Jumla ya mkopo huo wenye riba ya asilimia 15 kwa mwaka ni Sh 12,921,644,865.72. Mradi huu umedhaminiwa na Serikali kwa asilimia 100. Ripoti ya kukamilika kwa mradi, na ratiba ya mchanganuo wa ulipaji tayari umekwishawasilishwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya ulipaji wa mkopo. Serikali imeahidi kuanza kulipa mkopo huu katika mwaka wa fedha wa 2013/2014.
Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu
Mfuko ulitoa mkopo wa Sh bilioni 54.64 kwa Bodi hiyo katika kipindi cha kuanzia Februari 2006 hadi Februari 2007 kama ifuatavyo:
*Sh bilioni 20 kwa riba ya asilimia 15 kwa mwaka iliyotolewa Februari 2006 ambayo asilimia 50 ilitakiwa kulipwa Septemba 2006. Hata hivyo, kipindi cha ulipaji wa mkopo huu kiliongezwa kwa mwaka mmoja na kiasi cha riba cha Sh bilioni 1.64 kilijumuishwa kwenye mtaji huo na kufikia Sh bilioni 21.64.
*Sh bilioni 11 kwa riba ya asilimia 13.5 kwa mwaka iliyotolewa Juni 2006 kwa kipindi cha miaka miwili hadi Juni 2008.
*Sh bilioni 22 kwa riba ya asilimia 15 iliyotolewa Februari 2007 deni ambalo ilibidi lilipwe kwa kipindi cha mwaka mmoja, yaani Februari 2008.
Mikopo hii yote imedhaminiwa na Serikali kwa asilimia 100. Bodi ya Mikopo ilishindwa kulipa madeni hayo na hadi sasa imefanikiwa kulipa Sh bilioni 21.9 tu. Hata hivyo, Bodi hii imeuandikia Mfuko barua ya kuomba kusamehewa tozo la madeni hayo na Bodi hiyo imeahidi kuanza kulipa Sh bilioni 20 kila mwaka kuanzia mwaka wa fedha wa 2013/2014. Hadi kufikia Machi 31, mwaka huu, jumla ya deni lilifikia Sh bilioni 128.8 ambako Sh bilioni 54.64 ni mtaji, Sh bilioni 38.15 kiasi cha riba na Sh bilioni 36.01 ikiwa ni tozo.
Ukumbi wa Bunge
Mfuko ulishiriki ujenzi wa Ukumbi wa Bunge kupitia PPL. Kiasi kilichowekezwa na Mfuko kati ya Februari 2005 na Agosti 2006 kilikuwa Sh bilioni 9.6 kwa riba ya asilimia 12.94 kwa mwaka. Utaratibu wa uwekezaji huu ni kwa njia ya mkopo wa miaka 10 uliotolewa kwenye kampuni ya PPL ambayo Mfuko unamiliki hisa zake kwa asilimia 30.
Kiasi cha mtaji kilicholipwa kufikia Machi 31, mwaka huu, kilikuwa Sh bilioni 3.23 wakati kiasi cha riba kilikuwa ni Sh bilioni 5.2 ambayo kwa jumla ukusanyaji wake ni Sh bilioni 8.43. PPL imeshindwa kuwasilisha malipo yoyote kuanzia Aprili 2012 hadi leo, licha ya kuwakumbusha mara kadhaa na kufuatilia Wizara ya Fedha. Hadi kufikia Machi 31, 2013 kiasi kilichokuwa kikidaiwa na Mfuko kilifikia Sh bilioni 6.52.
Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela
Novemba 2010 Mfuko ulipitisha mkopo wa Sh bilioni 13.55 kwa PPL kugharamia ujenzi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela mjini Arusha. Mkopo huu unadhaminiwa na Serikali kwa asilimia 100.
Utalipwa katika miaka 10 na una kipindi cha neema (grace period) cha mwaka mmoja kwa riba ya asilimia 15. Agosti 2011 Bodi ya PSPF iliridhia kuiongezea taasisi hiyo ziada ya kiasi cha Sh bilioni 1.35 kwa ajili ya kazi ya ziada ya ujenzi wa barabara na kuboresha mandhari. Hivyo, baada ya mkopo wa ziada, jumla ya kiasi kilichokopeshwa kwa PPL ni Sh bilioni 14.9. Malipo yanatarajiwa kuanza kulipwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 baada ya kukamilisha na kuwasilisha hesabu za mwisho kwa Wizara ya Fedha.
Usalama wa Taifa (TISS)
Mradi huu unahusu ujenzi wa majengo 10 yenye vyumba 100 vya makazi kwa ajili ya wafanyakazi wa Ofisi ya Rais maeneo ya Kijitonyama na Mbweni, Dar es Salaam. Gharama za mradi ni Sh bilioni 17.4 na ulikabidhiwa kwa mkandarasi kwa ajili ya ujenzi Desemba 18, 2009. Mkopo huu unadhaminiwa na Serikali kwa asilimia 100 kwa kipindi cha ulipaji cha miaka saba baada ya mradi kukamilika. Una riba ya asilimia 15 kwa mwaka. Mkandarasi anatarajia kukamilisha kazi na kuukabidhi mradi huo Aprili 30, mwaka huu. Baada ya hapo, Mfuko utawasilisha hesabu za mwisho pamoja na ratiba na taarifa za ulipaji kwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya malipo.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
Novemba 2009, Mfuko ulitoa mkopo wa Sh bilioni 6 kwa Takukuru. Mkopo huu ni wa miaka saba wenye kiwango cha riba cha asilimia 11 na utakaolipwa kila mwezi wa Oktoba na Aprili. Ulitolewa ili kuwezesha ununuzi wa magari kwa lengo la kuimarisha shughuli za Takukuru mikoa mbalimbali wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
Mkopo huu wenye kipindi cha neema cha mwaka mmoja, umedhaminiwa na Serikali kwa asilimia 100. Takukuru ilishindwa kulipa riba yake ya Aprili na Oktoba, 2011, hivyo kiasi hicho cha riba kikaongezeka kwenye mtaji ambao ulifikia Sh bilioni 6.68.
Takukuru pia ilishindwa kulipa riba ya Aprili, 2012 na Oktoba 2012. Hii ilisababisha limbikizo la deni kufikia Sh bilioni 2.2 ambako Sh bilioni 1.5 ikiwa ni mtaji, Sh bilioni 0.6 ni riba na Sh bilioni 0.1 ni tozo. Mfuko na Takukuru vilifuatilia Wizara ya Fedha juu ya ulipwaji wa mkopo. Wizara hiyo iliahidi kuanza kulipa mkopo katika mwaka wa fedha wa 2013/2014. Hadi kufikia Machi 31, mwaka huu, jumla ya deni linalodaiwa na Mfuko lilifikia Sh bilioni 8.89.
Mpango wa kuinusuru PSPF
Iliyokuwa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) chini ya Mwenyekiti wake, Kabwe Zitto, ilishaliona tatizo la PSPF kufilisika tangu mwaka 2011.
Kamati mpya ya POAC inayoongozwa na Zitto, wiki iliyopita ilikutana na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), uongozi wa PSPF, Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na Wizara ya Fedha kutaka kupata picha halisi ya tatizo la Mfuko huo. Kamati ilitoa wiki moja kwa Serikali kuja na majibu.
Uwezo wa PSPF wa kuwalipa wastaafu mafao yao umeelezwa kuwa umeshuka kufikia asilimia 10 badala ya asilimia 40.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSPF, Adam Mayingu, alikieleza kikao hicho kuwa kama malimbikizo ya madeni hayo hayatalipwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa, Mfuko huo utakabiliwa na hatari ya kufilisika kabisa.
Mayingu alisema malimbikizo ya madeni hayo yalianza baada ya serikali kushindwa kulipa sh bilioni 250. Alisema fedha hizo zilitakiwa zilipwe na serikali baada ya kuwaingiza watumishi wake kwenye mfuko huo ulipoanzishwa mwaka 1999.
Mayingu aliendelea kuianika serikali kuwa kabla ya PSPF kuanzishwa, watumishi wa umma wastaafu walikuwa wakilipwa fedha za mafao yao kupitia Hazina. Alisema kikosi kazi kilichoundwa na serikali mwaka 1997, kilifanya tathmini na kubaini kwamba kama serikali isingekuwa imelipa fedha hizo sh bilioni 250 kufikia mwaka 2006, upungufu wa thamani ya fedha za PSPF ungefikia sh bilioni 658.
Alishauri kwamba pamoja na kulipa malimbikizo ya madeni hayo, Serikali inapaswa kuongeza michango kutoka asilimia 15 za sasa hadi asilimia 25 ili kufidia upungufu uliopo.
Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Irene Isaka, alisema kulingana na tathmini waliyoifanya, wamebaini kuwa PSPF ina hali mbaya. Wametoa mwongozo kwa kutaka wanachama wa Mfuko huo kutolipwa kiasi chote, bali kile tu walichochangia.