Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Arusha

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limefanikiwa kuwakamata watu wawili kwa tuhuma za mauaji ya Israel Paulo (36) Mkulima na Mkazi wa Leguruki, Wilaya ya Arumeru na Mkoa wa Arusha aliyefariki dunia tarehe 5 mwezi huu wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Tengeru baada ya kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake na watuhumiwa hao.

Akitoa taarifa hiyo leo Oktoba 09, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amewataja Watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Ndewario Lazaro maarufu kwa jina Shombotoni (60) Mkulima, Mkazi wa Mwaruvango Wilaya ya Arumeru na Oscar Ndewario (29) mkazi wa Moivaro ambaye alikamatwa huko Wilaya Simanjiro Mkoani Manyara ambaye alitoroka baada ya tukio hilo.

Aidha Kamanda Masejo amesema upelelezi wa tukio hilo unaendelea na pindi utakapokamilika jalada litapelekwa ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.

Jeshi la Polisi Mkoani hapo limewashukuru wananchi wa mkoa huo kwa namna ambavyo wanashirikiana katika kuzuia matukio ya uhalifu. Pia limewaaomba wananchi kufuata sheria na kuacha kujichukulia sheria Mkononi.