Bagamoyo
Na Mwandishi Wetu
Kwa Mtanzania halisi anayebeza hadhi za machifu au watemi atakuwa mgeni au hajaisoma vizuri historia ya Tanganyika ya kale kuelekea uhuru na mchango uliotolewa na machifu katika kukijenga Chama cha ukombozi cha TANU.
Kuwapuuza machifu hao ni ishara ya mhusika kutoielewa historia ya kweli, tawala za enzi zile na tawala za kienyeji, ujio wa Wadachi, Waingereza na hatimaye kuelekea Tanganyika huru.
Hayo yamebainishwa wiki iliyopita na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mohamed Abood Saleh, alipozungumza na JAMHURI.
Anasema kuwapuuza au kuukebehi uchifu na machifu wenyewe kwa namna yoyote ile hakuonyeshi heshima na uungwana, pia ni kukinzana na hadhi za nyakati hizo na sasa.
Abood anasema machifu hawakuwa na mipaka au maeneo yaliyoitwa nchi, lakini hadhi yao katika jamii waliyoishi ilikuwa ni ya juu; waliheshimika na kama si kuwapo kwao, jamii nyingi zingeishi bila kuwa na mfumo wa maisha adilifu.
Anasema machifu wengi katika jamii walipata elimu, walijua kusoma na kuandika lugha kama vile Kiarabu, Kiswahili, Kidachi na wengine Kiingereza, tena kwa usahihi na ufasaha mkubwa.
“Kwa mfano, Mangi Mkuu Thomas Mareale, Mangi Meli na Mangi Shangali wa kaskazini mwa Tanganyika walipambana na wakoloni kuihami nchi yao dhidi ya utawaka wa Wajerumani.
“Inawezekanaje leo mtu asimame na kusema uchifu si jambo la maana?” anahoji Abood.
Anasema si kwa Tanganyika tu lakini Afrika yote ilikuwa na viongozi wake wa kijadi na kijamii waliohusika kusimamia nidhamu, maadili na maisha ya jamii ili ziishi kwa amani, umoja, kujilinda na hata ilipobidi walipambana au kuongoza mapambano.
“Jamii za kichifu au watemi waliwaongoza watu na kuzitaka jamii zijiendeshe kwa adabu, mila, akhlaq na desturi njema huku zikizingatia maadili mema ambayo sasa kiuhalisia hayapo na Bara la Afrika linakabiliwa na mporomoko mkubwa wa maadili,” anasema kada huyo wa CCM na mfanyabiashara.
Abood anasema wapo baadhi ya watu wamekuwa wakipotosha ukweli wa historia hususan katika ukanda wa pwani na mashariki, hasa Bagamoyo na kutomtaja kwa heshima Chifu Abushir bin Salim Alharth, aliyepambana na Wajerumani.
Anasema chifu huyo alikuwa na himaya yake iliyoanzia maeneo ya Saadan hadi baadhi ya maeneo ya Mzizima akiwa na askari wake mstari wa mbele akina Diwani, Makanda, Simbambili na Jahazi ambao alinyongwa nao pamoja hadharani mwaka 1888, wakipinga utawala katili wa Kijerumani.
Aidha, kada huyo wa CCM anasema si kweli kuwa Chifu Abushir alijihusisha na biashara ya watumwa, kuwanunua au kuwauza, kwa kuwa hakulijua soko la kuuza watu, wala huko Ulaya na Marekani ambako kizazi cha masalia ya watumwa weusi bado kimelowea, hakukufahamu.
Anasema kilichofanyika katika serikali ya TANU ni kukataza ukabila, udini na kuukwepa mfumo wa serikali za majimbo uliowekwa na wakoloni, ikihofia huenda Tanganyika ingeshindwa kujenga umoja wa kitaifa na mshikamano.
“Watu wasimlishe maneno Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa kudai kuwa alipiga marufuku machifu na uchifu. Yeye mwenyewe ni mtoto wa Chifu Nyerere Burito.
“Machifu wametoa mchango mkubwa sana kuelekea uhuru. Hata baadhi ya machifu walikwenda Umoja wa Mataifa kudai uhuru waliambiwa uhuru hautolewi kwa majimbo,” anasema Abood.
Baadhi ya machifu wa kabila la Kinyakyusa waliokwenda Uingereza kudai uhuru wa nchi yao waliotaka kuiita REPUBLIC OF SOUTHERN HIGHLANDS hawakufanikiwa.
Baadhi ya machifu hao wa kabila la Kinyakyusa ni pamoja na Chifu Mwangobola, Chifu Mwansasu na Chifu Mwanempazi. Wengine ni Chifu Mwakalindile, Chifu Mwakasonda na Chifu Aniagile.