Hivi karibuni Rais John Pombe Magufuli ametoa msimamo kuwa chini ya uongozi wake mwanafunzi yeyote atakayepata mimba akiwa shuleni; shule za msingi na sekondari atafukuzwa shule.
Rais Magufuli amesema wazi kuwa watakaohusika kuwapa mimba watoto nao watafungwa kwa mujibu wa sheria ambayo ni miaka 30 jela. Ameeleza nia ya msimamo huu.

Amesema wapo wanaharakati wanahamasisha jamii ya Tanzania kuvunja maadili yetu kwa kuwapa moyo watoto watakaopata mimba kuwa watarejea shule hali inayoweza kuchochea mfumko wa mimba shuleni.
Amehoji iweje shule ziwe na mama watoto wanaolea watoto, ambapo inaweza kufika wakati nusu ya darasa wanafunzi wakawa wananyonyesha au kulea watoto wakati masomo yanaendelea.

Sisi tumemwelewa Rais Magufuli. Hakika si jambo zuri kuhamamisha watoto wetu kupata mimba wakiwa katika elimu ya msingi na sekondari kwa maelezo kuwa tunalinda haki za binadamu.
Watoto wakipata mimba na umri mdogo inahatarisha maumbile yao na hasa kupata ugonjwa wa fistula, ambao unatokana na maungo yao kutokuwa na uwezo mkubwa wa kubeba ujauzito.

Lakini pia watoto wetu wanastahili fursa ya kusoma bila kusumbuliwa. Tumaani woga ni sehemu ya malezi. Woga huzaa adabu na heshima katika malezi ya watoto. Mtoto akikosa woga, mwisho wa siku anakosa hofu na anaishia kutenda matendo ya ovyo.
Tanzania haipaswi kuruhusu watoto wetu kuishi maisha ya danguro wanapokuwa shuleni. Watoto wetu wanapaswa kutulia wakaitafuta elimu kwanza na wakifikia umari wa mtu mzima, wayasake maisha ya ndoa.

Hata hivyo, wakati tunatoa msimamo huo tunasema si vyema sana kuwafungia milango watoto wote waliopata mimba pasipo kufanya uchambuzi. Wapo watoto wanaoweza kupata mimba kutokana na makosa yaliyo nje ya uwezo wao.
Kwa mfano Rais Magufuli amesema watakaopatikana na kosa la kubaka wafungwe miaka 30 jela. Tunajiuliza je, hawa waliobakwa nao waache shule kwa makosa yasiyokuwa yao? Kwa ajali tu ya kubakwa wapoteze fursa maishani mwao?

Ni katika misingi hiyo tunapendekeza kuwa watakaoandaa kanuni za utekelezaji wa agizo la Rais, wahakikishe kanuni hizi zinaainisha mazingira ya mtoto kupata mimba na ni mazingira yapi ataruhusiwa kurejea shuleni au kufukuzwa shule moja kwa moja ikiwa alipata mimba kwa hiyari.
Vinginevyo, tunasema Rais yuko sahihi, huu si wakati wa watoto kuhamasishwa kuingia katika ndoa kabla ya umri wa maisha hayo kutimia. Mungu ibariki Tanzania.