Wanangu nendeni mkashinde, nendeni mkapeperushe vizuri bendera ya Tanzania, lengo letu iwe ni kushinda tu.” Ni nasaha iliyotolewa na Rais Dk. John Magufuli alipokutana na kuzungumza na wachezaji wa Taifa Stars wiki mbili zilizopita Ikulu, jijini Dar es Salaam. 

Ni nasaha iliyobeba maneno matatu muhimu; kwenda, lengo na ushindi. Si kwa wachezaji tu, bali pia kwa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ambao wote walihudhuria katika mazungumzo hayo wakiwa walezi na wasimamizi wakuu wa Taifa Stars. 

Nimeikubali kwa asilimia mia moja nasaha hii. Kwenda mahali kwingine ni kutafuta, kuchuma au kuvuna. Si kutembea au kutalii. Taifa Stars wanahitajika kuvuna ushindi, si kutalii jijini Maseru. Watambue Watanzania tuna uroho wa magoli na uchu wa ushindi nchini Lesotho.  

Lengo ni azima, ni makusudio yenye mwelekeo wa mtu, umoja au taifa katika mipango ya kujipatia maendeleo katika michezo, uchumi na kadhalika. Katika lengo kuna utashi, umoja na ushirikiano. Taifa Stars mna wajibu mkubwa wa kutimiza lengo letu. 

Ushindi ni furaha na ni kufanikiwa shindano lolote. Ni uthibitisho wa uwezo wa kutenda jambo, si ubwete. “Ushindi una baba wengi, ila kushindwa ni yatima.” (Rais John F. Kennedy – Amerika). Taifa Stars hamna budi kuelewa Watanzania tunahitaji furaha si uyatima.  

Uamuzi wa serikali na vyombo vyake vya michezo nchini wa kupeleka timu Afrika Kusini si kufanya mazoezi ya kucheza ‘singeli’ au ‘kwaito’. Hapana. Ni kwenda kufanya mazoezi ya kabumbu na kuzoea hali ya hewa, kwa minajili ya kupata ushindi tu. 

Maelezo yangu ni kuweka msisitizo juu ya mazungumzo ya Rais Magufuli kwa vijana wetu wa Taifa Stars. Kwa hiyo vijana hamna budi kukiri kushindana kwa lengo la kupata ushindi ambao kwayo asili yake kwanza utoke ndani ya nafsi zenu na ndani ya mioyo yenu. 

Sikumbuki kama kuna historia inayoeleza kwamba nchi ya Lesotho imewahi kuishinda nchi yetu katika soka. Isipokuwa ipo historia ya Tanzania kuishinda Lesotho katika mashindano ya Kombe la Washindi barani Afrika (African Winners’ Cup) mwaka 1977; miaka 41 iliyopita. Iwapo ipo naomba samahani. 

Mwaka huo timu yetu – Dar es Salaam Rangers International (au Mzizima Combine) iliyosimamiwa na Umoja wa Vijana wa TANU (TYL), Mkoa wa Dar es Salaam ilizishinda baadhi ya timu za kombaini za mikoa nchini, Zanzibar Combine na Ndola United ya Zambia. 

Huko Maseru, Lesotho tuliichabanga timu ya Matramah mabao 5 – 1 na walipokuja nchini tuliwabugiza mabao 6 – 0. Ushindi huu ulituwezesha kucheza na timu ya Al Ittihad ya Alexandria, Misri. Kwao tulifungwa mabao 2 – 1 na kwetu tulisuluhu 0 – 0 Uwanja wa Taifa. 

Vijana wetu walikuwa wepesi kupokea mafunzo ya mchezo kutoka kwa Mwalimu (Coach) wao, Shaaban Marijani na kukariri mawaidha ya Meneja wa Timu, Alhaj Ali Said Keto ‘Pwaguzi’. (Wawili hawa sasa ni marehemu) na kuzingatia diplomasia ya mchezo na ya watu kutoka kwa Mkuu wa Timu na Mwanamichezo, Angalieni Mpendu. 

Timu yetu ilikuwa na wachezaji wafuatao; Juma Pondamali, Bernard Madale, Juma Shaaban, Selemani Saidi, Charles Mwanga, Selemani Jongo na Adolph Rishad (Nahodha). Wengine ni Salum Mwinyimkuu, Sam Kampambe, Omari Gumbo, Shaaban Katwila, Yanga Bwanga, Muhaji Muki na Mwinda Ramadhani. 

Kwa timu ya taifa: “Nawapa shilingi milioni 50, nataka zikatumike kuimarisha timu na si kunufaisha viongozi…” (Rais Magufuli). Nawatakia kila la heri na afya njema safarini, kambini na mchezoni. Tunahitaji kula uhondo si kula uvundo.