Wananchi wasisitiza kutumia kwa usahihi miundombinu ya majitaka
JamhuriComments Off on Wananchi wasisitiza kutumia kwa usahihi miundombinu ya majitaka
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph amewataka wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya utumiaji wa mfumo wa mtandao wa majitaka ili kuondokana na adha ya kuziba mara kwa mara kwa mitandao hiyo.
Ameyasema hayo leo Machi 26, 2024 wakati alipotembelea Kata ya Majengo, Mtaa wa Kitenge eneo lililoathiriwa na kujaa kwa majitaka kwa lengo la kukagua na kujionea hali ya mazingira katika eneo hilo.
“Maendeleo yanaenda na mambo mengi na yanagharama kidogo, na gharama yenyewe ndio kama hii, lakini isingekuwa hivi, kama wananchi wanazingatia matumizi sahihi ya mtandao wa majitaka” amesema Mhandisi Aron.
Amesema uzibaji wa mara kwa mara katika mifumo ya majitaka sio kwa sababu ya majitaka kuwa mengi, bali ni kuingizwa kwa vitu na taka ngumu ambavyo vinasababisha mfumo huo kuziba.
“Tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi watumie kwa sahihi mfumo wa majitaka, mfumo wa majitaka ni kwa ajili ya kutumia majitaka tu hata maji ya mvua hayatakiwi kuingia kwenye mfumo huo” amesema Mhandisi Aron.
Nae Diwani wa Kata ya Majengo, Shufaa Ibrahim ameishukuru DUWASA kwa kupokea malalamiko na kufika eneo lenye changamoto ili kujionea hali halisi na kuweza kutatua changamoto hiyo na kuahidi kuitisha mkutano wa wakazi wa eneo hilo na kuwaita wataalamu kutoka DUWASA ili waweze kutoa Elimu ya kutosha kwa wananachi.