Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Njombe

Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi wapatao 32 wamewasili mkoani Njombe kwa kambi ya Siku tano (5) iliyoanza leo Desemba 2 hadi Desemba 6, 2024 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.

Akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa Kambi hiyo, Mkuu wa mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amewataka wananchi wenye matatizo mbalimbali yanayohitaji huduma za Kibingwa na wale wanaohitaji kujua hali ya afya zao, ni vema wakafika mapema katika Hospitali kuliko kusubiri siku za mwisho za kambi.

“Wananchi siku ya kwanza hawaji wanasubiri siku ya nne ndio wanaomba kuongezewa siku za matibabu, sasa ninawaambia wananchi wa Njombe kuwa Madaktari Bingwa wa Mama Samia wako hapa Njombe na tutumie fursa ya uwepo wa Kambi hiii ili madaktari hawa wafanyie kazi changamoto za afya zetu” amesema RC Mtaka. ,

Amesema kuwa uwepo wa Kambi hizi unaakisi uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo ununuzi wa mashine na vifaa vya kisasa, pamoja na ongezeko la wataalam Mabingwa na Bingwa Bobezi.

Amewataka watanzania kukubali na kuthamini uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali na hivyo kupunguza kasumba ya kutafuta matibabu nje ya nchi kwa huduma ambazo zinapatikana katika hospitali kubwa za Serikali hapa nchini.

Kambi ya Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi wa Dkt. Samia itadumu kwa siku tano huku wananchi wa mikoa ya Njombe, Ruvuma, Mbeya na Songwe wakitarajiwa kunufaika na uwepo wa Kambi hiyo kwa Nyanda za juu Kusini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Wizara ya Afya Dkt. Hamad Nyembea amesema kuwa, mbali na kambi hizo kurahisisha utoaji wa huduma za Kibingwa inasaidia kubadilishana uzoefu, na kutoa mafunzo kwa watumishi mbalimbali wa hospitali na hivyo kuongezewa ujuzi mahali pa kazi.