Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma

Wananchi wa Kata ya Ihumwa Jijini Dodoma wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua kali zinazochukuliwa dhidi ya watu wanaofanya uhalifu pamoja na vitendo vya ukatili kwa kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria kwa wakati.

Hayo yameelezwa Disemba 11, 2024 katika Mkutano wa hadhara wa wananchi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) George Katabazi wakati akisikiliza Kero za wananchi hao juu masuala ya ulinzi na usalama katika kata ya Ihumwa ambapo aliambatana na watendaji wake.

Mbali na pongezi hizo kwa Jeshi la Polisi wananchi wa Kata hiyo wameomba hatua zinazochukuliwa ziwe endelevu ili iwe fundisho kwa wahalifu wengine kutokana na kudhibiti mtandao wa uhalifu ulikuwa ukijihusisha na vitendo vya ukatili vilivyokuwa vikileta taharuki katika eneo hilo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wengine, Mussa Zakaria ameeleza umuhimu wa wananchi kishirikiana na Jeshi hilo katika kuwabaini wahalifu ili jamii iwe salama.

“Tunashukuru Jeshi letu lipo imara wakati wote chini ya Kamanda wake Katabazi, tunashuhudia wahalifu wanafikishwa sehemu wanazostahili na sasa wanannchi tuna imani na Jeshi letu na tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha jamii yetu inakuwa na amani bila kubughudhiwa na waovu, “ameeleza.

Kutokana na hayo Kamanda wa Polisi mkoani hapa George Katabazi ametumia nafasi hiyo kuwataka wazazi na walezi kusimama imara katika malezi na kufuatilia mienendo ya watoto ili kuepuka kutokea kwa vitendo viovu ambavyo huchagizwa na mmomonyoko wa maadili na kuingia katika wimbi la uhalifu.

Kamanda Katabazi amekemea baadhi ya vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wananchi hao vya kuwaficha wahalifu ambao wapo miongoni mwao kwa kuhofia kutoa taarifa za watoto wao huku akihimiza ushirikiano wa pamoja ili kuweza kuzuia na kutanzua uhalifu katika jamii.

Katika hatua nyengine Kamanda Katabazi ametembelea ujenzi wa kituo cha Polisi Kata ya Ihumwa kinacho jengwa Kwa nguvu ya wananchi na kupongeza Kwa hatua walizofikia na kuahidi kuunga mkono jitihada hizo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma pindi kitakapo kamilika.