Wananchi wa maeneo ya Kinyerezi, Chalinze na Tanga waliohamishwa kupisha mradi wa umeme wa North, East, Grid wa (Kv 400), wameilalamikia serikali kwa kushindwa kuwalipa fidia licha ya zoezi la uhakiki wa maeneo hayo kukamilika tangu mwaka 2015.

Wakizungumza na Gazeti la JAMHURI kwa nyakati tofauti, wamesema ukimya wa serikali juu ya jambo hilo tangu mwaka 2015 umekuwa kama msiba kwao kiasi cha  kusababisha wengine mali zao kupigwa mnada na taasisi za kifedha zilizowakopesha kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwenye maeneo hayo.

Wamesema kucheleweshwa kulipwa fidia kumezirudisha baadhi ya familia nyuma kimaendeleo kiasi cha  kushindwa kujenga makazi mapya baada ya kubomoa zile nyumba za awali kupisha mradi  tangu mwaka 2015.

Leonard Kishato, mkazi wa Kinyerezi anasema tangu kuhamishwa kupisha mradi huo maisha yake yamegeuka kuwa ya shida na kujikuta akishindwa kutimiza majukumu yake kama baba wa familia.

Anasema kabla ya kuhamishwa alikuwa  na mradi wa kilimo cha nyasi katika maeneo hayo, lakini alilazimika kusitisha tangu mwaka 2015 baada ya serikali kutangaza kuyachukua maeneo hayo kwa ajili ya mradi  wa umeme wa North, East, Grid wa (Kv 400).

“Kabla ya maamuzi ya serikali nilikuwa nalima kilimo cha kupanda nyasi kwa ajili ya mifugo kwa fedha ya mkopo, hata hivyo kutokana na amri ya serikali ya kusitisha shughuli za kimaendeleo, nyumba yangu tayari iko hatarini kupigwa mnada na taasisi za kifedha, ” anasema Kishato.

Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Peru, Chalinze, Mkoa wa Pwani, Nuru Pingo, amesema licha ya miaka mitatu kupita tangu kukamilika kwa zoezi la tathmini ya maeneo yao lakini ukimya wa serikali ni kama janga kwao.

“Mimi ni mmoja wa watu waliofanyiwa tathmini tangu mwaka 2015 kutokana na ukimya huo wa serikali nyumba yangu ya familia tayari imo shakani kupigwa mnada kulipia deni la benki baada ya kushindwa kulipa deni, ” anasema Pingo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Makweza, Chalinze, Mkoa wa Pwani, Ole Sokoti, amesema wakazi wa maeneo hayo wameendelea kuhangaika kwa kukosa maeneo ya kilimo baada ya maeneo yao kuchukuliwa kupisha mradi.

Amesema asilimia kubwa ya maeneo yaliyochukuliwa ni mashamba yaliyokuwa yakitumiwa na wananchi kwa shuguli za kilimo, ufugaji na mambo mengine ya kimaendeleo.

Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, alipoulizwa juu ya malalamiko ya wananchi hao amekiri kuyafahamu na kusema: “Kwa sasa sina jibu linalojitosheleza juu ya fidia hiyo, ninaloweza kusema, naomba unipe muda niweze kulifuatilia kwa undani nione limefikia wapi.”

Msimamizi wa miradi  kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Khalid James, anasema serikali inakamilisha taratibu za  kuwalipa wananchi wanaodai na inatarajia kuanza kulipa kuanzia  kipande cha  Kinyerezi hadi Chalinze na kufuatiwa na maeneo mengine katika mwaka huu wa fedha.

Amesema Wizara ya Fedha na Mipango tayari imekamilisha ulipaji wa  fidia ya  maeneo mbalimbali  nchini na kuongeza kuwa maeneo mengine ambayo bado taratibu za kifedha zinafanyika.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amekiri kuyafahamu na kusema wananchi hao waendelee kuwa na moyo wa subira wakati huu ambapo serikali inakamilisha taratibu za kifedha ili walipwe.

 “Serikali tayari imeshalipa fidia ya wananchi wa  Singida – Namanga na wale wa Bunlyanhulu  – Geita, kupisha miradi ya kimaendeleo kama hiyo ya Kinyerezi na kwingine,” anasema Mgalu.

Anasema ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma unautegemea mradi huo kwa ajili ya  kuendesha treni ya kisasa na kuongeza kuwa tayari serikali imekwisha kutenga zaidi ya shilingi bilioni 21 kwa ajili ya ulipaji wa fidia.

Anasema pamoja na  miradi hiyo ya kutoka Kinyerezi – Chalinze – Segera – Tanga pia kuna  msongo wa kilovoti 220 kutoka Bulyankulu – Geita – Nyakanazi – Lusumo na ule wa kilovoti 400 kutoka Singida – Arusha – Namanga inayotekelezwa kwa wakati mmoja.