Na Mwandishi Wetu, JAMHURI MEDIA
Wananchi zaidi ya 2,000 wa Kijiji cha Nyeburu, Kata ya Chanika, wanajiandaa kuvamia upya eneo lililomegwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) ili kuendeleza shughuli zao za kila siku, kwa madai serikali imeshindwa kutatua mgogoro wa mpaka kati yao na hifadhi ya Msitu wa Kazimzumbwi.
Wakizungumza na JAMHURI hivi karibuni wanasema hatua ya wao kuvamia eneo lililo karibu na hifadhi ya Msitu wa Kazimzumbwi unaotenganisha Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam ni baada ya shughuli ya ubainishaji na uwekaji wa alama za mpaka inayofanywa na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi upande unaopakana na Jiji la Dar es Salaam kuwa batili.
“Tunaona ofisi ya Kamishna inaendesha shughuli hii kwa ubabaishaji. Kwanza hatujashirikishwa, halafu upimaji unafanyika mlemle tunamolalamikia tangu mwanzo. Tumemwandikia barua kamishna tujue kwa nini anarejesha mipaka ileile hajatujibu.
“Pia tumemwandikia barua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Amos Makalla, tukimtaka kusitisha shughuli hii kwa sababu si halali, anatujibu majibu mkanganyiko,” anasema Charles Kang’ombe, katibu wa kamati inayofuatilia mgogoro huo katika ofisi za serikali.
Kang’ombe anasema wanafikiria kurejea kwenye maeneo yao baada ya kufuatilia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakabaini hakuna mabadiliko mapya ya michoro ya ramani iliyokuwapo awali na mpaka mpya uliowekwa na TFS.
“Mpaka mpya wa TFS si sahihi, ni mpaka wa kulazimishwa, tumefika Ofisi ya Waziri Mkuu tukitaka tuthibitishiwe kama kuna ramani au GN mpya, tumezungumza na wataalamu wa ardhi wametuthibitishia wazi kuwa GN sahihi ni iliyotangazwa mwaka 1954, ambayo ni GN 306, ramani Na. JB 196 ambayo hadi leo haijafanyiwa mabadiliko,” anasema.
Kang’ombe anaongeza kuwa wanalenga kurejea kwenye maeneo hayo ili kuishinikiza serikali kufuata ushauri wa wataalamu wa Wizara ya Ardhi ambao baada ya kulifuatilia eneo hilo walibaini kuwapo mipaka miwili; mmoja ukiwa ule wa zamani na mpya ambao umewekwa na TFS, ambapo hata hivyo walishauri serikali itangaze mpaka mmoja tu ambao unafaa kutumika.
“Vijiji ambavyo maeneo yao yalimegwa kwa sababu ya kuwa kwenye eneo la hifadhi ni Vibura na Maguruwe, sisi wakazi wa Nyeburu hatukumegwa, isipokuwa wakati wa utekelezaji wa kuwaondoa wananchi waliomegwa baada ya kushindwa kesi mahakamani kijiji chetu nacho kikajumlishwa humo,” anasema Kang’ombe.
Anadai kijiji hicho hakikuwa sehemu ya mgogoro lakini anadai sababu ya kusadikiwa kuwa kipo kwenye eneo lenye madini aina ya kaolin kuna watu wachache serikalini wana masilahi binafsi kuhusu eneo hilo, na kwamba ndio watengeneza mgogoro.
Kang’ombe pamoja na wenzake wanailaumu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC) wakidai imeshindwa kutatua mgogoro wao kwa hoja zisizo na mashiko, ikiwamo ya mgogoro wao kuwa mahakamani.
Mgogoro huo umetimiza miaka 29 sasa na rasmi anasema ulianza mwaka 1994 mara baada ya TFS kuhamisha mpaka wa zamani kwa kuusogeza kwenye makazi ya watu, huku akiitaja operesheni iliyofanywa na serikali mwaka 1998 kuwaondoa wananchi ilizaa matunda baada ya kufikishana mahakamani.
Mwenyekiti wa Kamati ya waathirika wa mgogoro huo, Bakari Msafiri, anasema mwaka 2011 rasmi serikali ilianza kuwaondoa wananchi waliotajwa kuvamia hifadhi lakini wakazi wa Nyeburu ikalazimika kuwatoa kimabavu kwa kutumia Jeshi la Polisi kwa sababu wao wanadai hawakuwa ndani ya mpaka halisi wa hifadhi.
“Tukio la mwaka huo nadhani kila mkazi wa Nyeburu analikumbuka, limetuacha kwenye dimbwi la umaskini.
“Kila familia kwa kipindi hicho ilikuwa na mifugo; kuku, mbuzi na ng’ombe lakini leo ukituuliza ilikwenda wapi mifugo yetu hatufahamu, si kwamba iliuawa, la hasha! Mizogo tungeiona. Waliotuvamia siku hiyo waliharibu na kuiba baadhi ya mali zetu,” anasema Msafiri huku akibainisha kwamba hadi mihogo ilichimbwa mashambani wakaondoka nayo.
Awali kabla ya kuzuka vurugu za kuondolewa kinguvu anasema aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe kwa kipindi hicho aliitisha mkutano uliohusisha wananchi pamoja na TFS na kutamka kuwa waliovamia kwenye hifadhi ya msitu wanatakiwa kuondoka ndani ya siku tatu.
“Tulidhani tamko linavihusu vijiji vingine, hatukujua na sisi linatuhusu. Tulikaa kwa amani ndani ya siku tatu, lakini zilipokwisha, ghafla askari polisi waliobeba kila aina ya silaha wakiongozwa na DC walituvamia na kuanza kuchoma nyumba, kutupiga na kusambaratisha kila kitu,” anasema Msafiri.
Anadokeza kwamba wananchi baada ya kusambaratishwa walikimbilia Mtaa wa Tariani kuomba hifadhi kwa muda na wakiwa mtaani hapo walijikusanya wakafanya kikao miongoni mwao wakaandamana hadi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambako walikutana na aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo Profesa Ana Ntibaijuka akawaahidi kutatua suala lao.
“Waziri alilifanyia kazi suala letu na Mei 25, mwaka 2012 alitoa tamko bungeni akisema Waziri wa Maliasili na Utalii wa kipindi hicho, Balozi Hamis Kagasheki na watu wake walifanya makosa wakati wa kutekeleza upimaji wa hifadhi ya msitu.
“Alitamka wazi kuwa upimaji uliacha nyuma eneo la hifadhi takriban mita 900 na kuingia eneo la wananchi mita 800 kwa upande wa mashariki ya Wilaya ya Kisarawe,” anasema.
Baada ya wananchi wa Nyeburu kulisikia tamko hilo waliandika barua kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi wakiomba awahakikishie ukweli wa tamko hilo na katibu mkuu akawajibu kwa barua kuwa ni la kweli, huku akiwashauri kulitumia kama kielelezo endapo wataamua kutumia vyombo vya sheria.
“Tulivyopata uhakika huo tulirejea tena kwenye maeneo yetu tukiamini mgogoro umekwisha, Desemba 28, 2014 ni siku nyingine ambayo tulipokea notisi ya siku tatu kutoka TFS ikitutaka tuondoke. Siku tatu hazikwisha, siku ya pili tu magari manane yaliyojaa askari wa kutuliza ghasia maarufu FFU walifika na kutufanyia kila aina ya uharibifu,” anasema.
Anaitaja familia moja iliyokuwa na mjamzito kwamba katika vurugu hizo alifariki dunia baada ya kuanguka kwenye matuta ya viazi wakati akikimbia vipigo vya skari hao.
Anasema kwa mara nyingine wakaifuata Wizara ya Ardhi ili kupata ufafanuzi lakini ikapata kigugumizi katika kuwajibu na kwamba mwaka 2015 walikaa kikao na aliyekuwa Naibu Waziri wa wizara hiyo, Angeline Mabula, wakamweleza juu ya mgogoro wao, naye akaahidi kuushughulikia.
Anasema Agosti, mwaka huo wataalamu kutoka wizarani walifika Nyeburu kufanya uhakiki kwa muda wa siku nne, lakini hadi leo hawajatoa majibu ya upimaji walioufanya.
“Kule wizarani kuna mtu alituonyesha makabrasha ya mgogoro wetu tukaona majibu ya timu ya Mabula, hayakuwa tofauti na majibu ya timu ya Profesa Tibaijuka,” anasema.
Baada ya kuchungulia majibu hayo, Msafiri anasema Januari, 2017 walihamasishana tena wakarejea kwenye maeneo yao lakini ilipofika Julai 30, Jeshi la Polisi liliwavamia na kufanya uharibifu kwa mara nyingine.
Msafiri anasema baada ya kuona mbinu ya kurejea kwenye maeneo yao imeshindikana wakaamua kuandika barua kwenda ofisi ya Tume ya Maadili ya Viongozi kwa Umma, barua hiyo haikujibiwa, badala yake walipewa mwongozo kwa mdomo namna ya kupata haki yao.
Waliandika barua nyingine Wizara ya Maliasili na Utalii, napo wakawajibu kwamba serikali imeshinda kesi mahakamani hivyo wao hawana haki.
“Tulikwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nako tukajibiwa kuwa tuna kesi mahakamani, tukawaambia hatuna kesi, wakaanza kututishia amani,” anasema Msafiri huku akidai ofisi hiyo imekuwa kikwazo kwa wao kupata haki.
Amina Lugiga ni mwathirika wa vurugu za kuhamishwa katika eneo hilo na sasa anamlaumu RC Makalla akidai ameshindwa kuwatatulia matatizo yao.
“Mwezi Februari mwaka huu alitueleza kuwa wananchi wa Nyeburu tusiwe na wasiwasi analishughulikia suala letu la mpaka, alituhakikishia mpaka utakuwa ule ule wa mwaka 1954. Cha ajabu watu wa Wizara ya Ardhi wamekuja na kulazimisha kurejesha mpaka pale pale penye mgogoro baina yetu na TFS,” anasema Amina.
Anadai ofisi za serikali zinawazungusha tu hivyo wanajiandaa kurejea kwenye maeneo yao huku akiiomba Ofisi ya Rais kuingilia kati mgogoro wao kwani ofisi nyingine za serikali zimeshindwa kuutatua.
JAMHURI limefika ofisini kwa RC Makalla na kuelezwa na Katibu wake, Raphael Kilave, kuwa mgogoro huo wamejaribu kuutatua kupitia mabaraza ya ardhi ikashindikana, sasa umefikishwa ngazi ya baraza la mawaziri, hivyo hawezi kuuzungumzia kwa kina.
Nayo Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam JAMHURI limeifikishia malalamiko ya wananchi hao lakini haikutoa nafasi ya kuuzungumzia wala kujibu ujumbe wa maandishi uliotumwa kwa Kamishna wa Ardhi kwa njia ya Whatsapp.