Mvutano umeibuka kati ya serikali na wakazi wa Kata ya Nyatwari, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara baada ya wananchi hao kutakiwa kuhama huku wao wakipinga amri hiyo.
Wananchi hao wametakiwa kuondoka kwenye kata hiyo ili kupisha njia ya wanyama wanaotoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwenda kunywa maji Ziwa Victoria.
Februari 21, mwaka huu, mamia ya wakazi wa Nyatwari waliapa kwa sauti huku wakiwa wamenyoosha mikono yao juu, kutokuhama makazi yao katika eneo hilo.
Kiapo hicho kilifanyika kwenye mkutano wa hadhara mbele ya Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Ester Bulaya, aliyefika kusikiliza kero zao kabla hajaelekea kwenye vikao vya Bunge la Bajeti la mwaka 2019/2020.
Wakizungumza mkutanoni hapo, baadhi ya wananchi wa kata hiyo wamesema hawawezi kuacha makaburi ya babu, bibi na ndugu zao na kuhamia kwingine.
“Mwaka 1969 Baba wa Taifa Julius Nyerere alitupa hati ya Nyatwari. Alikuja akaweka shamba lake hapa. Serikali ibadili uamuzi. Hatutaki kutoka hapa. Tuna makaburi tumezika ndugu zetu hapa halafu eti tuhame, hatutaki,” amesema Johua Marwa.
Moshi Bakari, mkazi wa kata hiyo ametaka viongozi wa serikali kumuenzi Nyerere kwa vitendo, kwa kuheshimu uamuzi wake wa kutoa hati katika eneo hilo.
Amesema habari za wao kutaka kuhamishiwa maeneo mengine hawataki kuzisikia, kwani babu zao wameishi hapo karne iliyopita.
Nyatwari inayoundwa na vijiji vitatu vya Tamau, Serengeti na Nyatwari, inapakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Kata hiyo kongwe inakadiriwa kuwa na wakazi 5,000 hadi 7,000.
“Sisi hatuhami hapa,” alisema Bakari aliyeshangiliwa na umati wa watu waliohudhuria mkutano huo.
Lakini, Hevock Malagila, kwa upande wake anasema iwapo serikali imeamua kuwaondoa, lazima wahame kupisha wanyama.
Ingawa Malagila alikumbana na kelele za kumzomea, wakati akiunga mkono hoja ya serikali kutaka kuwahamisha, alisema:
“Waziri Lukuvi amekuja hapa na timu yake, ametuambia fedha ipo ya kulipa fidia na maeneo ya kutupeleka yapo.”
Hata hivyo, wananchi walimzomea, hali iliyomlazimu kukatisha mazungumzo yake na kukaa.
Kwa upande wake, Andrew Malulu, mkazi wa Nyatwari, amesema kijiji hicho kilitumiwa na Mwalimu Nyerere kuomba Uhuru wa Tanganyika.
Amesema wakati huo alikuwa akipenda kwenda kusisitiza uhuru na kazi eneo la mashineni, hivyo kutaka kuwaondoa ni dhambi.
“Sisi tunasema hatuhami hapa. Kawaambie hivyo,” amesema Malulu akimwambia Mbunge Bulaya mkutanoni hapo.
Malulu ameeleza kuwa Nyatwari inapaswa kupewa hadhi ya kuwa makumbusho ya taifa kulingana na historia yake.
“Nyatwari ilikuwapo tangu mwaka 1700. Ni kijiji cha asili ambacho Baba wa Taifa alikipatia hati kamili. Sisi hatujavamia hifadhi, tulikuwapo tangu zamani.
“Mwaka 1974 kiliandikishwa kijiji cha Ujamaa. Kisiondolewe na kuletwa watalii Wazungu hawa wavaa kaptura ,” anasisitiza mkazi huyo na kushangiliwa na umati wa watu.
Wakati wananchi wakitoa msimamo wao huo, serikali nayo imekwisha kubainisha kwamba maeneo ya kuwahamishia raia hao yapo.
Februari 17, mwaka huu timu ya mawaziri iliyoundwa na Rais John Magufuli kuzunguka nchi nzima kutatua migogoro ya ardhi ilizuru na kufanya mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Nyatwari.
Katika mkutano huo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alieleza kuwa fedha na maeneo ya kuwahamishia wananchi ni masuala yaliyokwisha kukamilika.
Mbunge Bulaya
Akizungumza mbele ya umati huo, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, alisema haegemei upande wowote katika sakata hilo.
Aliwataka wananchi waliokuwapo mkutanoni hapo kupiga kura ya wazi, kujua wanaotaka kulipwa fidia wahame na wasiotaka kuhama, ili kukata mzizi wa fitina.
Mbunge huyo machachari, alisema watakachoamua wananchi juu ya hatima ya makazi yao atakiwasilisha bungeni.
Bulaya alihoji: “Wanaosema wanataka kuhama wanyooshe mikono juu (hakuna aliyenyoosha mkono). Wanaotaka walipwe waondoke nyoosheni mikono (hakuna aliyenyoosha).
“Wale ambao hawataki kuhama mikono juu (wananchi wote mkutanoni walinyoosha mikono).”
Mwandishi wa Gazeti hili la JAMHURI alishuhudia namna wananchi walivyokuwa wakipinga agizo hilo la serikali wakati wa mkutano huo.
Na kwa mujibu wa Bulaya, suala la wananchi kuhama au kutokuhama, hataliingilia, ingawa anaheshimu uamuzi uliofikiwa na wananchi.
“Najua masuala haya ya fidia yalishindikana Kigamboni. Dk. Ndugulile (Faustine – Mbunge wa Kigamboni) alikomaa hadi sasa wanaishi, hawakuondolewa.
“Kawe pale, Halima Mdee, naye alikomaa na hawakuondolewa. Badala yake wamepimiwa maeneo yao na kurasimishwa kuwa makazi rasmi ya watu,” amesema Bulaya.
Msimamo wa Serikali
Wakati hayo yakijiri, serikali imesema suala la wananchi wa Nyatwari kuyahama makazi yao liko pale pale.
Akizungumza na JAMHURI kuhusu msimamo huo wa wananchi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu, anasema lazima waondoke.
“Msimamo wetu kama serikali, lazima waondoke. Tulishatenga fedha nyingi tu kuwafidia. Hiyo ni sholoba (mapito) ya wanyama kwenda kunywa maji ziwani.
“Ieleweke kwamba ardhi ni mali ya serikali kwa mujibu wa sheria zetu,” Waziri Kanyasu alisema, akikumbusha kuhusu matakwa ya sheria.
Alipoulizwa ni lini serikali itaanza kuwalipa fidia wananchi hao, na wapi watapata makazi yao mapya, Waziri Kanyasu alisema: “Tutaanza kuwalipa mwaka ujao wa bajeti. Wakishalipwa fidia kila mtu atafute pa kwenda kuishi.”