Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wananchi wanaojitokeza katika banda la Mama Samia Legal Aid Campaign katika maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaama (DITF), kupata msaada wa kisheria wamefurahia huduma hiyo huku wakieleza itasaidia kukuza upatikaji wa haki.

Kampeni hiyo inayosimamiwa na Wizara ya Katiba na sheria ilianza mwaka 2023 na itadumu kwa kipindi cha miaka mitatu ikiwa na lengo la kutoa ushauri na kuongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu kwa jamii hususan haki za wanawake na watoto.

Wakizungumza na Mwananchi baada ya kutembelea banda hilo,Wananchi hao kwa nyakati tofauti wamesema kwa muda mrefu walikosa elimu ya namna ya kutafuta haki zao mathalani katika eneo la migogoro ya ardhi.

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo akimuhudumia mkazi wa mbangala Bw.Yunus Lilingani

“Tunashauri na kupewa elimu,nimefurahi kwakuwa nilikuwa na mgogoro wa ardhi nimewaelezea na wanasema watanisaidia namna ya kusuluhisha,”amesema John Salva

Kwa upande wake Mariam Said amebainisha kampeni kama hizo zinasaidia kufumbua akili wengi hasa wananchi waliokata tamaa katika kufuatilia haki zao.

“Tunatoka katika familia ambazo familia zetu hazijasoma na tunakosa watu wakutusaidia sasa kupitia kampeni kama hii ya Mama Samia Legal Aid itakuwa na msaada mkubwa kuinua haki zilizokuwa mbioni kutoweka kwa walala hoi,”amesema.

Wakati wakieleza hayo, Kaimu Mkrugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi amesema wananchi 490,000 kutoka mikoa saba wameshanufaika na kampeni hiyo.

“Eneo la migogoro ya ardhi linaongoza. Kwa hiyo Wizara iliona umuhimu wa kuleta kampeni hii ya kitaifa ya msaada wa kisheria ambayo imepewa jina mama Samia legal Aid Campain katika maonesho haya ya sabasaba kutokana na umuhimu wake katika kutatua migogoro ya wananchi na kampeni hii inatolewa bure,”amesema Ester

Amesema kampeni hiyo imejikita katika kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi hususan katika masuala ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi, usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala, na masuala yahusuyo haki za binadamu kwa ujumla.

“Utekelezaji wa kampeni unafanyika kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi za Serikali, Asasi za Kiraia, Wanazuoni na wadau wa Maendeleo. Inatoa huduma ya ushauri wa kisheria na unasihi kwa waathirika na manusura wa ukatili wa kijinsia; kuongeza uelewa kwa wananchi,”amesema.