• • Wachomewa  nyumba, waibiwa vitu 
  • • Polisi wahusika kusimamia uchomaji nyumba

KIBAHA

Na Mwandishi Wetu 

Wananchi wa Lupunga, Kibaha mkoani Pwani, wameuomba uongozi wa wilaya kuingilia kati kutatua mgogoro kati yao na mwekezaji mwenye asili ya Uarabuni kabla damu haijamwagika.

Inadaiwa kuwa Septemba 27, mwaka huu, Mwarabu huyo akiandamana na askari Polisi wamechoma moto nyumba na mashamba ya wanakijiji, wakachukua na kuondoka na mali mbalimbali na kuwasababishia hasara kubwa.

Mkazi mmoja, mzaliwa wa Lupunga, Saidi Pazi (80), anasema maisha yake yote ameishi hapo na familia yake kabla ya uvamizi wa Mwarabu.

“Ninakumbuka kwamba mwaka 1983 alikuja mtu mmoja anaitwa Abdallah mwenye asili ya Kiarabu, akaomba sehemu ya kufanya makazi. Wanakijiji tukaridhia ugeni huo na wala yeye hakuwa mtu wa kwanza kuomba sehemu ya kufanya makazi,” anasema.

Eneo hilo kuna Watanzania wengi wenye asili ya Kiarabu wanaoishi pamoja na wazawa kama ndugu.

Mzee Pazi anasema Abdallah alilima eneo alilopewa bila kupanda kitu.

“Baada ya Abdallah kufariki dunia, akaja Mwarabu mmoja na kujitambulisha kama mdogo wa marehemu. Akataka aonyeshwe mipaka ya eneo la kaka yake. Tukamwonyesha. 

“Lakini sasa amebadilika na anakuja kwa dhuluma, akitumia nguvu kutunyang’anya maeneo yetu tofauti na eneo ambalo kaka yake alipewa na kijiji. Anachofanya sasa ni dhuluma kwa wananchi,” anasema mzee Pazi.

Akizungumza na JAMHURI, Shomari Msasalo, ambaye pia ni mwenyeji wa kijijini hapo, anasema eneo linalogombewa ni mali ya babu yake, anayemtaja kwa jina la Msasalo.

“Hatujawahi kumuuzia mtu na humu kuna makaburi ya asili. Ni eneo letu la maziko.

“Alipokuja hapa Abdallah, kaka yake Mwarabu mwaka 1983 kuomba eneo la kuishi, tulimpa ekari nne tu,” anasema Shomari, aliyezaliwa mwaka 1942.

Anasema wazazi wake na mababu wote wamezaliwa hapo na kuzikwa hapo hapo, akisema mipaka ya eneo asilia la Abdallah ipo wazi na inafahamika.

Shomari anasema ujio wa Abdallah kijijini hapo ulipokewa kwa furaha na wanakijiji kiasi cha hata kufanya sherehe za kumkaribisha.

Anasema mambo yalibadilika baada ya kifo cha Abdallah na ujio wa mdogo wake aliyeamua kwa makusudi kutotambua mipaka ya eneo la kaka yake.

“Ameingia katika mashamba ya wanavijiji na kuyapora, akisema maeneo yote ni yake! Hii si kweli. Na bahati mbaya akiitwa alete nyaraka kuhalalisha umiliki wake, hataki!

“Haiwezekani hata makaburi ambayo mimi nimezaliwa na kuyakuta kuwa leo yapo kwenye eneo lake. Ndiyo maana tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan atusaidie kwa sababu hakuna hata kiongozi mmoja aliyewahi kuja kusikiliza matatizo yetu,” anasema Shomari.

Mzaliwa mwingine wa Lupunga, Fadhili Mohamed, ameliambia JAMHURI kuwa eneo aliloporwa na Mwarabu amelirithi kutoka kwa Msasalo, ambaye yeye pia ni babu yake.

“Tunacholalamikia ni Mwarabu kuja kuchukua maeneo yetu yenye mikorosho ya asili na makaburi. Tunaumia sana kuona makazi yetu yanavamiwa na mtu asiyejulikana,” anasema Mohamed.

Anaelekeza kilio kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kwa kutowapa ushirikiano wa kutosha na kuleta suluhu katika suala hilo ingawa taarifa wanazo.  

“Huyu Mwarabu alipoamza chokochoko, serikali ya kijiji ilimwita akitakiwa kupeleka uthibitisho wa kumiliki eneo hili, alishindwa. Akaondoka akisema ameuziwa eneo hilo na mkuu wa wilaya wa zamani,” anasema.

Sasa wanakijiji wanaomba uongozi wa wilaya au mkuu wa wilaya wa zamani (wanamtaja jina) waende kuthibitisha mauzo ya eneo hilo kwa Mwarabu.

Tatu Mbegu, mwanamke na mkazi wa kijiji hicho, anasema: “Mimi ni mmoja wa wanawake walioathiriwa na kutiwa umaskini na Mwarabu huyu.

“Siku ya tukio (la mashamba na nyumba kuchomwa moto) Mwarabu alikuja na askari wenye bunduki pamoja na vijana wake, wakabomoa na kuiba kuku wangu, magodoro na vitu vingine vingi. 

“Kwa kweli Mwarabu amenitia umaskini mkubwa na sasa watoto wa shule hawana vitabu! Tunalala kwenye vibanda kama wakimbizi.”

Anasema siku ya pili, Mwarabu akiwa na wajukuu wake alikwenda tena kijini hapo kuwaonyesha wajukuu wake eneo analodai ni la kwao.

“Wakati sisi na watoto wetu tunataabika, yeye akawa anawaambia wajukuu wake; ‘mmeona eneo lenu? Ni hili lote.’ Kisha akaja kwetu na kutamba akitutaka kuondoka katika eneo lake.

“Tunaomba serikali ije kusawazisha mgogoro huu vinginevyo atakapokuja tena kuvunja nyumba zetu tutalazimika kujipanga na kumzuia,” anasema Tatu.

Mwenyekiti (mstaafu) wa Lupunga, Saidi Omary, anakiri kulifuhamu sakata la Mwarabu na wanakijiji tangu akiwa kiongozi.

“Alipoanza tu, mimi na diwani mmoja ambaye sasa ni marehemu tulimwita atuletee nyaraka za umiliki wa eneo. Akasema hana na kwamba amepewa eneo na mkuu wa wilaya.

“Tukasema tunachotaka ni nyaraka. Akaondoka na hakurudi tena hadi mwaka huu alipokuja kuvunja nyumba za watu na kuiba vitu mbalimbali,” anasema Omary. 

Kauli yake inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Kitongoji, Abdallah Selemani, akisema inaonekana kwamba Mwarabu huyo hana nyaraka za umiliki wa eneo.

Selemani anasema hata yeye pia ameshamwita ofisini mara kadhaa bila mafanikio.

“Mimi nilitaka kumuunganisha na wananchi lakini hataki! Ofisi yangu haimtambui mtu huyu, hayumo katika orodha ya wamiliki,” anasema.

Anasema siku ya tukio alimfuata akamsaidia kuwaondoa wananchi, huku akiwa na askari wenye silaha, akakataa. 

Selemani anasema askari hao walikwenda wenyewe na yeye akampigia simu mtendaji wa kata kumuuliza kama ana taarifa za mtu huyo na ujio wake, lakini hata mtendaji akasema hamtambui na kumsihi Selemani kutojiingiza katika sakata hilo.

Polisi Pwani haina taarifa

JAMHURI limemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa, kutaka kufahamu iwapo jeshi hilo lina taarifa za kuwapo kwa suala hilo.

Afande Nyigesa anasema hana taarifa zozote kuhusu tukio hilo na kuahidi kulifuatilia.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Butamo Ndalahwa, anasema wakati taarifa zikifikishwa ofisini kwake, hakuwapo.

“Hata hivyo mimi na timu yangu tutakwenda huko Jumatatu (jana) na kumaliza suala hilo,” anaahidi Ndalahwa.

JAMHURI limemtafuta pia Mwarabu anayedaiwa kumiliki eneo hilo.

Hata hivyo, baada ya simu kupokewa na mwandishi wa habari hii kujitambulisha, mtu aliyepokea akajibu akisema Mwarabu huyo hayupo nchini kwa sasa.

Umiliki wa Mwarabu katika eneo hilo pia unakanwa na Mtendaji wa Kata, Palekege Jailos, akisema ofisini kwake hakuna taarifa za Mwarabu kumiliki eneo hilo linalodhaniwa kuwa na ukubwa wa zaidi ya ekari 1,000.

“Nilipozungumza naye aliniambia eneo hilo alipewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati hakukuwa na uongozi wa serikali,” anasema Palekege.

Palekege anasema baada ya uharibifu wa mali za wananchi kufanyika, aliandika barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya lakini hadi alipozungumza na JAMHURI hakuwa amepata majibu.